Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ameupongeza Uongozi wa
shule ya Dar es Salaam International Academy kwa kuwajengea uwezo na kuona
umuhimu wa kuwafundisha na kuwapa nafasi wanafunzi kujifunza wenyewe.
Prof.
Ndalichako ametoa pongezi hizo jijini Dar es Salaam aliposhiriki katika maonesho
mbalimbali ya wanafunzi wa darasa la tano katika shule hiyo ambapo amesema
wanafunzi hao wamefundishwa kutafuta taarifa mbalimbali kutokana na mada
walizopewa.
“Nimefurahi
kuona wanafunzi wa darasa la tano wanaonesha ubunifu katika kuangalia matatizo
ya jamii kwani hata mada walizoangalia zinaendana na hali halisi ya sasa ambayo
serikali imekuwa ikiwekea msisitizo kama masuala ya jinsia, magonjwa ya homa ya
ini na Ebola, dawa za kulevya pamoja na Teknolojia,” amesema Ndalichako.
Waziri
Ndalichako amesema katika kutafuta taarifa wanafunzi hao wameonyesha vipaji vya
hali ya juu wakati wa kuandaa mada za maonyesho kwani wametumia mitandao pamoja
na kuwahoji watu waliowaona muhimu kuwapatia taarifa zilizowawezesha
kukamilisha mada zao kwa ajili ya maonyesho hayo.
Aidha,
Waziri Ndalichako ametoa wito kwa walimu kuwawezesha na kuwapa nafasi wanafunzi
katika kuwa na ubunifu, kujiamini na kuweza kutafuta taarifa mbalimbali katika
kujifunza kwani wanafunzi wa kitanzania wana uwezo wa kufanya mambo makubwa
sana lakini wanakwama kutokana na kushindwa kujiamini na uoga wakati shuleni ni
sehemu ambayo vipaji hivyo vinaweza kuendelezwa.
“Suala la kujiamini ni changamoto kubwa kwa
watanzania wengi, wana uwezo, akili na vipaji lakini wanakuwa hawajiamini hili
ni tatizo, kwa hiyo tuendelee kuwa na
maonyesho kama haya ambayo yatawajengea wanafunzi wetu uwezo, kujiamini,
kuonyesha yale wanayoweza na kutoogopa kusema mbele za watu,” amesisitiza Waziri Ndalichako.
Aidha,
Waziri Ndalichako amesema hata katika shule za serikali maonyesho kama hayo
yanafanyika katika ngazi ya shule za
sekondari ambayo yanaanza katika ngazi ya shule, wilaya na kilele inakuwa
katika ngazi ya Kitaifa hata hivyo wameahidi kuangalia namna ya kuanza
kushirikisha wanafunzi wa shule za msingi kwani kufanya hivyo inawezesha
kuwaandaa wabunifu tangu wakiwa katika umri mdogo.
Akizungmzia
mkakati wa serikali wa kutambua na kukuza ubunifu nchini Waziri Ndalichako
amesema kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia inazo atamizi ambazo zinatumika
kuendeleza ubunifu lakini pia imeona si rahisi kila mtu kuweza kufika katika
Tume hiyo hivyo imeanza utaratibu wa kuanzisha katika ngazi za Halmashauri
ambapo mwaka huu mwongozo umetoka wa kuangalia namna gani wabunifu
wakitambulika wanaweza kuendelezwa.
“Pia
katika vyuo vikuu vyetu kuna hatamizi kwa mfano Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
Nelson Mandela kuna atamizi ambazo zinafanya vizuri sana na wao wamejikita
katika mazao na kuangalia vitu ambavyo vinaweza kuweka sumu katika mazao lengo
ni kuhakikisha tunaongeza wigo ili vipaji wa watanzania viweze kuendelezwa,”
amesema Ndalichako.
Naye
Mkuu wa Shule hiyo, Fawzya Hirji amesema shule hiyo imejipanga kuhakikisha
kunakuwa na ushirikiano kati ya walimu,
wanafunzi na wazazi katika kuwawezesha wanafunzi hao kuwa na uwezo wa ubunifu,
kujiamini na kutumia mitandao katika kutafuta taarifa mbalimbali zinazowapatia maarifa
ya kujua mambo mbalimbali duniani.