Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli imeandika historia kwa kufanya uwekezaji mkubwa kwenye Sekta ya Elimu
kwa lengo la kutimiza azma yake ya kupata nguvu kazi iliyo mahiri katika sekta mbalimbali
za ufundi itakayofanya kazi katika viwanda ili kufikia uchumi wa kati na wa
viwanda ifikapo 2025.
Hayo yameelezwa Jijini
Mwanza na Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia William ole Nasha
alipofanya ziara katika Wilaya za Sengerema, Kwimba na Misungwi kukagua miradi
ya maendeleo ya ujenzi wa ofisi mpya za Uthibiti ubora wa shule wilaya na ukarabati wa Vyuo vya Maendeleo ya
Wananchi (FDC) unaoendelea katika wilaya hizo.
Ole Nasha alisema pamoja na
mambo mengine mengi ambayo serikali imetekeleza katika Sekta ya Elimu katika
mwaka wa fedha 2019/20 Serikali imetenga fedha kiasi cha sh bilioni 40 kwa
ajili ya ujenzi wa Vyuo vipya 25 vya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA)
vya Wilaya lakini pia kuna vyuo 5 vya mkoa vinaendelea kujengwa ili kuwezesha
vijana wa kitanzania kusomea elimu ya ufundi itakayowawezesha kujiajiri.
Naibu Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akikagua ujenzi wa majengo ya Chuo cha
Maendeleo ya Wananchi Karumo kilichopo Wilaya ya Sengerema Mkaoni Mwanza.
|
Pia alisema Serikali inajenga na kukarabati vyuo 55 vya Maendeleo ya Wananchi (FDC) ili kuboresha miundombinu ya vyuo hivyo itakayotoa fursa kwa vijana wengi kujifunza na kupata elimu ya ufundi itakayowawezesha kufanya kazi za uzalishaji katika maeneo yao lakini pia watakuwa chachu ya maendeleo ambayo ndio Serikali inahitaji.
“Katika moja ya eneo ambalo
Mhe. Rais Magufuli ameelekeza nguvu nyingi katika kipindi cha utawala wake ni
kuboresha elimu na sababu ni rahisi
huwezi kusema unajenga nchi ili kufikia uchumi wa kati unaotegemea
uchumi wa viwanda kama huna nguvu kazi iliyoelimika,”alisema Naibu Waziri Ole
Nasha
Alisema kwa sasa ukitembea
nchi nzima utaona ujenzi na ukarabati unaoendelea katika vyuo, shule za msingi
na sekondari hii yote ni mkakati wa Serikali wa kuboresha elimu katika gazi
zote za za elimu nchini.
“Mwaka uliopita pekee wizara
ya Elimu, Saynsi na Teknolojia kupitia Programu ya EP4R imekarabati na kujenga
miundombinu mipya kwenye shule zaidi ya 500 ambapo zaidi ya sh bilioni 90
zimetumika na hapa nazungumzia kile kinachotekelezwa na Wizara ya Elimu pekee
na sio TAMISEMI. Hii inaakisi uwekezaji mkubwa ambao umefanyika kwenye sekta ya
elimu,” alisema Naibu Waziri Ole Nasha.
Naibu Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akikagua miundombinu ya vyoo katika
moja ya bweni la wanafunzi katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Karumo Jijini
Mwanza.
Alisema haya yote yanatokana
na ukweli kwamba elimu ndio msingi mkubwa wa kuleta mabadiliko yanayotakiwa
katika nchi yetu na ndio maana serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika
sekta ya elimu.
“Utaona uwekezaji huu
haufanyiki tu kwenye kujenga tunaweka vifaa vya kufundishia na kujifunzia. Katika
vyuo ambavyo vinashughulika na ufundi wa Kati Serikali imeendelea kupeleka
vifaa kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji,” aliongeza Naibu Waziri
Ole Nasha
Pia alisema kwa miaka
mitatu mfululizo Serikali imeajiri
takribani walimu wapya elfu 18, na
kwamba katika mwaka huu wa fedha serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuajiri
walimu wengine wapya lengo ni kuwa na uwiano mzuri kati ya mwalimu na
mwanafunzi.
Alitaja eneo lingine ambalo
fedha nyingi za umma zinaelekezwa ni ugharamiaji wa Elimu bila malipo ambapo
kila mwezi Serikali hutoa zaidi ya bilioni 20 kugharamikia elimu kuanzia elimu
ya awali hadi kidato cha nne. Alisema lengo ni kumwezesha mtoto wa kitanzani
mwenye umri wa kuanza shule aweze kusoma bila kisingizio cha kukosa ada.
Naibu Waziri Ole Nasha alisema kwa upande wa Elimu ya Juu Serikali imepanua wigo wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ambapo katika mwaka huu inategemea wanafunzi wapya elfu 45 huku fedha za mikopo zikiongezeka kutoka shilingi bilioni 427 za mwaka jana hadi kufikia 450 mwaka huu.
Katika hatua nyingine Naibu
Waziri Ole Nasha amezitaka Halmashauri za Kwimba, Sengerema na Misungwi kusimamia
vizuri fedha zinazokuja katika maeneo yao kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya
maendeleo ili iweze kukamilika kwa wakati na matokeo yaakisi thamani ya fedha
zilizotolewa
“Mhe. Rais katika jambo ambalo anasisitiza
kila siku ni matumizi sahihi ya fedha za miradi ukiona fedha zinakuja fahamu ni
kwa sababu serikali imetumia nguvu kubwa katika kukusanya kodi na kuzitafuta
fedha hizo zisimamieni vizuri’’alisema Naibu Waziri Ole Nasha.
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Juma Sweda, Mkuu wa wilaya ya Kwimba Senyi
Nganga na yule wa Sengerema Emmanuel Kipoyo wameahidi kuendelea kusimamia
ipasavyo fedha za miradi ya maendeleo zinazoletwa katika Wilaya zao ili ziweze
kutimiza lengo na matokeo yaakisi gharama ya fedha zilizotolewa ikiwa ni pamoja
na kusimamia elimu ipasavyo katika Wilaya hizo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.