Waziri Ndalichako ameyasema hayo jijni Dar e Salaam alipomuwakilisha Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Semina ya Kimataifa ya kuwajengea uwezo vijana wa kike (Girl Guides) katika masuala ya Uongozi ijulikanayo kama Julitte Low Seminar.
Amesema lengo la semina ni kupanua na kuimarisha ushiriki wa wasichana katika masuala ya girl guides lakini pia kuwawezesha kushirikiana katika masula ya kiutamaduni na uongozi ikiwa ni pamoja na kuwatia moyo wasichana hao ili wazidi kufanya vizuri zaidi katika Jamii wanazotoka.
“Naamini baada ya semina hii ya siku saba wasichana watakuwa na uwezo kushiriki katika masuala ya uongozi na kukemea imani potofu ambazo zinakuwa zikionesha kuwa mwanamke ni kiumbe dhaifu na kutengeneza mtazamo chanya kuwa wanawake ni viumbe kama wanaume na wana uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko katika ulimwengu huu,”Alisema Prof Ndalichako.
Prof Ndalichako amesema Nchi ya Tanzania inatekeleza mipango inayozingatia usawa wa kijinsia na kuwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanawake na wanaume wana fursa sawa katika maendeleo.
“Mhe Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu asingeweza kupata nafasi aliyo nayo kama nchi ingekuwa bado ina dhana potofu , uwepo wake ktk nafasi ya Makamu wa Rais, viongozi na wataamu wengine katika nyanja mbalimbali inaonesha kuwa nchi yetu imepiga hatua katika kuweka usawa wa kijinsia ”aliongeza Prof ndalichako
Amewapongeza Waandaaji wa Semina hiyo kwa kuchagua Tanzania kuwa nchi mwenyeji na kwamba Tanzania ina historia ya kutoa wanawake ambao ni wa nguvu akiwataja viongozi hao kwa uchache kuwa ni marehemu bibi Titi Mohamed ambaye amekuwa kiongozi wa nchi yetu wakati wa uongozi wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Getrude Mongela ambaye alishiriki kwenye mkutano wa Beijing, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Asha-Rose Migiro, Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Anna makinda na sasa Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Nae Mwenyekiti wa Chama cha Girl Guides Taifa Prof Martha Qorro amesema semina ya mafunzo ya uongozi kwa vijana wa kike (Girl Guides) inafanyika ulimwengu mzima na itasaidia wasichana hao kujitegemea, kujitambua, kujithamini, kupenda taifa lao kumpenda Mungu kuhesimu wengine na kusaidia mahali popote panapohitaji msaada.
Kwa upande wake mwakilishi wa Bodi ya Dunia katika "World Association of Girl Guide and Girl Scout" kwa kanda ya Afrika Florentina Mganga amesema semina hii inaendelea ulimwenguni kote na vijana wa kike 700 watapata mafunzo juu wa uongozi na itawawezesha kujua kuwa mtoto wa kike anaweza kuwa kiongozi wanachotakiwa ni kujiamini.
Semina ya Kimataifa ya kuwajengea uwezo vijana wa kike juu ya masula ya uongozi inashirikisha nchi 17 ambazo ni Marekani, Uingereza, Ujerumani Swizaland, Ghana, Zimbawe, Malawi, Rwanda, Burundi, Kenya, Madagascar, Egypt, Germany,Uganda, Sierra Leone, Poland, Hong Kong, Philippines na Tanzania ikiwa kama Mwenyeji wao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.