Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Uongozi
wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kushirikiana na Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia kuona namna ya kuboresha mitaala ya chuo hicho ili kifikie
viwango vya Elimu ya Juu.
Mhe.
Majaliwa ametoa wito huo Jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa kongamano
la maadhimisho ya Kumbukizi ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere ambapo amesema mpaka sasa chuo hicho kina majengo, sifa na kwamba elimu
inayotolewa katika chuo hicho ndio inasisitizwa nchini.
Ameutaka
uongozi wa chuo hicho kutia mkazo katika mafunzo ya uongozi hususan yale yenye
mwelekeo wa kujenga uzalendo na kuendelea kutumia fursa ya kuwepo kwa
makongamano kukuza uelewa wa jamii ya watanzania kuhusu umuhimu wa kuenzi
falsafa za Mwalimu katika umoja, upendo, uzalendo, uadilifu na mshikamano wa
kitaifa.
Aidha
Mhe. Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua kwa kujenga
misingi ya amani, umoja na kuleta maendeleo ya jamii nchini kwa vitendo na
kuwataka watanzania kuzingatia maadili, uzalendo na utaifa katika
uwajibikaji wa kila siku, kuungana kwa
pamoja bila kujali itikadi za kisiasa au kikabila katika kulinda na kudumisha
tunu hizo.
“Nimpongeze
Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
juhudi anazochukua ili kuhakikisha anairejesha nchi yetu kwenye misingi yake ya
awali ambayo ni kuwa na viongozi waadilifu, wazalendo na wenye kulinda amani na
kudumisha umoja katika jamii, watanzania wote tunapaswa kuunga mkono jitihada
hizi na kuzilinda kwa nguvu zote,” amesema Mhe. Majaliwa.
Naye
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema ni
vizuri kumuenzi Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kuwa
ni mtu ambaye amelipigania Taifa na kuliletea ukombozi na ameipongeza Serikali
ya Awamu ya Tano kwa kufuata nyayo za Baba wa Taifa.
Waziri
Ndalichako ameeleza kufurahishwa na ushiriki wa wanafunzi katika kongamano hilo
kwa kuwa linawapa fursa ya kupata uelewa mpana zaidi wa kile wanachofundishwa darasani,
na kwamba taifa linawategemea kuwa chachu ya mabadiliko katika nchi.
Awali
Mwenyekiti wa Bodi ya Uendeshaji wa Chuo hicho, Steven Wassira alimweleza
Waziri Mkuu kuwa wanaomba katika kumenzi Baba wa Taifa Chuo hicho kipandishwe
hadhi na kuwa Chuo Kikuu na kwamba mazingira yake yaboreshwe yawe na hadhi ya
Hayati Baba wa Taifa.
Kwa
upande wake Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Prof. Shadrack
Mwakalila amesema, Uongozi wa chuo hicho unaendelea na maboresho ya kutoa
taaluma yenye kujenga uzalendo kwa vijana wa kitanzania.
Kongamano
la Maadhimisho ya Kumbukizi ya Baba wa Taifa limechagizwa na mada isemayo
Mchango wa Mwalimu Nyerere katika kujenga Amani, Umoja na Kuleta Maendeleo ya
Jamii nchini.