Jumatatu, 20 Aprili 2015

WALIMU ZAIDI YA 4000 WAPATIWA MAFUNZO YA KUKUZA STADI ZA KKK



Walimu zaidi ya 4000 wa shule za msingi nchini wamepatiwa mafunzo ya kukuza stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) unaolenga kuhakikisha walimu wote wanaofundisha darasa la I na II wanakuwa mahiri katika ufundishaji wa Stadi za KKK

Akizungumzia mafunzo hayo wakati wa ufunguzi Mhe. Kassim Majaliwa Kassim (MB) Naibu Waziri (Elimu), Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI alisema Serikali imefanya juhudi za makusudi kuendesha mafunzo haya ili kuhakikisha inawajengea uwezo walimu ili waweze kuwasaidia wanafunzi kumudu kikamilifu stadi za KKK.

Alisema ni vema wale wanaosimamia kuratibu walimu kuja kwenye mafunzo kuhakikisha wanaokuja ni wale ambao kweli wanahusika na kufundisha darasa la I na II, na kwamba ufuatiliaji ufanyike kuona kuwa walimu wa madarasa yaliyolengwa ndio wanakuja kwenye mafunzo hayo.

Mhe. Majaliwa amewataka walimu waliochaguliwa kushiriki mafunzo haya kutumia fursa hii vizuri na kuwa chachu ya kuleta mabadiliko chanya katika ufundishaji wa Stadi za KKK. ‘’Napenda kuwakumbusha kuwa mmechaguliwa miongoni mwa walimu walio wengi kushiriki mafunzo haya hivyo, itumieni fursa mliyoipata vizuri na hata mkirejea katika vituo vyenu vya kazi mkaache mtindo wa kufanya kazi kwa mazoea bali kujituma na kutanguliza uzalendo” Alisema Naibu Waziri Majaliwa.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Kituo cha Mafunzo ya Mtaala Bibi Fika Mwakabungu alisema Mafunzo ya Kukuza Stadi za Kusoma Kuandika na Kuhesabu ni endelevu na yanafanyika kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI na yanalenga kuwafikia walimu 18,000 kutoka mikoa 14 ya Tanzania Bara.

Akiitaja Mikoa itakayohusika ni pamoja na Arusha, Dar Es Salaam, Morogoro, Pwani, Rukwa, Ruvuma,Tanga,Singida, Kilimanjaro, Manyara, Kagera, Katavi, Geita na Mwanza.

Kwa upande mwingine Mhe. Majaliwa alisema Serikali imeanzisha chombo kimoja maalumu kitakachosimamia stahili za Walimu na kurahisisha usimamizi wa upandishaji wa madaraja sambamba na kurekebisha mishahara ikiwa ni hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kutatua changamoto zinazowakabili walimu.

Pia alisema Serikali imeridhia na kutoa muundo mpya wa kada za walimu ambao utawawezesha walimu waliokuwa wamefikia ukomo katika muundo wa zamani kunufaika na muundo mpya katika bajeti ya Mwaka 2015/16.












 




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni