Ijumaa, 24 Julai 2015

Ziara ya Viongozi wa Elimu kutoka Nigeria walipotembelea Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Taasisi zake. Ziara hiyo ilianza Jumatatu, Julai 20, 2015.







Alhamisi, 2 Julai 2015


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
 
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MATAPELI WANAOOMBA RUSHWA KWA KUJITAMBULISHA KAMA VIONGOZI WA ELIMU
Kumejitokeza kundi la watu ambao ni matapeli wanaoomba rushwa kwa kujitambulisha kama viongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na kutumia namba za simu zilizoandikishwa kwa kutumia majina ya viongozi hao. Namba hizo hutumika kwa muda na baada ya kufanikisha  lengo lao, watu hao huzifunga na hivyo kutokupatikana tena hewani.
Majina ya viongozi yanayotumika katika utapeli huo ni ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Katibu Mkuu, Kamishna wa Elimu na ya baadhi ya Wakurugenzi katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Namba hizo za simu hutumika na matapeli hao kwa kuwapigia watu wanaohitaji huduma katika ofisi za elimu na kuwaomba wawatumie  fedha kupitia namba hizo ili kufanikisha upatikanaji wa huduma wanazozihitaji kutoka katika ofisi hizo. Huduma zinazotajwa ni pamoja na kufanikisha usajili wa shule na vyuo.
 Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inawatahadharisha wananchi kujiepusha na kundi hili la matapeli na ifahamike kuwa huduma zote zinazotolewa katika ofisi za elimu zikiwemo za usajili wa shule hazitolewi kwa rushwa au malipo ya aina yoyote.
Maelezo kamili kuhusu usajili wa shule yanapatikana katika ofisi za Ukaguzi wa Shule za Wilaya na Kanda na ofisi za Makao Makuu ya Wizara, au chumba namba 21 na 36 hapa wizarani. Tafadhali wasiliana na Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu au Kamishna wa Elimu endapo utapigiwa simu na  mtu  usiyemfahamu atakayejitambulisha kwako na kudai fedha ili afanikishe usajili wa shule au kupata huduma zingine wizarani. Usikubali kudanganywa na kutoa fedha kwa huduma inayopatikana bure.
Imetolewa na:
Katibu Mkuu,
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
02 Julai, 2015
 
 

Jumanne, 12 Mei 2015

Waziri Mkuu afungua Maadhimisho ya Wiki ya Elimu Kitaifa

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Peter Pinda amewataka wazazi na jamii kutambua umuhimu wa watoto kupata elimu na kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanaandikishwa na wanahudhuria bila kukosa hadi kuhitimu elimu ya msingi. Aidha almewataka walimu kufundisha ipasavyo ili elimu itolewayo iwe bora kwa maendeleo ya Taifa.

Waziri Mkuu alisema hayo wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya wiki ya elimu kitaifa yanayofanyika kwa mara ya pili nchini katika uwanja wa Jamhuri, Mjini Dodoma. Maadhimsho haya yaliyoanza tarehe Mei 11 yanakwenda sambamba na maonesho ya wadau mbalimbali wa Elimu na  yanatarajiwa kuhitimishwa siku ya Ijuma tarehe Mei 15 na Rais wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.

Aidha, katika ufunguzi huu Mhe. Waziri Mkuu ametoa tuzo kwa Shule, Mikoa na Halmashauri zenye ufaulu uliotukuka na zilizoongeza ufaulu kwa kiwango cha juu katika mitihani 2014 ikilinganisha na matokeo ya 2013. Sambamba na utoaji wa tuzo pia alitoa pikipiki kwa Waratibu Elimu Kata sita waliowakirisha Waratibu Elimu Kata wa nchi nzima

 
 
 



 
 
 
 
 









 

Jumanne, 5 Mei 2015

AWAMU YA PILI YA MAFUNZO YA KKK - CHUO KIKUU CHA DODOMA

Awamu ya pili ya mafunzo ya kuwajengea uwezo walimu wa shule za Msingi wanaofundisha darasa la I na II yakiendelea katika Chuo Kikuu cha Dodoma ambapo walimu wengine zaidi ya elfu nne wameshiriki kutoka mikoa ya Kilimanjaro, Manyara, Kagera, Katavi, Geita na Mwanza

 Katika awamu ya kwanza mikoa iliyoshiriki ni pamoja na Arusha, Dar es Salaam, Morogoro, Pwani, Rukwa, Ruvuma, Tanga na Singida







.

Jumatano, 29 Aprili 2015



JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI




MAADHIMISHO YA WIKI YA ELIMU MWAKA 2015

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) inawatangazia wabunifu wote wa namna ya kutoa elimu kwa njia mbalimbali kuwasilisha andiko la ubunifu wao, ili waweze kushiriki katika maonesho yatakayokwenda sambamba na maadhimisho ya Wiki ya Elimu itakayoanza tarehe 11- 15 Mei 2015 katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma.

Andiko la ubunifu liwe limewasilishwa kwa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo, 7 Mtaa wa Magogoni, 11479 DAR ES SALAAM siku ya Jumamosi tarehe 02/05/2015.



Elimu Msingi ni Haki ya Kila Mtoto kwa Maendeleo ya Taifa


IMETOLEWA NA:
Katibu Mkuu,
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi