Alhamisi, 18 Juni 2020

SERIKALI KUTUMIA ZAIDI YA SHILINGI MILIONI 700 KUWAENDELEZA WABUNIFU

Serikali imetenga kiasi cha Shilingi milioni 750 kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa ajili ya kuwaendeleza wabunifu 70 walioshiriki katika fainali za Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) 2020.


Hayo yamesemwa Jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako wakati akitangaza Washindi wa MAKISATU 2020 ambapo amesema Serikali imepanga kuendeleza ubunifu unaozalishwa ili kuwa bidhaa na kuchangia katika harakati za kukuza uchumi.


Waziri Ndalichako amefafanua kuwa MAKISATU ni moja ya mikakati ya Serikali ya kuibua, kutambua na kuendeleza ubunifu na ugunduzi unaofanywa na watanzania hususani wa ngazi za chini.


Waziri Ndalichako ametumia fursa hiyo kuwashukuru wadhamini wa MAKISATU 2020 ambao wamekuwa sehemu ya kuendeleza Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ambao ni benki ya CRDB, VODACOM Foundation, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na Mfuko wa Ubunifu kwa Maendeleo ya Binadamu (HDIF)







Jumatano, 17 Juni 2020

NDALICHAKO ATANGAZA MIHULA NA TAREHE ZA KUANZA MITIHANI

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako leo Juni 17, 2020 ametangaza tarehe za kuanza kwa mitihani ya Taifa ya Darasa la Saba, Kidato cha Nne na Upimaji wa kitaifa wa Darasa la Nne na Kidato cha Pili.

Akizungumza na Waandishi wa habari Jijini Dodoma, Prof. Ndalichako amesema Darasa la Saba watafanya Mtihani kuanzia tarehe 7 - 8 Oktoba, 2020 wakati Kidato cha Pili wataanza mitihani Novemba 9 - 20, 2020. Darasa la Nne watafanya Novemba 25 - 26, 2020 wakati Kidato cha Nne watafanya kuanzia Novemba  23 hadi Disemba 11, 2020.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako akiongea na Waandishi wa habari (hawapo pichani) Jijini Dodoma wakati akitangaza mihula na tarehe za kuanza mitihani ya Taifa kwa shule za msingi na sekondari nchini.

Profesa Ndalichako amezungumzia mihula mipya ya shule ambapo amesema shule za msingi na sekondari watamaliza muhula wa kwanza wa masomo Agosti 28, 2020 na kuanza muhula wa pili utakaoishia Disemba 18, 2020. Amesema kuwa ili kukamilisha muhtasari wa masomo, shule zitalazimika kuongeza saa 2 za masomo kwa kila siku ili kufidia muda uliopotea huku akisisitiza kuwa maelekezo ya kuongeza muda hayatahusu madarasa ya awali.

Aidha, Profesa Ndalichako ametoa ufafanuzi kuhusu mihula kwa wanafunzi wa Kidato cha Tano ambapo amesema wanafunzi hao wataanza masomo Juni 29, 2020 kama ilivyoagizwa na kukamilisha muhtasari wa masomo yao na kufanya mitihani yao ya kumaliza Kidato cha Tano ifikapo Julai 24, 2020. Wanafunzi hawa wataanza rasmi masomo ya Kidato cha Sita Julai 27, 2020.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako (katikati) akiongea na Waandishi wa habari (hawapo pichani) Jijini Dodoma wakati akitangaza mihula na tarehe za kuanza mitihani ya Taifa kwa shule za msingi na sekondari nchini. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu, Profesa James Mdoe na kulia ni Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Ave Maria Semakafu.

Waziri Ndalichako ameagiza Uongozi wa shule zote kuhakikisha wanafunzi, walimu na wafanyakazi wengine wote wanazingatia maelekezo ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona kama yalivyotolewa katika Mwongozo wa Wizara ya Afya ikiwemo kuhakikisha kuwa shule zote zinanunua vifaa vya kutosha kwa ajili ya kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni.

Jumamosi, 13 Juni 2020

WATUMISHI WIZARA YA ELIMU WAPATIWA MAFUNZO JUU YA MAGONJWA SUGU

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa James Mdoe amesema afya ya mtumishi ni nguzo kubwa na muhimu ya uendeshaji wa shughuli za taasisi yeyote. 

Akizungumza Jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uelewa watumishi wa Wizara hiyo kuhusu Virusi vya Ukimwi (VVU), Ukimwi na Magonjwa Sugu yasiyoambukizwa, Profesa Mdoe amesema watumishi wasipopewa mafunzo ya uelewa juu ya magonjwa hayo kuna uwezekano wa Taifa kupoteza nguvu kazi. 
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa James Mdoe akiongea na watumishi wa Wizara ya Elimu kabla ya kuanza mafunzo ya kuwajengea uelewa watumishi hao kuhusu Virusi vya Ukimwi (VVU), Ukimwi na Magonjwa Sugu yasiyoambukizwa.

Naibu Katibu Mkuu Mdoe amesema magonjwa hayo yanaweza kupoteza maisha ya watumishi ama kusababisha utendaji kazi wa watumishi kushuka kutokana na kuugua mara kwa mara na kuwa na afya dhoofu. 

“Watumishi ni muhimu katika taasisi yoyote, hivyo afya zao ni muhimu sana kwa taasisi. Katika utumishi wa umma kuna miongozo iliyotolewa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Umma na Utawala Bora ambayo inaelekeza namna bora ya kutoa huduma kwa watumishi,” amesema Naibu Katibu Mkuu. 

Baadhi ya watumishi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uelewa watumishi hao kuhusu Virusi vya Ukimwi (VVU), Ukimwi na Magonjwa Sugu yasiyoambukizwa.

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu, Moshi Kabengwe akiongea na watumishi wa Wizara ya Elimu kabla ya kuanza mafunzo ya kuwajengea uelewa watumishi hao kuhusu Virusi vya Ukimwi (VVU), Ukimwi na Magonjwa Sugu yasiyoambukizwa 

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Moshi Kabengwe akizungumza katika mafunzo hayo amesema Wizara imeamua kutoa mafunzo hayo ili kuwawezesha watumishi kupata uelewa na mbinu za kukabiliana na magonjwa hayo.

Baadhi ya watumishi wa Wizara ya Elimu wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uelewa kuhusu Virusi vya Ukimwi (VVU), Ukimwi na Magonjwa Sugu yasiyoambukizwa.

Ijumaa, 22 Mei 2020

WAZIRI NDALICHAKO ATANGAZA TAREHE ZA MITIHANI KWA KIDATO CHA SITA NA VYUO VYA UALIMU

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako amezitaka  shule zote zenye wanafunzi wa kidato cha sita kuanza maandalizi ya kupokea wanafunzi hao ili waanze masomo Juni 1 2020 kama ilivyoelekezwa.

Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo Jijini Dodoma wakati alipoongea na waandishi wa habari ambapo amesema ni vizuri kwa shule za bweni zikaanza kupokea wanafunzi hao Mei 30, 2020 ili waanze masomo katika muda uliopangwa.
 
Amesema wakati shule za bweni zikipokea wanafunzi Mei 30, 2020 shule za kutwa nazo zianze maandalizi huku akilitaka Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) kusambaza ratiba za mtihani mapema kwa ajili ya maandalizi.

"Mitihani ya Kidato cha sita na Vyuo vya Ualimu inaanza Juni 29, 2020 na kukamilika Julai 16, 2020 hivyo NECTA sambazeni ratiba za mtihani mapema ili shule  na vyuo vianze maandalizi na kumbukeni mtapaswa kutoa  matokeo ya mtihani huo kabla ya Agosti 30, 2020,"alisema Wziri Ndalichako.

Kwa upande wa Vyuo vikuu na Vyuo vya Kati waziri   Ndalichako ameyataka mabaraza pamoja na Seneti ya Vyuo kupanga ratiba za masomo kwa lengo la kufidia muda wa masomo ambao wanafunzi wamepoteza wakiwa nyumbani na kuwasilisha ratiba hizo Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania(TCU) ili mwaka huu wa masomo ukamilike bila kuathiri ratiba za masomo kwa nwakali 2020/2021

Pia amevitaka vyuo hivyo kuwasilisha nyaraka muhimu zinazohitajika Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu ili Mikopo kwa wanafunzi na ada zao ziweze kutolewa mapema kwa kuwa tayari Serikali imeshatoa jumla ya sh Bilioni 122.8  kwa ajili hiyo.

Itakumbukwa kwamba Mei 21 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli wakati akihutubia wananchi kupitia Vyombo vya habari alitangaza kufungua vyuo vya elimu ya Juu, Kati na Masomo kwa wanafunzi wa kidato cha sita.