Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amezindua Chuo cha Elimu na
Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) cha Wilaya ya Urambo ambapo amesema serikali
katika bajeti ya mwaka huu imetenga
jumla ya Shilingi bilioni 40 kwa ajili
ya kujenga vyuo vipya katika wilaya 25.
Waziri Ndalichako
ametoa kauli hiyo mkoani Tabora wakati wa uzinduzi wa chuo hicho ambapo amesema
ongezeko la vyuo vya ufundi nchini linasaidia kuongeza idadi ya wanafunzi
wanaopata elimu ya ufundi ambao wanahitajika katika viwanda mbalimbali vinavyoanzishwa nchini.
"Kadri
tunavyoongeza vyuo hivi vya ufundi katika wilaya mbalimbali tunasogeza
elimu ya ufundi itolewayo na vyuo vya
VETA karibu na wananchi ili kuwawezesha kupata ujuzi na stadi zinazohitajika
katika kipindi hiki ambacho nchi yetu inalenga kujenga uchumi wa viwanda
kuiwezesha kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, " amesema
Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.
Joyce Ndalichako akizungumza na viongozi
mbalimbali wa Serikali na
wananchi wa Mkoa wa Tabora (Hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa Chuo
cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA)
Waziri Ndalichako
amezitaja wilaya nyingine ambazo zitajengewa vyuo hivyo kuwa ni pamoja na
Wilaya za Chunya, Kilindi, Korogwe, Ukerewe, Igunga, Pangani, Kishapu, Rufiji,
Uyui, Kwimba, Bahi, Mafia, Longido, Mkinga, Uvinza, Ikungi, Iringa Vijijini,
Lushoto, Mbarali, Monduli, Buhigwe, Ulanga, Masasi, Butiama na Chemba.
Aidha, Waziri
Ndalichako amewashukuru Viongozi wa Mkoa wa Tabora, Halmashauri ya Wilaya ya
Urambo, Mbunge wa Jimbo la Urambo, Mhe. Margreth Sitta na wananchi wote wa
Wilaya hiyo kwa utayari wao wa kuhakikisha upatikanaji wa majengo na eneo lenye
ukubwa wa mita za mraba 45,000 kwa ajili ya Chuo cha VETA cha Urambo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.
Joyce Ndalichako pamoja na Viongozi wengine wakifurahia jambo mara baada ya
kuzindua Chuo cha VETA cha wilaya ya Urambo Mkoani Tabora aliyevaa koti ni Mkuu
wa Mkoa wa Tabora
Wakati huo huo Waziri
Ndalichako ametumia nafasi hiyo kuagiza Uongozi wa VETA kukamilisha ujenzi
unaoendelea wa vyuo vya VETA katika wilaya kwa wakati na ubora
Mkuu wa Mkoa wa
Tabora, Aggrey Mwanry, akizungumza katika uzinduzi huo, amewataka vijana wa
wilaya ya Urambo kujiunga na chuo hicho ili kupata ujuzi na stadi
zitakazowawezesha kufanya kazi katika miradi ya ujenzi ya kimkakati ya mkoa
huo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.
Joyce Ndalichako, Mbunge wa Urambo Magreth Sit, Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanry pamoja na Viongozi
wengine wakikata utepe kuashiria uzindua wa Chuo cha VETA cha wilaya ya Urambo
Mkoani Tabora.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt. Pancras Bujulu, akitoa Maelezo ya mradi huo amesema umehusisha ukarabati wa
majengo, ununuzi wa samani za ofisi, vifaa na vitendea kazi vya ofisi , zana za
kufundishia na samani za mabweni ya
wanafunzi umegharimu zaidi ya shlingi milioni 200.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.
Joyce Ndalichako, akikagua baadhi ya vifaa vya kufundishia na kujifunzia
vilivyonunuliwa kwa ajili ya Chuo cha VETA cha wilaya ya Urambo Mkoani Tabora.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.