Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako ametoa wito kwa Viongozi wa Elimu ya juu nchini
kuhakikisha wanasimamia ipasavyo mchakato wa udahili wa wanafunzi wa elimu ya
juu kwa mwaka wa masomo 2019/20 ili kuondoa usumbufu usiokuwa wa lazima kwa
wanafunzi, wazazi, walezi na wafadhili wa wanafunzi hao.
Waziri Ndalichako ametoa
wito huo Jijini Dar es Salaam wakati akifunga maonesho ya 14 ya elimu ya juu yaliyofanyika
katika viwanja vya Mnazi ambayo yalikuwa na kauli mbiu isemayo Jukumu la Taasisi za Elimu ya Juu Katika Kuzalisha Ujuzi
Unaohitajika kwa ajili ya Viwanda.
Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akipata maelezo ya programu
zinazotolewa na Chuo Kikuu Dodoma wakati wa maonesho ya 14 ya elimu ya Juu
yalivyofanyika katika viwanja vya Mnazi mmoja Jijini Dar es Salaam.
Katika hotuba yake amesema
asingependa kuona changamoto zilizotokea mwaka jana katika kujiunga na vyuo
zinajirudia kwani changamoto nyingine zilisababishwa na Vyuo vyenyewe kutokuwa
na mifumo thabiti ambayo wanafunzi wangeweza kufanya maombi na kujithibitisha
katika vyuo kwa urahisi.
“Nafahamu kwamba TCU
wameshatoa mafunzo na maelekezo ya kutosha kwa wataalamu wa mifumo ya kompyuta
na maafisa udahili wa vyuo vyote ambao mnadahili wanafunzi kwa mwaka wa masomo
2019/20 kwa hiyo naamini kwamba zoezi la udahili kwa mwaka huu litafanyika kwa
ufanisi zaidi kuliko ilivyokuwa mwaka jana,” alisema Waziri Ndalichako.
Waziri Ndalichako alisistiza kuwa kwa mujibu wa sheria ya vyuo
vikuu sura ya 346 ya sheria za Tanzania jukumu la kudahili wanafunzi ni la
Seneti za Vyuo Vikuu au Bodi ya za Chuo husika, hivyo amewataka Viongozi wa
Vyuo kutumia mamlaka ya Seneti za Vyuo Vikuu au Bodi kuhakikisha kuwa wanasimamia
kikamilifu udahili wa wanafunzi ili waweze kujiunga kwa urahisi huku akisistiza
pia vigezo, masharti, taratibu na sifa
za mwanafunzi kujiunga na chuo kuzingatiwa.
“Niwakumbushe tu Serikali iko macho, katika mchakato wa
udahili msipofuata taratibu mkaweka watu wasio kuwa na sifa tutawaondoa lakini
kumbukeni na ninyi mloiwaingiza hamtabaki salama, hakikisheni zoezi hilo
linafanyika kwa ufanisi,”aliongeza Waziri Ndalichako.
Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akipata maelezo katika banda
la DIT wakati wa maonesho ya 14 ya elimu ya Juu yaliyofanyika katika viwanja
vya Mnazi mmoja Jijini Dar es Salaam
Sambamba na hilo amewataka wanafunzi wanaotarajia kujiunga na masomo ya elimu ya juu kutokuwa wavivu wa kusoma maelekezo kabla ya kuanza kujiunga ama kuchagua kozi katika vyuo. Amewaasa kuzingatia sifa zinazohitajika kwa kulinganisha ufaulu wao wakati wa kuchagua kozi huku akisistiza kuwa Serikali haina utaratibu wa kumpangia mwanafunzi programu ya kusoma isipokuwa inachagua mwanafunzi kutokana na sifa alizonazo katika kozi husika.
Katika hatua nyingine Waziri
Ndalichako amezitaka Taasisi za Elimu ya juu na Vyuo vikuu kuendelea kujitathmini
ni kwa kiasi gani tafiti ambazo wamekuwa
wakizifanya zinagusa moja kwa moja jamii na kusaidia kutatua changamoto
mbalimbali zilizopo katika jamii.
“Ninyi Taasisi za Elimu ya
Juu macho yenu na masikio yawe wazi kila mara ili muweze kusikiliza wapi katiika
jamii kuna changamoto na kwa kutumia utaalamu wenu mshiriki kuzitatua, kumbukeni
elimu ya juu katika nchi yoyote ile ndio kitovu cha maarifa hivyo muendelee
kutumika katika kutatua changamoto hizo,” aliongeza waziri Ndalichako.
Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na baadhi ya
wanafunzi waliofika katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam
kutembelea maonesho ya 14 ya elimu ya juu.
Akizungumza kwa niaba ya
washiriki wa maonesho Profesa Uswegi Minga Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Tumaini amesema
uwepo wa maonesho hayo umetoa nafasi ya vyuo vyenyewe kujitangaza kuhusu fursa
zinazopatikana katika vyuo vyao, lakini pia imekuwa nafasi nzuri ya
kubadilishana uzoefu kutokana na kujifunza
namna vyuo vingine vinavyofanya kazi hivyo kusaidia kufanya maboresho katika
maeneo ya uendeshaji wa Vyuo lakini pia katika upangaji na ufundishaji wa
programu mbalimbali.
Maonesho ya 14 ya Vyuo
vya Elimu ya Juu yameandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu nchini na kwa mwaka huu yamekuwa
na washiri zaidi ya 80 vikiwemo kutoka nje ya nchi na vile vyaTanzania.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.