Jumanne, 11 Februari 2020

Kongamano la Kimataifa la kuunganisha wanataaluma na wadau wa sekta ya Utalii na Ukarimu

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akiongea wakati wa kufunga Kongamano la Kimataifa la kuunganisha wanataaluma na wadau wa sekta ya utaliina ukarimu liliofanyika Jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha amesema taasisi za mafunzo na wadau wa sekta ya utalii wanahitajika kufanya kazi kwa pamoja ili kutatua changamto zilizopo ikiwemo nguvu kazi yenye weledi na ufanisi wa kutosha  katika tasnia hiyo.

Naibu Waziri Ole Nasha ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam wakati wa kufunga Kongamano la Kimataifa la kuunganisha wanataaluma na wadau wa sekta ya Utalii na Ukarimu ambapo amesema ushindani katika soko ni mkubwa hivyo kunahitajika maandalizi mazuri ya rasilimali watu ili kuweza kushindana katika soko la dunia.



Mmoja wa washiriki wa   Kongamano la Kimataifa la kuunganisha wanataaluma na wadau wa sekta ya utalii akipokea cheti cha ushiriki kutoka kwa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha wakati wa kufunga kongamano hilo Jijini Dar es Salaam.

Amesema Utalii ni moja ya Sekta inayolipatia  Taifa  fedha za kigeni akitolea mfano mwaka jana 2019 nchi ilipata fedha za kigeni dola  milioni 2.4 kutokana na utalii hivyo kukiwa na nguvu kazi yenye weledi na ufanisi wa kutosha nchi itaneemeka kupitia utalii.

“Hakika tunahitaji kuandaa vizuri rasilimali watu, nchi jirani zimepiga hatua kwenye kuvutia watalii sio kwamba wana vivutio vingi kuliko sisi ni kutokana na  pamoja na mambo mengine kuwa na nguvu kazi yenye weledi ndio maana kama Taifa tunawekeza katika kutayarisha vijana ili kuwa na nguvu kazi yenye weledi katika sekta ya utalii," amesema Naibu Waziri Ole Nasha.
Mmoja wa washiriki wa kongamano  la Kimataifa la kuunganisha wanataaluma na wadau wa sekta ya utalii  na Ukarimu Zera Mwanga kutoka Chuo cha Taifa cha Utalii cha Jijini Dar es Salaam akionesha cheti cha ushiriki mara baada ya kukabidhiwa.
Kiongozi huyo aliongeza kuwa kwa sasa Taifa letu linatoa kipaumbele katika kuimarisha viwanda ili kuleta mabadiliko ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuandaa nguvu kazi, hivyo ni vizuri kukawa na mfumo wa mafunzo pacha kati ya Taasisi za mafunzo na wamiliki wa viwanda.

“Ninawiwa kusema kuwa kongamano hili limekuja kwa wakati muafaka sana na Wizara yangu itayachukua kwa uzito mapendekezo yote yaliyotolewa ukizingatia kuwa kuimarisha muunganiko kati ya wanatasnia na wanataaluma ni moja ya vipaumbele katika wizara yangu ili kuhakikisha tunazalisha wahitimu bora wanaokidhi mahitaji ya soko,” aliongeza Naibu Waziri Ole Nasha. 

Naibu Waziri Ole Nasha amekipongeza chuo cha Taifa cha Utalii na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kuandaa mkutano wa kuwaunganisha wakufunzi na watoe huduma hiyo walio katika biashara ya Utalii kwani kwa pamoja wanaweza kutatua changamoto zilizopo.

Naye Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii, Dkt. Shogo Mlozi amesema kwa kushirikiana na vyuo vingine vinavyotoa mafunzo ya utalii wataendelea kuimarisha mpango wa utoaji mafunzo  kwa kufanya kazi karibu na watoa huduma ili kupata nguvu kazi yenye weledi na ujuzi. 
Baadhi washiriki wa kongamano  la Kimataifa la kuunganisha wanataalumana wadau wa sekta ya Utalii na Ukarimu wakifuatlia hotuba ya Naibu Waziri wa Elimi, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha wakati wa kufunga kongamano hilo jijini Dar es Salaam
Kwa upande wake mshiriki wa kongamano hilo kutoka VETA makao makuu,  Happiness Salema amesema ni vizuri kukawa na makongamano ya aina hii kwa kuwa yanawaleta pamoja watoa mafunzo na wamiliki wa viwanda, jambo ambalo linasaidia kuona changamoto zilizopo na kuweka mkakati kwani nchi zilizoendelea zinatumia mfumo huu katika kutoa mafunzo.

"Soko la hotelia na utalii liwe tayari kupokea mfumo wa mafunzo pacha hali kadhalika kuwa tayari kutoa nafasi kwa ajili ya walimu kupata ujuzi kwani kwa kufanya hivyo nchi itakuwa ya kwanza kuongoza kwenye sekta ya utalii na ukarimu," amesema Salema.

Kongamano la kimataifa la kuunganisha sekta ya Utalii na Ukarimu katika nchi zinazoendelea limefanyika kwa siku mbili Jijini Dar es Salaam na limewakutanisha  wadau  na wanataaluma katika sekta ya Utalii na Ukarimu kutoka nchi zinazoendelea.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni