Jumatano, 22 Mei 2019

NDALICHAKO AVUTIWA NA WANAFUNZI WA SHULE YA DAR ES SALAAM INTERNATIONAL ACADEMY KWA UWEZO WA KUJIAMINI

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ameupongeza Uongozi wa shule ya Dar es Salaam International Academy kwa kuwajengea uwezo na kuona umuhimu wa kuwafundisha na kuwapa nafasi wanafunzi kujifunza wenyewe.


Prof. Ndalichako ametoa pongezi hizo jijini Dar es Salaam aliposhiriki katika maonesho mbalimbali ya wanafunzi wa darasa la tano katika shule hiyo ambapo amesema wanafunzi hao wamefundishwa kutafuta taarifa mbalimbali kutokana na mada walizopewa.

“Nimefurahi kuona wanafunzi wa darasa la tano wanaonesha ubunifu katika kuangalia matatizo ya jamii kwani hata mada walizoangalia zinaendana na hali halisi ya sasa ambayo serikali imekuwa ikiwekea msisitizo kama masuala ya jinsia, magonjwa ya homa ya ini na Ebola, dawa za kulevya pamoja na Teknolojia,” amesema Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na wanafunzi, walimu na wazazi (Hawapo Pichani) wa shule ya Dar es Salaam International Academy wakati wa maonesho mbalimbali ya wanafunzi wa darasa la tano.
Waziri Ndalichako amesema katika kutafuta taarifa wanafunzi hao wameonyesha vipaji vya hali ya juu wakati wa kuandaa mada za maonyesho kwani wametumia mitandao pamoja na kuwahoji watu waliowaona muhimu kuwapatia taarifa zilizowawezesha kukamilisha mada zao kwa ajili ya maonyesho hayo.  

Aidha, Waziri Ndalichako ametoa wito kwa walimu kuwawezesha na kuwapa nafasi wanafunzi katika kuwa na ubunifu, kujiamini na kuweza kutafuta taarifa mbalimbali katika kujifunza kwani wanafunzi wa kitanzania wana uwezo wa kufanya mambo makubwa sana lakini wanakwama kutokana na kushindwa kujiamini na uoga wakati shuleni ni sehemu ambayo vipaji hivyo vinaweza kuendelezwa.

“Suala la kujiamini ni changamoto kubwa kwa watanzania wengi, wana uwezo, akili na vipaji lakini wanakuwa hawajiamini hili ni tatizo,  kwa hiyo tuendelee kuwa na maonyesho kama haya ambayo yatawajengea wanafunzi wetu uwezo, kujiamini, kuonyesha yale wanayoweza na kutoogopa kusema mbele za watu,” amesisitiza  Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na kusalimiana na walimu wa shule ya Dar es Salaam International Academy wakati wa maonesho mbalimbali ya wanafunzi wa darasa la tano.
Aidha, Waziri Ndalichako amesema hata katika shule za serikali maonyesho kama hayo yanafanyika  katika ngazi ya shule za sekondari ambayo yanaanza katika ngazi ya shule, wilaya na kilele inakuwa katika ngazi ya Kitaifa hata hivyo wameahidi kuangalia namna ya kuanza kushirikisha wanafunzi wa shule za msingi kwani kufanya hivyo inawezesha kuwaandaa wabunifu tangu wakiwa katika umri mdogo.

Akizungmzia mkakati wa serikali wa kutambua na kukuza ubunifu nchini Waziri Ndalichako amesema kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia inazo atamizi ambazo zinatumika kuendeleza ubunifu lakini pia imeona si rahisi kila mtu kuweza kufika katika Tume hiyo hivyo imeanza utaratibu wa kuanzisha katika ngazi za Halmashauri ambapo mwaka huu mwongozo umetoka wa kuangalia namna gani wabunifu wakitambulika wanaweza kuendelezwa.

“Pia katika vyuo vikuu vyetu kuna hatamizi kwa mfano Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Nelson Mandela kuna atamizi ambazo zinafanya vizuri sana na wao wamejikita katika mazao na kuangalia vitu ambavyo vinaweza kuweka sumu katika mazao lengo ni kuhakikisha tunaongeza wigo ili vipaji wa watanzania viweze kuendelezwa,” amesema Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiangalia kipeperushi kilichotengenezwa na wanafunzi Dar es Salaam International Academy wakati wa maonesho mbalimbali ya wanafunzi wa darasa la tano.
Naye Mkuu wa Shule hiyo, Fawzya Hirji amesema shule hiyo imejipanga kuhakikisha kunakuwa na ushirikiano  kati ya walimu, wanafunzi na wazazi katika kuwawezesha wanafunzi hao kuwa na uwezo wa ubunifu, kujiamini na kutumia mitandao katika kutafuta taarifa mbalimbali zinazowapatia maarifa ya kujua mambo mbalimbali duniani.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akisikiliza maelezo kutoka kwa wanafunzi wa shule ya Dar es Salaam International Academy wakati wa maonesho mbalimbali ya wanafunzi wa darasa la tano.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.