Ijumaa, 14 Februari 2020

WAZIRI NDALICHAKO ATAKA USIMAMIZI THABITI WA MIRADI YA ELIMU

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako ametoa rai kwa watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kusimamia vizuri fedha za  miradi ya Elimu inayotelekezwa katika maeneo yao ili  ikamilike kwa wakati na ubora.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa uzinduzi wa Jengo la  Utawala la Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam, Jijini Dar es Salaam
Waziri Ndalichako ametoa rai hiyo Jijini Dar es Salaam wakati akizinduzia Jengo la Utawala la Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) lililokarabatiwa na kuongeza ukubwa ambapo amesema Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi za Miradi lakini haikamiliki kutokana na usimamizi mbovu hivyo kutaka watendaji hao kusimamia miradi ipasavyo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizindua Jengo la Utawala la Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam, Jijini Dar es Salaam
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano imefanya kazi kubwa sana katika kuboresha mazingira ya utoaji elimu  na kwamba kukamilika kwa mradi wa upanuzi wa Jengo la Utawala la Chuo Kishiriki cha DUCE ni sehemu tu ya mambo mengi ambayo Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na serikali yake imefanya.
Baadhi ya Wanajumuiya ya Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako wakati wa uzinduzi wa Jengo la Utawala la Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam, Jijini Dar es Salaam
Profesa Ndalichako aliongeza kuwa wakati Serikali ikiendelea na maboresho hayo, taasisi za elimu ya juu zinatakiwa kuendelea  kutekeleza wajibu wao ipasavyo ambao  ni kutoa taaluma, kufanya tafiti pamoja na kutoa huduma na ushauri kwa jamii.

“Vyuo Vikuu vimekuwa vikijikita katika utoaji wa taaluma wakati mwingine vinakuwa vikisahau jukumu la kufanya tafiti na ndio maana tunaona idadi ya machapisho imekuwa ikipungua mwaka hadi mwaka. Niwaambie tunapokuwa tunafanyiwa tathmini ya upangaji wa madaraja ya vyuo, sehemu ambayo mara nyingi imekuwa ikituangusha ni sehemu ya tafiti, kwa hiyo nitumie nafasi hii kuzikumbusha Taasisi za elimu ya juu kuendelea kufanya tafiti na tafiti zenyewe ziwe ni zile zinazotoa mchango moja kwa moja katika maendeleo ya nchi,” amesema Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanajumuiya wa Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam mara baada ya  kuzindua Jengo la utawala la chuo hicho,  jijini Dar es Salaam
Katika hatua nyingine Profesa Ndalichako ametoa wito kwa Vyuo vya Elimu ya Juu nchini kutumia vema mapato yao ya ndani yanayotokana na huduma wanazotoa  kama za ushauri na tafiti kwa maendeleo ya Vyuo ikiwa ni pamoja na  kutenga sehemu ya Mapato hayo ndani kugharamia masomo ya watumishi.

“Nakipongeza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kuweza kutumia fedha kutoka kwenye mapato  ya ndani kutoa ufadhili wa masomo kwa watanzania wenye ufaulu wa kiwango cha Juu. Huu ni mchango mkubwa kwa Taifa letu kwani unatoa fursa kwa watanzania ambao wamefaulu vizuri lakini kutokana na sababu mbalimbali wasingeweza kunufaika na mikopo itolewayo na Bodi ya Mikopo,” alisema Waziri Ndalichako.
 
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kishiriki cha Dar es Salaam ambae pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya DUCE Profesa William Anangisye amemuahidi Waziri Ndalichako kuendelea kusimamia vizuri matumizi ya fedha za Miradi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha jengo lililozinduliwa leo linatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuwa chachu ya maendeleo ya Chuo hicho.

“Mhe. Waziri nakuahidi kuwa majengo haya yatatunzwa vizuri na kutoa mchango mkubwa katika utekelezaji wa majukumu ya chuo,” amesema Prof. Anangisye.

Naye Kaimu Rasi wa Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), Prof. Stephen Maluka ameishukuru Serikali kwa namna inavyoendelea kuboresha mazingira ya utoaji elimu kwa Taasisi za elimu ya Juu ambapo amesema katika Chuo hicho upanuzi wa Jengo la utawala umeondoa changamoto iliyokuwepo ya ukosefu wa ofisi za watumishi huku akiiomba Serikali kuwapatia fedha kwa ajili ya kusomesha wataalamu wao.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni