Walimu zaidi ya
4000 wa shule za msingi nchini wamepatiwa mafunzo ya kukuza stadi za Kusoma, Kuandika
na Kuhesabu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa
(BRN) unaolenga kuhakikisha walimu wote wanaofundisha darasa la I na II wanakuwa
mahiri katika ufundishaji wa Stadi za KKK
Akizungumzia mafunzo
hayo wakati wa ufunguzi Mhe. Kassim Majaliwa Kassim (MB) Naibu Waziri (Elimu),
Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI alisema Serikali imefanya juhudi za makusudi kuendesha
mafunzo haya ili kuhakikisha inawajengea uwezo walimu ili waweze kuwasaidia wanafunzi
kumudu kikamilifu stadi za KKK.
Alisema ni vema
wale wanaosimamia kuratibu walimu kuja kwenye mafunzo kuhakikisha wanaokuja ni
wale ambao kweli wanahusika na kufundisha darasa la I na II, na kwamba ufuatiliaji
ufanyike kuona kuwa walimu wa madarasa yaliyolengwa ndio wanakuja kwenye mafunzo
hayo.
Mhe. Majaliwa amewataka
walimu waliochaguliwa kushiriki mafunzo haya kutumia fursa hii vizuri na kuwa chachu
ya kuleta mabadiliko chanya katika ufundishaji wa Stadi za KKK. ‘’Napenda kuwakumbusha
kuwa mmechaguliwa miongoni mwa walimu walio wengi kushiriki mafunzo haya hivyo,
itumieni fursa mliyoipata vizuri na hata mkirejea katika vituo vyenu vya kazi mkaache
mtindo wa kufanya kazi kwa mazoea bali kujituma na kutanguliza uzalendo” Alisema
Naibu Waziri Majaliwa.
Naye Mkurugenzi wa Idara
ya Kituo cha Mafunzo ya Mtaala Bibi Fika Mwakabungu alisema Mafunzo ya Kukuza Stadi
za Kusoma Kuandika na Kuhesabu ni endelevu na yanafanyika kwa ushirikiano kati ya
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na
Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI na yanalenga kuwafikia walimu 18,000 kutoka mikoa
14 ya Tanzania Bara.
Akiitaja Mikoa itakayohusika
ni pamoja na Arusha, Dar Es Salaam, Morogoro, Pwani, Rukwa, Ruvuma,Tanga,Singida,
Kilimanjaro, Manyara, Kagera, Katavi, Geita na Mwanza.
Kwa upande mwingine Mhe. Majaliwa alisema Serikali imeanzisha chombo kimoja maalumu
kitakachosimamia stahili za Walimu na kurahisisha usimamizi wa upandishaji wa madaraja
sambamba na kurekebisha mishahara ikiwa ni hatua zilizochukuliwa na Serikali katika
kutatua changamoto zinazowakabili walimu.
Pia alisema Serikali
imeridhia na kutoa muundo mpya wa kada za walimu ambao utawawezesha walimu waliokuwa
wamefikia ukomo katika muundo wa zamani kunufaika na muundo mpya katika bajeti ya
Mwaka 2015/16.