Jumatano, 1 Mei 2019

WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA YAPONGEZWA KWA KUBORESHA CHUO CHA UALIMU MPUGUSO


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Joseph Magufuli amefurahishwa na mradi wa ujenzi na ukarabati wa Chuo cha Ualimu Mpuguso kilichopo katika Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya na ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mradi huo.

Rais Magufuli amesema hayo wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa majengo mapya na ukarabati katika Chuo hicho kwa lengo la kuboresha na kuongeza miundo mbinu ili kuongeza nafasi na kuweka mazingira bora ya ufundishaji na ujifunzaji.

“Niwapongeze Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kukiboresha Chuo hiki ambacho ni cha zamani kilianza mwaka 1926 ikiwa ni shule ya awali hadi mwaka 1975 kilipobadilishwa kuwa Chuo cha Ualimu na sasa kuna wanafunzi zaidi ya 900,” amesema Rais Magufuli.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akivuta utepe pamoja na viongozi wengine kuashiria uwekaji wa jiwe la msingi ujenzi wa Majengo mapya ya Chuo cha Ualimu Mpuguso Rungwe mkoani Mbeya. 

Katika hatua nyingine akizungumza na wananchi baada ya uwekaji jiwe la msingi amesema Serikali yake imeamua kuboresha Vyuo vya Ualimu ili viweze kuandaa walimu bora na kusisitiza kuwa ajira za waalimu watumishi wengine kwenye sekta ya elimu zinaendelea kutolewa ambapo zaidi ya watumishi 19,000 wenye sifa wameajiriwa mwaka huu,  huku akiwataka waalimu wanafunzi kuongeza juhudi katika masomo na kutembea kifua mbele kwani Serikali iko pamoja.

Rais Magufuli pia amewataka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, pamoja na Mkandarasi anaejenga Chuo hicho kuhakikisha kazi inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaolingana na thamani ya fedha ya mradi. Aidha ameagiza Barabara inayoingia katika Chuo hicho kurekebishwa na baadae kutengewa fedha ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami.

Awali akitoa taarifa ya mradi wa Mpuguso, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leornard Akwilapo amesema unagharimu shilingi Bilioni 9.6 na unahusisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 16, maktaba, maabara 2 za sayansi, kumbi za mihadhara 2, bwalo la chakula, mabweni 2 ya wanafunzi 154 kila moja na nyumba za walimu zinazochukua familia 13.  Amesema mradi huo pia unahusisha ukarabati wa nyumba 4 za walimu, mabweni 2 , vyoo na mabafu7.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwasalimia wananchi wa Mpuguso Rungwe mkoani Mbeya mara baada ya kuweka jiwe la msingi msingi ujenzi wa Majengo mapya ya Chuo cha Ualimu Mpuguso.


Mradi wa Ukarabati na ujenzi wa majengo mapya katika Vyuo vya Ualimu unagharamiwa na Serikali ya Tanzania na Canada, ambapo unahusisha vyuo vya ualimu 4 kikiwemo Mpuguso.  Vingine ni Kitangali Mtwara, Shinyanga na Ndala kilichopo Tabora. Kwa ujumla Mradi huu utagharimu shilingi Bilioni 36.4

Nae Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (Mb) amepongeza wana Mpuguso kwa  kupata mradi huo mkubwa na kuwaasa kuhahakikisha wanatumia vizuri majengo hayo na kuyatunza.

Hafla hiyo ilihudhuriwa mamia ya wananchi wa Rungwe na viongozi akiwemo Mhe. Dkt. Tulia Akson Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania, Mhe. Suleiman Jafo(Mb) Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Japhet Hasunga(Mb) Waziri wa Kilimo, Mhe Joseph Kakunda(Mb) Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Mary Mwanjelwa(Mb) Naibu Waziri Utumishi na Mh Elias Kwandikwa(Mb) Naibu Waziri wa Ujenzi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiimba pamoja na wananchi waliokusanyika katika viwanja vya Chuo cha Ualimu Mpuguso mara baada ya kuwasili chuoni hapo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni