Waziri
wa Eimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amefungua na kushiriki
Mdahalo juu sekta ya Elimu uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Mjadala
huo ulioandaliwa na Mwanachi Communications Ltd., (MCL) kwa kushirikiana na
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ulihusisha majadiliano juu ya uwezeshaji
vijana katika kukuza maarifa na ujuzi mahususi.
Akifungua
mdahalo huo Waziri Ndalichako amesema Serikali ya awamu ya Tano imewekeza kiasi
kikubwa cha rasilimali ili kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji
katika ngazi zote za elimu ili vijana wanaosoma wapate mafunzo katika mazingira
yatakayowawezesha kuwa mahiri katika fani wanazosomea.
Prof.
Ndalichako ameongeza kuwa katika ngazi ya elimu ya ufundi na elimu ya juu
serikali inaboresha maabara na karakana na kuweka vifaa vya kisasa ili mafunzo
kwa vitendo yafanyike kwa tija na kulingana na mazingira ya sasa. Aidha ametolea
mfano wa maktaba ya kisasa inayojengwa katika Chuo Kikuu cha Teknolojia Mbeya (MUST)
itakayokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 2,500 kwa mara moja ambayo inagharimu
fedha za ndani zaidi ya shilingi bilioni 11.
Ndalichako
amewashukuru MCL kwa kufungua njia ya kuwa na mijadala ya wazi juu ya maendeleo
ya elimu na kuahidi kuandaa mjadala mwingine wa Elimu utakaohusisha wadau. Pia amepongeza washiriki kwa kutoa maoni
ambayo yana tija katika kuboresha elimu, huku akisisitiza kuwa elimu yetu
inaandaa vijana mahiri ambao wanashiriki kujenga taifa.
"Humu
ndani tumesikia fikra mahiri zinazotokana na vijana ambao wanasoma hapa hapa
nchini na mitaala ni hii hii, hivyo tujiamini kuwa elimu yetu ni bora na
inawezesha vijana kuwa mahiri katika fani mbalimbali," alisema Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako akiwa na baadhi ya wadau wa Elimu wakifuatilia mjadala juu ya uwezeshaji vijana katika kukuza maarifa uliofanyika jijini Dar es Salaam. |
Ndalichako
amesisitiza juu ya uboreshaji elimu ya ufundi ambapo amesema katika mwaka huu
wa fedha vyuo vipya vya VETA 25 vinajengwa kwa shilingi bilioni 40.
Ndalichako
pia amesema Serikali kupitia VETA inaendelea na programu ya kutambua na
kurasimisha ujuzi kwa vijana ambapo amesema mwaka huu zaidi ya vijana 10,000
watapatiwa mafunzo kutokana na ujuzi walio nao na kupatiwa vyeti vya kurasimisha
ujuzi huo. Amesema lengo la kurasimisha ni kuwatambua, kuwapa stadi na kuwaongezea
ujuzi vijana walioko katika maeneo mbalimbali ambao wamekuwa wakifanya kazi za
ujuzi bila vyeti.
Awali,
akizungumza katika mjadala huo Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Francis Nanai amemshukuru
Waziri Ndalichako na Viongozi wa wizara kwa kukubali kushiriki mjadala na
kupokea maoni. Amesema wao kama sekta
binafsi wanalo jukumu la kushirikiana na serikali katika kusukuma mbele
maendeleo kulingana na eneo lao la biashara.
Akiongea
katika Mjadala huo, Prof. Lughano Kusiluka ambaye ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu
cha Mzumbe amesema Vyuo Vikuu vinaandaa mitaala kulingana na uhitaji wa soko na
mahitaji ya wakati. Amewaasa vijana pia
kuona umuhimu wa kutumia elimu wanayopata na vipaji walivyo navyo kubuni
biashara na kujiajiri badala ya kusubiri ajira.
Kusiluka
amesema Vyuo vikuu vina programu za kukuza bunifu za wanafunzi na kuziendeleza
kuwa biashara kupitia Vituo Atamizi na kambi za ujasiriamali.
Naye
mmoja wa washiriki, Abel Nyengo ameiomba Serikali kuhakikisha kila kijana aliyeko
katika chuo anapata nafasi ya mafunzo kwa vitendo.
"Nishauri
serikali kuwa mafunzo kwa vitendo iwe ni lazima na ipewe umuhimu mkubwa katika
kutahini wanafunzi badala ya kutegemea mitihani,” alisema Nyengo.
Wananchi
na wadau mbalimbali wametoa maoni mengi juu ya mada hiyo wakihusisha mitaala,
utoaji elimu na ujuzi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.