Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako ameonesha kukerwa na usimamizi mbovu wa
miradi ya Elimu katika Halmashauri ya Wilaya Buhigwe mkoani Kigoma na kumuagiza
Katibu Mkuu wa Wizara anayoisimamia, Dkt. Leonard Akwilapo kuleta wataalamu
watakaofanya ukaguzi maalum wa utekelezaji wa miradi ya elimu katika wilaya
hiyo.
Waziri Ndalichako ametoa
kauli hiyo Wilayani Buhigwe mkoani
Kigoma mara baada ya kukagua baadhi ya
miradi ya Elimu inayotekelezwa na Wizara kupitia Mpango wa Lipa
Kulingana na Matokeo (EP4R)na kubaini uwepo wa kasoro kadhaa ikiwemo matumizi
ya vifaa vya ujenzi vilivyo chini ya Kiwango na
majengo ya shule ya Msingi ya mfano Bwega kutofautiana na ramani iliyopendekezwa na
wizara.
"Kwa ujumla usimamizi
wa Miradi katika wilaya ya Buhigwe siyo
mzuri, maafisa elimu hawawajibiki katika kuangalia kazi zao, unakuta kazi
zimefanyika hovyo, watu hawafuatilii," alisema Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia akikagua moja ya nyumba za walimu katika Shule ya Msingi Kasumo
iliyoko wilayani Buhigwe mkoani Kigoma
Waziri Ndalichako amesema
Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe hatimizi wajibu wake ipasavyo kwa
kuwa ameshindwa kusimamia miradi hiyo kwa viwango vinavyotakiwa na kuruhusu
matumizi ya vifaa vya ujenzi visivyo na ubora lakini pia ameshindwa kufuata
ramani katika ujenzi wa majengo ya shule
ya msingi ya mfano inayojengwa wilayani humo.
Kiongozi huyo amesema
tayari amewasiliana na Katibu Mkuu wa
Wizara, Dkt. Leonard Akwilapo ili ufanyike ukaguzi wa kina katika miradi ya
elimu Wilaya ya Buhigwe lengo likiwa ni kubaini
mapungufu na iwapo kuna mtu kafanya uzembe kwa manufaa yake awajibike.
"Inabidi kabla ya
kuleta fedha nyingine za miradi ya elimu wilayani Buhigwe ije timu ya watalaamu
mainjinia wachunguze walinganishe BoQ na kilichofanyika, haiwezekani turuhusu
uzembe kama huu kuendelea kwenye miradi inayotumia fedha ya wananchi wanyonge,"
aliongeza Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akionesha dosari kwenye jengo la maabara la
shule ya sekondari Janda wakati akikagua miradi ya elimu inayotekelezwa katika
shule hiyo na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R)
Kwa upande wake Mkuu wa
Wilaya ya Buhigwe, Kanali Michael Ngayanalina amemshukuru Waziri Ndalichako kwa
ziara yake wilayani humo na kusema kuwa
mapungufu yote yaliyobainika tayari
Kamati yake imeyatolea maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo na
kwamba zoezi linaloendelea ni kuwachukulia hatua wahusika.
"Kamati ya Usalama ya
wilaya ilibaini mapungufu katika miradi mbalimbali na tulitoa maelekezo kupitia
kwa Mkurugenzi na vyombo vyetu
vilishaagizwa kufanya uchunguzi na kuchukua hatua stahiki," amesema Mkuu
wa Wilaya hiyo, Ngayalina.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikagua ujenzi wa maabara unaoendelea katika
shule ya sekondari Janda iliyoko Buhigwe Mkoani Kigoma
Naye Mkurugenzi wa
Halmashauri hiyo, Anosta Nyamoga amesema ofisi yake tayari imemfukuza kazi
fundi aliyekuwa na mkataba wa kufanya ukarabati na ujenzi wa vyumba vya
madarasa katika Shule ya Sekondari Janda kutokana na kufanya kazi hiyo chini ya
viwango na kuahidi kuzifanyia kazi kasoro zote ambazo zimebainishwa na Waziri
Ndalichako.
Akiwa wilayani Buhigwe
Waziri Ndalichako amekagua miradi ya elimu katika shule ya msingi Bwega, shule
ya sekondari Janda, shule ya sekondari
Muyama na shule ya msingi Kasumo ambayo kwa pamoja inatarajia kugharimu zaidi
ya shilingi bilioni moja.
Waziri Ndalichako yuko
Mkoani Kigoma kwa ziara ya kikazi kukagua miradi ya Elimu katika Halmashauri ya
Wilaya ya Buhigwe na Halmashauri ya Mji Kasulu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikagua moja ya dawati lililoko katika Shule
ya Sekondari Muyama mara baada ya kukagua ujenzi wa darasa hilo
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.