Jumatano, 8 Mei 2019

WAZIRI NDALICHAKO AIPONGEZA UDSM KWA KUTENGA BILIONI MOJA ZA KUENDELEZA UTAFITI


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ameupongeza uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kutenga kiasi cha shilingi bilioni moja katika bajeti yake ya mwaka 2019/20 kwa ajili ya kutoa fursa kwa  wahadhiri na wanafunzi kendeleza tafiti

Waziri Ndalichako ametoa pongezi hizo jijini Dar es Salaam wakati akifunga maadhimisho ya tano ya Wiki ya Utafiti ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo amesema utafiti una mchango katika ukuaji wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akihutubia washiriki wa maadhimisho ya tano ya Wiki ya Utafiti ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati wa kufunga Wiki hiyo jijini Dar es Salaam

Prof. Ndalichako amesema serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda lengo likiwa kuhakikisha kunakuwa na viwanda ambavyo vinatumika kuzalisha bidhaa na kutoa huduma zitakazotosheleza jamii ya Kitanzania na kusaidia kuongeza ajira kwa vijana.

“Serikali kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia ilizipatia Taasisi nane za Tanzania Bara kiasi cha shilingi bilioni tatu na milioni mia mbili wakati upande wa Zanzibari shilingi milioni 960 zilitolewa kwa ajili ya utafiti, Taasisi hizo zilishinda uandishi wa tungo za miradi ya uboreshaji wa miundombinu ambayo ina uwezo wa kutoa mchango madhubuti katika Dira ya nchi yetu ya uendeshaji wa viwanda kwa lengo la kuimarisha uchumi wa nchi yetu” amesisitiza Waziri Ndalichako.

Akizungumzia Wiki ya Utafiti Waziri Ndalichako amesema inawapa wadau wa utafiti na ubunifu jukwaa la kufahamu aina za shughuli za utafiti zinazofanyika; sehemu gani kuna mapengo na changamoto; na mikakati gani ya kimipango inahitajika ili kuziba mapengo pamoja na kutatua changamoto zilizobainika.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikabidhi tunzo kwa washindi wa auandishi wa miradi ya tafiti wakati wa kufunga  maadhimisho ya tano ya Wiki ya Utafiti ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. 

"Kama taifa, tuna wajibu mkubwa na fursa nyingi za kuweza kutumia utafiti, ubunifu na ujasiriamali hususan kupitia sekta ya elimu ili kuongeza kasi ya maendeleo ya viwanda nchini. Kwa kufanya hivyo, kutawezesha kutekeleza azma ya Serikali ya awamu ya tano ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Dira ya Taifa ya 2015, ya kuhakikisha kuwa Tanzania inafikia hadhi ya kuwa na uchumi wa kati na unaoendeshwa na sekta ya viwanda," amesisitiza Waziri Ndalichako.

Aidha, Waziri amesema wizara imeandaa mwongozo wa kutamba na kuendeleza ugunduzi, ubunifu na maarifa hasilia nchini ili kujenga na kukuza hamasa ya matmizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika shughuli za jamii na maendeleo na hivyo kuongeza mchango wake katika uchumi wa nchi.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiangalia baadhi ya maandiko ya tafiti mbalimbali zinazoonyeshwa katika maadhimisho ya tano ya Wiki ya Utafiti ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati wa kufunga Wiki hiyo jijini Dar es Salaam
Akizungumza katika sherehe hizo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye amesema chuo hicho kitaendelea kusimamia  ufanyaji wa tafiti kwani ndo kigezo kimojawapo kinatmika katika kupima ubora wa vyuo Duniani.

“Katika kuhakikisha chuo hiki kinarudi katika falsafa yake, tumetenga kiasi cha shilingi bilioni moja katika bajeti ya mwaka 2019/20 ili kuwawezesha wahadhiri na wataalam kufanya tafiti,” amesema Makamu Mkuu wa Chuo.


Baadhi ya washiriki wa maadhimisho ya tano ya Wiki ya Utafiti ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakifatilia kwa makini hotuba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako (Hayupo Pichami) wakati wa kufunga maadhimisho hayo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.