Jumatano, 12 Februari 2020

UFUNGUZI WA MAFUNZO YA MAAFISA BAJETI WA WIZARA NA WA OFISI ZA UTHIBITI UBORA WA SHULE KANDA

Serikali imeweka kipaumbele katika kuwajengea uwezo watendaji wake ili kutimiza majukumu yao kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kuongeza nidhamu katika matumizi ya fedha na usimamizi fanisi wa mali za serikali.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Maafisa Bajeti wa Wizara nawa Ofisi za Uthibiti Ubora wa Shule Kanda mkoani Morogoro
Hayo yamesemwa Mkoani Morogoro na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha wakati wa Ufunguzi wa Mafunzo ya Maafisa Bajeti wa Wizara na wa Ofisi za Uthibiti Ubora wa Shule Kanda yenye lengo la kuboresha utendaji kazi hususani katika maandalizi ya Bajeti.

Kiongozi huyo amesema utoaji wa mafunzo haya utasaidia kutoa maarifa mapya na stadi zaidi katika utekelezaji wa majukumu ikiwa ni Pamoja na  kuongeza uwazi na uwajibikaji katika utendaji kazi.

Mkurugenzi wa Idara ya Uthibiti Ubora wa Shule kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Mwl Euphrasia Buchuma akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mafunzo ya Maafisa Bajetu wa Wizara na wa Ofisi za Uthibiti Ubora wa Shule Kanda Mkoani Morogoro

“Mkurugenzi wa Uthibiti Ubora wa shule amenieleza kuwa kulikuwa na changamoto katika uaandaji wa bajeti kwa kuwa haikuwa na uhalisia, natambua mwenye kujua hali halisi kwenye ofisi ya uthibiti ubora ni yule ambaye yuko katika ofisi husika za kanda na wilaya na kwa kuwa  wataalamu wa bajeti wameona kuna mapungufu ndiyo maana tumeitisha mafunzo haya ili katika kupanga bajeti iwe na uhalisia,”alisema Naibu Waziri Ole Nasha
Mwezeshaji kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Pendo Sianga akiwapitisha wajumbe kwenye utaratibu wa kuandaa bajeti wakati wa mafunzo ya bajeti mkoani Morogoro

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Ole Nasha amesema Serikali katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano imeweka mkazo katika kuimarisha Uthibiti Ubora wa Shule kwa kuwajengea uwezo wa kiutendaji Wathibiti Ubora na kuweka mazingira sahihi ya ufanyaji kazi.

Ametaja maboresho yaliyofanyika katika eneo hilo kuwa ni pamoja na  ununuzi wa magari 45 ya wathibiti ubora wa Shule kwa wilaya ambazo hazikuwa na magari Pamoja na Kujenga Ofisi 100 za Wathibiti na kuziwekea samani na vitendea kazi. Aidha Serikali pia imenunua pikipiki 2,894 za Maafisa elimu Kata ili kuimarisha usimamizi wa  shule, pamoja na kuwapatia mafunzo ya kiutendaji wathibiti Ubora wa shule 1,276.
Baadhi ya Washiriki wa mafunzo ya Bajeti Mkoani Morogoro wakifuatilia hotuba ya Ufunguzi ya Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha
Maboresho mengine ni Kuongeza idadi ya Maafisa Uthibiti Ubora wa shule 400 ngazi ya Wilaya na Kanda pamoja na kuanzisha ofisi mpya 5 za Uthibiti Ubora wa shule katika wilaya mpya za Songwe, Kigamboni, Ubungo, Chalinze na Ushetu ili kurahisisha utoaji huduma za uthibiti Ubora huku serikali ikijipanga kununua magari mengine mapya 65 kwa ajili ya idara hiyo.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Uthibiti Ubora wa Shule Mwl. Euphrasia Buchuma amesema mafunzo haya yanafanyika kutokana na changamoto ambazo zimekuwa zikibainika katika bajeti zinazoandaliwa ikiwa ni pamoja na kueleweshana taratibu za matumizi ya fedha kulingana na vifungu vilivyowekwa.
 
Mafunzo ya kuwajengea uwezo maafisa bajeti wa Wizara na wa Ofisi za Uthibiti Ubora wa shule za Kanda yameanza leo Februari 12, 2020 na yana jumla ya washiriki 70 kutoka Ofisi hizo na Wizara ya Elimu Makao makuu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni