Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassimu Majaliwa (Mb) ameitaka
Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) nchini kuhakikisha mitaala inayotumika katika vyuo vikuu
iweze kuandaa wahitimu siyo tu kwa kuajiriwa, bali pia kuwa na uwezo wa
kujiajiri na kutengeneza ajira kwa wengine.
Waziri
Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa maonesho
ya 14 ya elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia nchini ambapo amesema uwepo wa
mitaala ya aina hiyo utasaidia kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi na maendeleo
ya watu kwa ujumla.
“Nimeelezwa
kuwa tayari baadhi ya Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu zimeshaanza
kuchukua hatua za kutengeneza Mitaala mipya na kuhuisha ile ya zamani ili
kuifanya iendane na mahitaji ya sasa ya taifa na soko la ajira, nitoe wito kwa
Taasisi zote za Elimu ya Juu kuendelea kuhuisha na kuboresha mitaala yao kwa
mwelekeo huo,” alisema Mhe Majaliwa.
Akizungumzia
azma ya serikali ya kuongeza udahili katika Vyuo Vikuu, Waziri Mkuu ameitaka
Tume ya Vikuu kutafuta mbinu za kuviwezesha vyuo zaidi ikiwa ni pamoja na
kujengea uwezo vyuo vikuu binafsi ili visaidie katika kuongeza udahili pamoja
na kufikia viwango vinavyotakiwa na siyo kuwapunguzia viwango vya matakwa ya
usajili.
“Msimamo
wa Serikali uko wazi na unataka Vyuo Vikuu Binafsi kuwa washirika muhimu kwenye
maendeleo ya Sekta ya Elimu ya Juu nchini, hata hivyo nai vema nikaeleweka vizuri
hakuna mbadala wa elimu bora, ni wajibu wetu kuhahakikisha vyuo vyote vinatoa elimu bora.
TCU endeleeni kutekeleza majukumu yenu
ya kimsingi ya kudhibiti na kushauri lakini zaidi jipambanue katika uwezeshaji wa vyuo hivyo ili kuondoa
taswira hasi iliyojengeka katika jamii kuwa kazi ya Tume ni kuvifungia vyuo vikuu badala ya kutatua
changamoto zinazowakabili.” Alisema Mhe.
Majaliwa.
Alisema
ili kuongeza idadi ya watanzania wanaopata nafasi ya Elimu ya Juu, ni lazima
kama nchi kupanga mikakati kwa kushirikiana na sekta binafsi, ambao ni wadau wakubwa
sana katika Elimu ya Juu kwani ukiangalia kati ya wahitimu wote wa Vyuo vikuu kwa
mwaka, asilimia 25 wanatoka katika vyuo vikuu binafsi.
Katika
hatua nyingine Mhe. Majaliwa ameitaka TCU kuhakikisha wanakutana na taasisi
binafsi zinaowasaidia watanzania kupata nafasi katika vyuo vikuu nje ya nchi
ili ziweze kuwatambua, kuwasajili lakini pia kufanya nao kazi kwa karibu ili
kuwaambia mahitaji halisi ya kwenda vyuo vikuu ni yapi na wao washiriki katika
kumshauri kijana ni alama zipi za ufaulu zinafaa kwenda kwenye digrii, diploma na
ama cheti ili kuepukana na changamoto ya kutotambulika kwa vyeti pindi
wanapohitimu katika ngazi hizo za elimu akitolea mfano watanzania ambao
wamesoma kwenye moja ya Chuo Kikuu kilichopo nchini Misri lakini vyeti vyao kutotambulika.
“Naona
kundi kubwa la vijana wa kidato cha sita wanatafuta vyuo kupitia taasisi hizo
ni vyema sasa TCU kwa kuwa mko katika maonesho hayo mshirikiane kuwasaidia
vijana wetu hawa kupata vyuo vinavyostahiki ili wakienda kusoma akipata cheti
na kurejea muweze kuvitambua vyeti hivyo,” alisema Mhe. Majaliwa
Awali
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William ole Nasha alimweleza
Waziri Mkuu kuwa ili kuongeza idadi ya wahitimu watakaochochea ukuaji uchumi kwa kupitia sekta
zinazochangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa uchumi tayari baadhi ya vyuo
vimefanya maboresho ya mitaala kutoka kwenye mfumo unaozingatia ufahamu na kwenda
kwenye mfumo wa umahiri.
Pia
Wizara kwa kushirikiana na Taasisi za sekta binafsi Tanzania imeanzisha
mabaraza 6 ya kisekta ya ujuzi na maarifa katika Sekta za Kilimo, Ujenzi,
Uchukuzi, Utalii, Nishati na TEHAMA kwa lengo la kushauri kuhusu mitaala na
mahitaji halisi ya soko la ajira.
Nae
Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu nchini Charles Kihampa amesema Maonesho
ya Vyuo Vikuu kwa mwaka huu yamehudhuriwa na taasisi 81 ambapo taasisi 66 ni za
ndani ya nchi na 15 ni taasisi za kutoka nje ya nchi.
Akizungumza
wakati wa ufunguzi wa maonesho ya 14 ya elimu ya Juu Mwenyeketi wa Kamati ya
Wakuu wa Vyuo vikuu vya Umma nchini Prof. Raphael Chibunda ameipongeza Wizara
ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Serikali kwa Ujumla kwa kuhakikisha kuwa Mikopo ya
wanafunzi wa elimu ya juu inaongezeka jambo ambalo limepunguza migogoro katika
Vyuo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.