Alhamisi, 14 Novemba 2019

ZAIDI YA MILIONI 280 ZATUMIKA KUJENGA NA KUKARABATI MIUNDOMBINU YA SHULE YA MSINGI BUHANGIJA





Serikali kupitia Mpango wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) imetumia kiasi cha shilingi milioni 286.6 kwa ajili ya kukarabati na kujenga miundombinu katika shule ya msingi Buhangija ya Mkoani Shinyanga.

Akizungumza shuleni hapo Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Selemani Kipanya amesema mwaka 2018 Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iliipatia shule hiyo fedha hizo kwa ajili ya kujenga vyumba vinne vya madarasa, mabweni mawili na matundu 18  ya vyoo.

"Majengo haya yamesaidia sana kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani na vyooni pamoja na kuboresha mazingira ya kufundushia na kujifunzia," amesema Mwalimu Kipanya.

Mwalimu Kipanya amesema shule hiyo ambayo ni jumuishi ina jumla ya wanafunzi 1,052 ambapo kati yao 230 ni wenye mahitaji maalum na kwamba wanafunzi hao wenye mahitaji maalum wanaishi bweni wakati wengine wanasoma kutwa.

Naye Mwalimu Mohamed Makana ameishukuru serikali kwa kuikumbuka shule hiyo ambayo ilikuwa na changamoto nyingi za miundombinu pamoja na vifaa vya kujifunzia na kufundishia hasa kwa upande wa wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Mwalimu Makana amesema shule hiyo imepatiwa vifaa vya kufundishia na kujifunzia vya kutosha kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum ikiwemo kofia pamoja na miwani kwa ajili ya watoto wenye ualbino.

Mwanafunzi Jesca Michael mwenye ualbino ameishukuru Serikali kwa kuwalinda pamoja na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia huku akiiomba serikali kuendelea kuwaangalia kwa ukaribu wanafunzi wenye mahitaji maalum ili nao waendelee kupata elimu bora.


Darasa lililojumuisha watoto wenye mahitaji maalum na wale wa kawaida katika shule ya msingi Buhangija



Baadhi ya miundombinu iliyojengwa na Mpango wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) katika shule ya msingi Buhangija iyopo mkoani Shinyanga 
Mtoto mwenye ulemavu wa kutokuona akitumia kifaa maalum kwa ajili ya kuandikia katika shule ya msingi Buhingili. Kifaa hicho ni moja ya vifaa vilivyonunuliwa kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum .


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.