Jumatano, 22 Mei 2019

SERIKALI KUENDELEA NA MIKAKATI YA KUMLINDA MTOTO WA KIKE ILI AWEZE KUMALIZA ELIMUMSINGI



Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha amesema serikali inaendelea na mikakati ya kumlinda mtoto wa kike ili aweze kupata elimumsingi bila kukatiza.

Naibu Waziri ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam alipokutana na Waziri wa Maendeleo na Mahusiano ya Kimataifa kutoka Sweden, Peter Erickson ambapo amesema mikakati  hiyo inamuwezesha mtoto wa kike kusoma katika mazingira  salama.

"Mikakati tunayoendelea nayo ya kuwawezesha watoto wa kike wasikatishe masomo yao ni kutoa ushauri nasaha na kuwawezesha kutambua kuwa elimu ni muhimu kwao na wazazi wao ili kuwaepusha na vikwazo vyovyote ambavyo vinaweza kusababisha kukatisha masomo yao,"  amesisitiza Ole Nasha.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha akisalimiana na Waziri wa Maendeleo na Mahusiano ya Kimataifa kutoka Sweden, Peter Erickson aliyefika na ujumbe wake katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
Ole Nasha amesema serikali ina mifumo mizuri ambayo imekuwa ikitumika kwa miaka mingi katika kumsaidia mtoto wa kike aliyepata ujauzito kuweza kuendelea na masomo yake katika kupata ujuzi na utaalamu utakaomsaidia kujiletea maendeleo yake.

"Mtoto wa kike anapopata mimba akiwa shuleni ametengenezewa mifumo mingine itakayomuwezesha kupata ujuzi na utaalamu huku akiendelea kulea mtoto wake, mifumo hiyo ni pamoja na elimu ya ufundi na elimu ya watu wazima," ameelezea Ole Nasha.

Akizungumzia mahusiano yaliyopo kati ya Tanzania na Sweden Naibu Waziri amesema  ni ya  miaka mingi inayokaribia 50 ambapo katika miaka yote hiyo nchi ya Sweden imeweka alama  katika kufadhili miradi na programu mbalimbali za elimu.

Ole Nasha ameitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (P4R) ambao umewezesha kujengwa na kukarabati miundombinu mbalimbali ya shule na Mradi wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (LANES) ambao umesaidia  katika  kuinua ubora wa elimu nchini.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha akizungumza na Waziri wa Maendeleo na Mahusiano ya Kimataifa kutoka Sweden, Peter Erickson aliyefika na ujumbe wake katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri ameongeza kuwa mbali na miradi hiyo pia Sweden imesaidia kujenga uwezo katika maeneo ya utafiti katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) ambapo jumla ya wahadhiri 63 wanaosoma Shahada ya Umahiri na 43 wanaosoma Shahada ya Uzamili wamefadhiliwa na Sweden.

Akizungmza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo amesema mradi wa LANES unaofadhiliwa kwa kiwango kikubwa na Sweden umesaidia katika kuwajengea uwezo walimu wa madarasa ya chini kwa kuwapa mbinu za kufundisha madarasa yenye watoto wengi na kuandaa vifaa ya kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi wa madarasa ya chini.

Naye Waziri wa Maendeleo na Mahusiano ya Kimataifa kutoka Sweden, Peter Erickson amesema Sweden imekuwa na mahusiano mazuri na Tanzania kwa muda mrefu ambapo imekuwa ikifadhili miradi mbalimbali ya Elimu yenye kulenga kuinua ubora wa Elimu.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha, Katibu Mkuu Dkt. Leonard Akwilapo, Naibu Katibu Mkuu Ave Maria Semakafu wakiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Maendeleo na Mahusiano ya Kimataifa kutoka Sweden, Peter Erickson pamoja na ujumbe alioongozana nao katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
Aidha, waziri huyo amesema ameridhishwa na jinsi serikali inavyoendelea kuboresha elimu na kuahidi kuendelea na programu za kuisaidia serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu imetekeleza vizuri miradi mbalimbali inayofadhiliwa na nchi yake.

"Nimeongea na Viongozi wa elimu ambao wameelezea vizuri jinsi mtoto wa kike anavyowezeshwa katika kupata ujuzi na utaalamu baada ya kupata mimba, hivyo wafadhili mbalimbali kupitia GPE wamekubali kutoa kiasi cha dola za kimarekani milioni 90 kuboresha Elimu ya msingi," amesema Peter Erickson.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni