Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha inalinda haki za mtoto wa kike kielimu, kiuchumi na kijamii na kuhakikisha pia anaingia katika ulimwengu wa kidigitali.
Waziri Ndalichako amesema hayo Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla fupi iliyoandaliwa na Balozi wa Uingereza nchini David Concar katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya mtoto wa kike ambapo amesema ni vizuri tunapoadhimisha siku ya mtoto wa kike kukumbuka kuwapa nafasi watoto hao kwani itasaidia kujua uwezo mkubwa walio nao ili kuwaendeleza.
Kauli mbiu ya Mwaka huu ya siku ya mtoto wa Kimataifa ni “kizazi cha kidigitali kizazi changu” ambapo Waziri Ndalichako amesema inalenga kuikumbusha jamii nzima kuhusu haki sawa watoto wote katika teknolojia ya kidigitali ili waweze kuitumia kwa maendeleo na ustawi wa jamii bila kusahau watoto wa kike wenye mahitaji maalum.
“Kwa mfano wapo wabunifu mbalimbali wa kike kwenye masuala ya kidigitali lakini hawajitokezi kwa kuwa aidha mazingira sio rafiki au kutojiamini kwa kuwa jamii imeshawajengea mtazamo kuwa wao hawana uwezo kwa hiyo hata yule mwenye uwezo anakuwa anaona aibu kujitokeza kwamba labda kitu alichobuni sio kizuri. Tuwatie shime watoto wa kike waweze kujitokeza kuonesha ubunifu wao na uwezo wao katika masuala ya teknolojia na kidijitali,” amesema Waziri Ndalichako
Akizungumzia jitihada zinazofanywa na Serikali kuhakikisha mtoto wa kike anasoma bila changamoto amesema Serikali inaendelea kusimamia sheria ambazo zinalenga kuwalinda watoto wa kike husasani kupata elimu ambapo Mwaka 2016 ilifanya marekebisho ya sheria ya elimu kwa lengo la kuendela kumlinda mtoto wa kike katika Elimu.
Ameongeza kuwa Serikali imeimarisha suala na unasihi na malezi shuleni pamoja na kuendelea kujenga hosteli kwa ajili ya watoto wa kike ili kuhakikisha hawatembei umbali mrefu wa kwenda na kurudi shule ili kumuepushia changamoto ambazo zinaweza kukatisha masomo yake.
Waziri Ndalichako amesema Kupitia Mradi wa Kuimarisha elimu ya Sekondari (SEQUIP) Serikali inakwenda kujenga shule 26 maalum kwa ajili ya mtoto wa kike, moja kwa kila Mkoa zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1000 na tayari fedha za kuanzia kujenga wa shule 10 zimeshapokelewa. Zote hizo ni juhudi za kuhakikisha mtoto wa kike anasoma bila changamoto lakini pia ushiriki wa mtoto wa kike katika sayansi na teknolojiana masula ya kidigitali kwa kuwa zitakuwa za mchepuo wa sayansi.
Waziri Ndalichako ametumia nafasi hiyo kuwashukuru na kuwapongeza wadau wote wanaojihusisha na masuala ya haki za mtoto wa kike ambao wamejitoa kutumia rasilimali zao, muda, ujuzi kuhakikisha wanalinda haki ya mtoto wa kike, wafadhili wetu na washirika wa maendeleo ambao katika mipango yao wamekuwa wakihakikisha suala la mtoto wa kike wanalipa kipaumbele
Kwa upande wake Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, David Concar amesema Serikali ya Tanzania imekuwa na ushirikiano na Serikali ya Uingereza katika maeneo tofauti hususani la kumwezesha mtoto wa kike ambapo hivi karibuni Waziri Mkuu wao ametangaza kuongeza msaada wa paundi milioni 55 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya elimu nchini.
Nae Kaimu Mkurugenzi Mkazi wa British Council Atiya Sumar amesema badala ya kuendelea kuzungumzia changamoto katika utoaji wa elimu kwa mtoto wa kike sasa tuendelee kufanyia kazi changamoto wanazopitia ili waweze kusoma bila changamoto yoyote.
Mwanafunzi Sarafina Frank kutoka Shule ya sekondari Mikocheni amesema matumizi chanya ya kidigitali yanaweza kutumika katika kupambana na kutokomeza mila na desturi zenye madhara kwa mtoto wa kike na hivyo kuwaondolea adha na vikwazo vinavyokwamisha kufikia malengo. Ameiomba Serikali kuboresha huduma za kidigitali hasa kwa kumlenga mtoto wa kike kwa kumuwezesha vitendea kazi ikiwemo simu au kompyuta aweze kuvitumia katika kujifunza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.