Naibu Waziri wa
Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha amesema serikali inaendelea na
mikakati ya kumlinda mtoto wa kike ili aweze kupata elimumsingi bila kukatiza.
Naibu Waziri ametoa
kauli hiyo jijini Dar es Salaam alipokutana na Waziri wa Maendeleo na Mahusiano
ya Kimataifa kutoka Sweden, Peter Erickson ambapo amesema mikakati hiyo inamuwezesha mtoto wa kike kusoma katika
mazingira salama.
"Mikakati
tunayoendelea nayo ya kuwawezesha watoto wa kike wasikatishe masomo yao ni
kutoa ushauri nasaha na kuwawezesha kutambua kuwa elimu ni muhimu kwao na
wazazi wao ili kuwaepusha na vikwazo vyovyote ambavyo vinaweza kusababisha
kukatisha masomo yao," amesisitiza
Ole Nasha.
Ole Nasha amesema
serikali ina mifumo mizuri ambayo imekuwa ikitumika kwa miaka mingi katika
kumsaidia mtoto wa kike aliyepata ujauzito kuweza kuendelea na masomo yake
katika kupata ujuzi na utaalamu utakaomsaidia kujiletea maendeleo yake.
"Mtoto wa kike
anapopata mimba akiwa shuleni ametengenezewa mifumo mingine itakayomuwezesha
kupata ujuzi na utaalamu huku akiendelea kulea mtoto wake, mifumo hiyo ni
pamoja na elimu ya ufundi na elimu ya watu wazima," ameelezea Ole Nasha.
Akizungumzia
mahusiano yaliyopo kati ya Tanzania na Sweden Naibu Waziri amesema ni ya
miaka mingi inayokaribia 50 ambapo katika miaka yote hiyo nchi ya Sweden
imeweka alama katika kufadhili miradi na
programu mbalimbali za elimu.
Ole Nasha ameitaja
baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo
(P4R) ambao umewezesha kujengwa na kukarabati miundombinu mbalimbali ya shule
na Mradi wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (LANES) ambao umesaidia katika
kuinua ubora wa elimu nchini.
Naibu Waziri
ameongeza kuwa mbali na miradi hiyo pia Sweden imesaidia kujenga uwezo katika
maeneo ya utafiti katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha
Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) ambapo jumla ya wahadhiri 63 wanaosoma
Shahada ya Umahiri na 43 wanaosoma Shahada ya Uzamili wamefadhiliwa na Sweden.
Akizungmza katika
kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard
Akwilapo amesema mradi wa LANES unaofadhiliwa kwa kiwango kikubwa na Sweden
umesaidia katika kuwajengea uwezo walimu wa madarasa ya chini kwa kuwapa mbinu
za kufundisha madarasa yenye watoto wengi na kuandaa vifaa ya kufundishia na
kujifunzia kwa wanafunzi wa madarasa ya chini.
Naye Waziri wa
Maendeleo na Mahusiano ya Kimataifa kutoka Sweden, Peter Erickson amesema Sweden
imekuwa na mahusiano mazuri na Tanzania kwa muda mrefu ambapo imekuwa
ikifadhili miradi mbalimbali ya Elimu yenye kulenga kuinua ubora wa Elimu.
Aidha, waziri huyo
amesema ameridhishwa na jinsi serikali inavyoendelea kuboresha elimu na kuahidi
kuendelea na programu za kuisaidia serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwa sababu imetekeleza vizuri miradi mbalimbali inayofadhiliwa na nchi yake.
"Nimeongea na
Viongozi wa elimu ambao wameelezea vizuri jinsi mtoto wa kike anavyowezeshwa
katika kupata ujuzi na utaalamu baada ya kupata mimba, hivyo wafadhili
mbalimbali kupitia GPE wamekubali kutoa kiasi cha dola za kimarekani milioni 90
kuboresha Elimu ya msingi," amesema Peter Erickson.