Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha amewataka wazazi
kuacha kuwageuza mitaji watoto wao wa kike kwa kuwaozesha mapema na badala yake
wawasaidie katika kupata elimu ili baadaye wawe msaada kwao na taifa kwa
ujumla.
Ole
Nasha ameyasema hayo leo alipofanya ziara ya kikazi wilayani Itilima
mkoani Simiyu ambapo amekagua ujenzi wa mabweni mawili ya wasichana
katika shule ya sekondari Nkoma yenye uwezo wa kuchukua watoto 160 kwa wakati
moja.
"Niwaambie
kitu wazazi, kama unataka kumfanya mwanao wa kike mtaji basi mtaji mkubwa ni
kumpa elimu na sio kumuozesha," alisema Ole Nasha.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha akiongea na wazazi, walezi na wanafunzi wa shule ya sekondari Nkoma iliyopo wilaya ya Itilima mkoani Simiyu. |
Baadhi ya wazazi na walezi wa wanafunzi wa shule ya Nkoma wakimsikiliza Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha (hayupo pichani) alipokuwa akiongea nao shuleni hapo. |
Aidha
Naibu Waziri Ole Nasha amewataka wazazi kuwekeza kwenye elimu ya watoto wao
huku akisisitiza kuwa mtoto wa kike ana haki ya kupata elimu sawa na mtoto wa
kiume, ambapo amesema katika jamii nyingi bado hawajawapa kipaumbele cha kupata
elimu watoto wa kike.
"Kuna
baadhi ya wazazi bado wanashawishi watoto wao kufanya vibaya katika mitihani
yao ya mwisho ili wasiendelee na masomo. Nawaomba wazazi msishawishi watoto wa
kike na kuwatilia vikwazo vya kukatisha masomo ili muwaozeshe. Mtoto wa kike
ana nafasi ya kupata elimu sawa na mtoto wa kiume," alisema Naibu Waziri Ole
Nasha.
Mwalimu Mkuu wa shule ya sekondari Nkoma, Sarah Matonya akisoma taarifa ya ujenzi wa mabweni mawili mapya mbele ya Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha (hayupo pichani). |
Ole
Nasha aliongeza kuwa serikali na wadau wa elimu wanatakiwa waendelee kutoa
hamasa ya elimu kwa jamii, wanafunzi na wazazi ili miundombinu ya elimu
inayojengwa iweze kutumika kwa faida ya wananchi wote katika kuboresha na
kukuza elimu.
Naibu
Waziri Ole Nasha amepongeza usimamizi wa fedha za miradi ya elimu katika
wilaya hiyo kutokana na kutokuwepo kwa malalamiko yoyote ya matumizi mabaya ya
fedha hizo.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha akizindua mabweni katika shule ya sekondari Nkoma ya wilayani Itilima mkoani Simiyu. |
Awali,
akisoma taarifa ya ujenzi wa mabweni hayo, Mwalimu Mkuu wa shule ya sekondari
Nkoma, Sara Matonya alisema mabweni hayo yamegharimu zaidi ya shilingi milioni
300 na kwamba kukamilika kwa mradi huo wa ujenzi wa mabweni kumechochea hamasa
ya wanafunzi wa kike kusoma kwa bidii kutokana na kuboreshwa kwa mazingira ya
kujifunzia.
"Mabweni
haya mawili yana uwezo wa kubeba wanafunzi 80 kila moja na yamesaidia wanafunzi
kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu wa zaidi ya kilometa 10 kufika
shuleni. Wanafunzi wa kike pia wameepukana na vishawishi na mimba zilizokuwa
zikiwasababishia kukatisha masomo," alisema Mwalimu Matonya.
Kwa
upande wao wazazi na wanafunzi wameipongeza serikali kwa kutoa elimu bila
malipo pamoja na kuwajengea mabweni, hali iliyopelekea kuongezeka kwa
mahudhurio ya wanafunzi darasani, ufaulu na mwitikio wa elimu katika jamii.
"Tunaipongeza
serikali kwa ujenzi wa mabweni haya ambayo yametupunguzia changamoto ya
kutembea umbali mrefu na pia tumekuwa na muda mwingi wa kujifunza na kujisomea,
na hivyo kutuwezesha kufanya vizuri katika masomo yetu," alisema Myano Ngusa,
mwanafunzi wa shule ya sekondari Nkoma.
Mojawapo ya chumba katika bweni jipya la shule ya sekondari Nkoma ya wilayani Itilima mkoani Simiyu. |
Katika
ziara hiyo Ole Nasha pia alikagua ofisi ya Uthibiti Ubora wilaya ya Itilima
ambazo ujenzi wake umekamilika pamoja na majengo ya VETA yanayoendelea kujengwa
katika kijiji cha Kanadi wilayani humo.
Muonekano wa nje wa moja kati ya mabweni yaliyojengwa katika shule ya sekondari Nkoma ya Itilima mkoani Simiyu lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 kwa wakati mmoja. |
Muonekano wa nje wa jengo la ofisi za Uthibiti Ubora wilaya ya Itilima mkoani Simiyu. |
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha akikagua ofisi ya Uthibiti Ubora wilaya ya Itilima mkoani Simiyu. |
Muonekano wa ndani wa chumba kimojawapo katika majengo ya VETA, Itilima mkoani Simiyu. |
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha (mwenye skafu) akisikiliza maelezo kuhusu VETA kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Benson Kilangi. |
Muonekano wa nje wa jengo la VETA la wilayani Itilima mkoani Simiyu. |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.