Jumatano, 23 Septemba 2015

Waziri Kawambwa afanya ziara AIMS – Tanzania


Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dkt. Shukuru Kawambwa mwishoni mwa wiki alitembelea Taasisi ya  African  Institute for  Mathematical  Sciences - Next Einstein Initiative (AIMS-NEI) kampasi ya Tanzania na kuzungumza na viongozi na wanafunzi wa Shahada ya Uzamili katika masomo ya  Hisabati na Sayansi kwa mwaka 2015/16. Taasisi ya AIMS hapa nchini imeanzisha kampasi yake Bagamoyo, mkoani Pwani ambapo hivi sasa inatumia kwa muda majengo ya Alpha Zulu Villa na baadaye itatumia majengo ya Old Boma na Datoo yaliyoko Bagamoyo mjini baada ya kufanyiwa ukarabati.
Wanafunzi 45 kutoka nchi mbalimbali za Afrika wamedahiliwa kuanza masomo katika taasisi ya AIMS – Tanzania kwa mwaka 2015/16 wakiwemo Watanzania 17 na wengine wanatoka nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Cameroon, DRC, Msumbiji, Nigeria, Zimbabwe, Afrika Kusini, Sudani na mmoja anatoka Uingereza.
Kuanza kwa mafunzo hayo ni jitihada za Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete kuhakikisha kuwa Taifa linakuwa na wataalam wa kutosha katika Nyanja za Hisabati na Sayansi. Mheshimiwa Rais alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa taasisi hiyo alipokuwa ziarani nchini Canada mwishoni mwa mwaka juzi.
 
 


 

 

 

Jumatano, 16 Septemba 2015


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MAONESHO YA MATUMIZI YA TEHAMA KATIKA ELIMU YA MSINGI
Wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi inaandaa maonesho ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa ajili ya kuongeza Ufanisi katika Ujifunzaji na Ufundishaji katika Elimu ya Msingi nchini.
Maonesho haya yanalenga kutoa fursa kwa wabunifu, wauzaji na wadau wa elimu kuonesha bunifu mbalimbali za teknolojia ya habari na mawasiliano zitakazoweza kutumiwa katika Elimu ya Msingi ili kuongeza ufanisi katika Ujifunzaji na Ufundishaji wa stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) na katika masomo mengine.
Maenesho haya yatafanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere mkoani Dar es Salaam, kuanzia tarehe 28/9/2015 hadi tarehe 02/10/2015
Washiriki wa maonesho haya wanatakiwa kujiandikisha kupitia wavuti: www.lanes-moe.go.tz, kabla ya tarehe 24/9/2015. Aidha, washiriki watakaokidhi vigezo vinavyotakiwa, kazi zao zitatumika katika Ujifunzaji na Ufundishaji katika Elimu ya Msingi Nchini.
Wizara inawahimiza wabunifu wote  wa ndani na nje ya nchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maonesho haya.
Imetolewa na
Katibu Mkuu
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
13/09/2015

Jumatatu, 10 Agosti 2015

Serikari yakabidhiwa Shule ya Sekondari

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mhe.Dkt. Shukuru Kawambwa amekabidhiwa shule ya sekondari na Balozi wa Korea Kusini Mhe. Chung Il iliyojengwa na Shirika la Good Neighbors International na Washirika wake. Shule hiyo ya sekondari ya Fukayosi imejengwa wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani kwa msaada wa mashirika mbalimbali ikiwemo KOICA kutoka Korea ya Kusini.Ijumaa, 24 Julai 2015

Ziara ya Viongozi wa Elimu kutoka Nigeria walipotembelea Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Taasisi zake. Ziara hiyo ilianza Jumatatu, Julai 20, 2015.Alhamisi, 2 Julai 2015


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
 
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MATAPELI WANAOOMBA RUSHWA KWA KUJITAMBULISHA KAMA VIONGOZI WA ELIMU
Kumejitokeza kundi la watu ambao ni matapeli wanaoomba rushwa kwa kujitambulisha kama viongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na kutumia namba za simu zilizoandikishwa kwa kutumia majina ya viongozi hao. Namba hizo hutumika kwa muda na baada ya kufanikisha  lengo lao, watu hao huzifunga na hivyo kutokupatikana tena hewani.
Majina ya viongozi yanayotumika katika utapeli huo ni ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Katibu Mkuu, Kamishna wa Elimu na ya baadhi ya Wakurugenzi katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Namba hizo za simu hutumika na matapeli hao kwa kuwapigia watu wanaohitaji huduma katika ofisi za elimu na kuwaomba wawatumie  fedha kupitia namba hizo ili kufanikisha upatikanaji wa huduma wanazozihitaji kutoka katika ofisi hizo. Huduma zinazotajwa ni pamoja na kufanikisha usajili wa shule na vyuo.
 Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inawatahadharisha wananchi kujiepusha na kundi hili la matapeli na ifahamike kuwa huduma zote zinazotolewa katika ofisi za elimu zikiwemo za usajili wa shule hazitolewi kwa rushwa au malipo ya aina yoyote.
Maelezo kamili kuhusu usajili wa shule yanapatikana katika ofisi za Ukaguzi wa Shule za Wilaya na Kanda na ofisi za Makao Makuu ya Wizara, au chumba namba 21 na 36 hapa wizarani. Tafadhali wasiliana na Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu au Kamishna wa Elimu endapo utapigiwa simu na  mtu  usiyemfahamu atakayejitambulisha kwako na kudai fedha ili afanikishe usajili wa shule au kupata huduma zingine wizarani. Usikubali kudanganywa na kutoa fedha kwa huduma inayopatikana bure.
Imetolewa na:
Katibu Mkuu,
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
02 Julai, 2015