Jumamosi, 29 Januari 2022

WAZIRI MKENDA AITAKA DIT KUANZA KUTENGENEZA VIPURI


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi kutoka Wizarani na Menejimenti ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) wakati alipotembelea taasisi hiyo Januari 28, 2022.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda ameitaka Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kujitanua zaidi kwa kutengeneza vipuri vya vyombo vya moto ikiwemo vya bajaji na pikipiki.

Ameyasema hayo leo Januari 28, 2022 Jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea Taasisi hiyo ili kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa hapo ambapo amesema tunaweza kukua kiteknolojia kwa kuboresha vitu ambavyo tayari vimeshatengenezwa na nchi nyingine.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akizungumza na Menejimenti ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) wakati alipotembelea taasisi hiyo Januari 28, 2022.

"Nimefurahi sana kuona mna kampuni inayosaidia kubiasharisha bidhaa za ubunifu ila niwatake mboreshe kwa kutengeneza vipuri ambavyo vinahitajika sana kama vya bajaji na pikipiki," amesema Prof. Mkenda.

Aidha Waziri Mkenda ameipongeza taasisi hiyo kwa kuwa na kampuni inayosaidia kubiasharisha bunifu mbalimbali na kuwataka  DIT kuhamisha ujuzi wa kiteknolojia kutoka nchi nyingine na kuja kuutumia hapa nchini katika uzalishaji wa bidhaa zitakazokidhi mahitaji ya jamii.

"Tunaweza tukaleta nchini kitu ambacho kimezalishwa mfano nchi ya Uturuki kisha tukaangalia uwezekano wa kukitengeneza na kukiuza ndani na nje ya nchi ili kukuza uchumi wetu," amesema Prof. Mkenda.

Katika hatua nyingine Waziri Mkenda ameusisitiza uongozi wa DIT kuendelea kujenga na kukuza ushirikiano na taasisi nyingine hasa za nje ya nchi ili kubadilishana wataalamu watakaosaidia kuendelea kukuza teknolojia nchini.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda (mwenye tai) akiwa ameongozana na Mkuu wa Taasisi ya DIT, Prof. Preksedis Ndomba (kushoto) na maafisa wengine kutoka Wizarani na DIT,  wakati Waziri huyo alipotembelea taasisi hiyo Januari 28, 2022.

Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi hiyo, Prof. Preksedis Ndomba amesema wamepokea maelekezo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi ili kuboresha utendaji wa taasisi hiyo.

Jumanne, 30 Novemba 2021

ELIMU YA MICHEZO NA SANAA KUIMARISHWA KATIKA VYUO VYA UALIMU

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul akiongea na wananchi (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa mashindano ya Umoja wa Michezo na Sanaa kwa Vyuo vya Ualimu Tanzania (UMISAVUTA) uliofanyika mkoani Mtwara Novemba 29, 2021. Mashindano hayo yanaendelea hadi Desemba 5, 2021.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Profesa Joyce Ndalichako amesema kuwa Sera, Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo vitasimamiwa ipasavyo ili kuimarisha ufundishaji na  ujifunzaji wa michezo shuleni na katika Vyuo vya Ualimu.

Hayo yamesemwa kwa niaba yake Novemba 29, 2021 mkoani Mtwara na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul wakati akifungua mashindano ya Umoja wa Michezo na Sanaa kwa Vyuo vya Ualimu Tanzania (UMISAVUTA) yanayoendelea mkoani humo hadi Desemba 5, 2021.

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. James Mdoe akiongea na wananchi (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa mashindano ya Umoja wa Michezo na Sanaa kwa Vyuo vya Ualimu Tanzania (UMISAVUTA) uliofanyika mkoani Mtwara Novemba 29, 2021. Mashindano hayo yanaendelea hadi Desemba 5, 2021

Amesema Rais Samia Suluhu alitoa maelekezo ya kuboresha mitaala na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika nyakati tofauti ameagiza kutekelezwa kwa ufundishaji wa masomo ya sanaa na michezo,  hivyo Wizara inaendelea kutekeleza maagizo hayo ili kufikia azma ya Serikali ya kuhakikisha vipawa vya wanamichezo na Sanaa vinakuzwa kuanzia shuleni  na pia Taifa linakuwa na wananchi wenye nguvu na afya njema kuweza kulitumikia Taifa.

Baadhi ya wananchi wakimsikiliza mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul (hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa mashindano ya Umoja wa Michezo na Sanaa kwa Vyuo vya Ualimu Tanzania (UMISAVUTA) uliofanyika mkoani Mtwara Novemba 29, 2021. Mashindano hayo yanaendelea hadi Desemba 5, 2021.

Aidha, katika hatua nyingine Naibu Waziri Gekul amewataka washiriki wote wa mashindano hayo kuhakikisha wanachukua tahadhari zote za maambukizi ya ugonjwa wa Uviko-19 katika kipindi chote cha mashindano hayo, na kuwahimiza kupata chanjo ya ugonjwa huo.

Mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul akipita kukagua timu mbalimbali zinazoshiriki mashindano ya UMISAVUTA yanayoendelea mkoani Mtwara.

Awali, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. James Mdoe alisema lengo la mashindano hayo ni kukuza na kuendeleza vipaji kwa walimu tarajali ili nao waweze kwenda kukuza vipaji vya wanafunzi katika michezo na sanaa.

Aidha Naibu Katibu Mkuu huyo amemuhakikishia mgeni rasmi kuwa Wizara itahakikisha mashindano hayo yatafanyika kwa nidhamu na maadili hadi yanapofikia tamati.

Naye Mwenyekiti wa Walimu wa Vyuo vya Ualimu vya Serikali Tanzania Bara, Mwl. Dorothy Mhaiki amesema mashindano hayo yamehusisha wanachuo 665 kutoka vyuo 36  vya ualimu vikiwemo 35 vya Serikali na kimoja binafsi.

Timu za mpira wa miguu kutoka Kanda ya Ziwa na Kanda ya Kati ndizo zilizofungua dimba la mashindano hayo ambapo timu ya Kanda ya Ziwa iliibuka na ushindi wa mabao 3 - 0.

Ijumaa, 15 Oktoba 2021

"TUNAKWENDA KUJENGA VYUO VYA VETA KILA MKOA" Naibu Waziri wa Elimu, Saya...

SERIKALI YAJIZATITI KUHAKIKISHA MTOTO WA KIKE ANASOMA BILA CHANGAMOTO YOYOTE

 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema Serikali  inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha inalinda haki za mtoto wa kike kielimu, kiuchumi na kijamii na kuhakikisha pia anaingia katika ulimwengu wa kidigitali.

Waziri Ndalichako amesema hayo Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla fupi iliyoandaliwa na Balozi wa Uingereza nchini David Concar katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya mtoto wa kike ambapo amesema ni vizuri tunapoadhimisha siku ya mtoto wa kike kukumbuka kuwapa nafasi watoto hao kwani itasaidia kujua uwezo mkubwa walio nao ili kuwaendeleza.

Kauli mbiu ya Mwaka huu ya siku ya mtoto wa Kimataifa ni “kizazi cha kidigitali kizazi changu” ambapo Waziri Ndalichako amesema inalenga     kuikumbusha jamii nzima kuhusu haki sawa watoto wote katika teknolojia ya kidigitali ili waweze kuitumia kwa maendeleo na ustawi wa jamii bila kusahau watoto wa kike wenye mahitaji maalum.

 “Kwa mfano wapo wabunifu mbalimbali wa kike kwenye masuala ya kidigitali lakini hawajitokezi kwa kuwa aidha mazingira sio rafiki au kutojiamini kwa kuwa jamii imeshawajengea mtazamo kuwa wao hawana uwezo kwa hiyo hata yule mwenye uwezo anakuwa anaona aibu kujitokeza kwamba labda kitu alichobuni sio kizuri. Tuwatie shime watoto wa kike waweze kujitokeza kuonesha ubunifu wao na uwezo wao katika masuala ya teknolojia na kidijitali,” amesema Waziri Ndalichako

Akizungumzia jitihada zinazofanywa na Serikali kuhakikisha mtoto wa kike anasoma bila changamoto amesema Serikali inaendelea kusimamia sheria ambazo zinalenga kuwalinda watoto wa kike husasani kupata elimu ambapo Mwaka 2016 ilifanya marekebisho ya sheria ya elimu kwa lengo la kuendela kumlinda  mtoto wa  kike katika Elimu.

Ameongeza kuwa Serikali imeimarisha suala na unasihi na malezi shuleni pamoja na  kuendelea kujenga hosteli kwa ajili ya watoto wa kike ili kuhakikisha hawatembei umbali mrefu wa kwenda na kurudi shule ili kumuepushia changamoto ambazo zinaweza kukatisha masomo yake.

 Waziri Ndalichako amesema Kupitia Mradi wa Kuimarisha elimu ya Sekondari (SEQUIP) Serikali inakwenda kujenga shule 26 maalum kwa ajili ya mtoto wa kike, moja kwa  kila Mkoa zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1000 na tayari fedha za kuanzia kujenga wa shule 10 zimeshapokelewa. Zote hizo ni juhudi za kuhakikisha mtoto wa kike anasoma bila changamoto lakini pia ushiriki wa mtoto wa kike katika sayansi na teknolojiana masula ya kidigitali kwa kuwa zitakuwa za mchepuo wa sayansi.

 

Waziri Ndalichako ametumia nafasi hiyo kuwashukuru na kuwapongeza wadau wote wanaojihusisha na masuala ya haki za mtoto wa kike ambao wamejitoa kutumia rasilimali zao, muda, ujuzi kuhakikisha wanalinda haki ya mtoto wa kike, wafadhili wetu na washirika wa maendeleo ambao katika mipango yao wamekuwa wakihakikisha suala la mtoto wa kike wanalipa kipaumbele

Kwa upande wake Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, David  Concar amesema Serikali ya Tanzania imekuwa na ushirikiano na Serikali ya Uingereza katika maeneo tofauti hususani la kumwezesha mtoto wa kike ambapo hivi karibuni Waziri Mkuu wao ametangaza kuongeza msaada wa paundi milioni 55 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya elimu nchini.

Nae Kaimu Mkurugenzi Mkazi wa British Council Atiya Sumar amesema badala ya kuendelea kuzungumzia changamoto katika utoaji wa elimu kwa mtoto wa kike  sasa tuendelee kufanyia kazi changamoto wanazopitia ili waweze kusoma bila changamoto yoyote.

Mwanafunzi Sarafina Frank kutoka Shule ya sekondari Mikocheni amesema matumizi chanya ya kidigitali yanaweza kutumika katika kupambana na kutokomeza mila na desturi zenye madhara kwa mtoto wa kike na hivyo kuwaondolea adha na vikwazo vinavyokwamisha kufikia malengo. Ameiomba Serikali kuboresha huduma za kidigitali hasa kwa kumlenga mtoto wa kike kwa kumuwezesha vitendea kazi ikiwemo simu au kompyuta aweze kuvitumia katika kujifunza.