Alhamisi, 14 Machi 2019

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE HUDUMA NA MAENDELEO YA JAMII YAKAGUA MRADI WA UPANUZI NA UKARABATI WA JENGO LA UTAWALA DUCE



Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. James Mdoe wakati alipowasili katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) kwa ajili ya kikao cha pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ilipotembelea chuo hicho kukagua utekelezaji wa Mradi wa upanuzi na ukarabati wa jengo la Utawala la chuo hicho.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imeiagiza serikali kuhakikisha inafanikisha upatikanaji wa kiasi cha Shilingi Bilioni 1.1 kwa ajili ya kukamilisha ukarabati na upanuzi wa jengo la Utawala la Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE).

Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Peter Serukamba Jijini Dar es Salaam baada ya kukagua utekelezaji wa Mradi huo wa ukarabati na upanuzi wa jengo hilo ambapo amesema kuchelewa kumalizika kwa wakati kunaweza kusababisha kuongezeka kwa gharama za ujenzi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kupanda kwa gharama za vifaa.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako na Mwenyekiti Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Mhe. Peter Serukamba wakipitia taarifa ya utekelezaji wa mradi wa upanuzi wa jengo la Utawala la Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE).
Mhe. Serukamba amesema kiasi hicho cha fedha ni muhimu kikapatikana kwa sasa ambapo kazi ya ujenzi na ukarabati ikiwa inaendelea kwani itasaidia pia kuondoa usumbufu kama jengo hilo litakamilishwa nusu na kuanza kutumika.

“Kucheleweshwa kwa fedha zilizobaki zitafanya jengo hili kujengwa kwa gharama kubwa sana kwani vifaa vya ujenzi vinapanda, lakini pia haitakuwa vizuri kumalizia upande mmoja wa jengo watu waingie wafanye kazi baadaye wapishe ujenzi inakuwa ni usumbufu kwa watumishi” amesema Mhe. Serukamba.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako na baadhi ya Viongozi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) wakielekea katika jengo la Utawala linalokarabatiwa.
Aidha, Mhe. Serukamba amekitaka Chuo hicho kwa kushirikiana na serikali kuhakikisha maktaba ya Chuo hicho inakuwa kamilifu na kupewa kipaumbele ili kuwa na maktaba inayojitosheleza kwa kuwa na eneo lenye ubora, vitabu vya kutosha ikiwemo vitabu vya elektroniki.  Vilevile ameutaka Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuweka utaratibu wa wanafunzi wa DUCE kuweza kutumia maktaba ya kisasa iliyopo katika kampasi yake kuu

Pamoja na hayo Kamati pia imeitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kusimamia madai ya watumishi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ujumla na kuhakikisha madai stahiki yanalipwa.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako pamoja na Mwenyekiti na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii wakisikiliza taarifa ya maendeleo ya kazi ya upanuzi na ukarabati wa jengo la Utawala katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE).
Awali Rasi wa Duce, Prof. Bernadeta Killian ameieleza Kamati hiyo kuwa Mradi huo wa upanuzi na ukarabati jengo la Utawala unagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 3.2 kwa ujumla, kiasi ambacho kinajumuisha gharama za ujenzi, ukarabati, kuweka mifumo ya TEHAMA pamoja na samani za ndani za jengo hilo ambapo mpaka sasa bado kiasi cha Shilingi Bilioni 1.1 kinahitajika ili kukamilisha.

Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ameishukuru Kamati hiyo kwa kutembelea Mradi huo na ameahidi kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Kamati hiyo.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii pamoja na viongozi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kukagua maendeleo ya kazi ya upanuzi na ukarabati wa jengo la utawala katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE).

SERIKALI IMESEMA INATAMBUA MCHANGO WA VYUO VIKUU BINAFSI HAPA NCHINI


Rais Mstaafu wa awamu Tatu Benjamin William Mkapa amekipongeza Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordan JUCo kwa kutimiza jubilee ya miaka 25 ya utoaji huduma ya Elimu ya Juu nchini  na kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa wa Chuo hicho na vyuo vingine binafsi katika kuwezesha upatikanaji wa elimu nchini hususan elimu ya juu .

Mhe. Mkapa amesema hayo katika kilele cha sherehe za Jubilee  zilizofanyika katika Chuo hicho jijini Morogoro na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi. Aidha amesema pamoja na kazi nzuri wanayofanya vyuo binafsi, ada zinazotozwa katika vyuo hivyo bado ziko juu, hivyo amevitaka kuhahakisha wanajiendesha kwa gharama nafuu bila kuathiri ubora na kuhakikisha wanatoza ada kwa viwango ambavyo Watanzania walio wengi watamudu na kuweza kupata elimu hiyo kwa maendelo yao na taifa kwa ujumla.

“Niseme kuwa Elimu pekee ndiyo inachangia maendeleo ya mtu mmoja mmoja na baadae Taifa kwa ujumla, hivyo ni vyema gharama za ada ziwe ni zile ambazo wananchi wa kawaida watamudu, ikumbukwe kuwa wananchi walio wengi wanategemea mikopo inayotolewa na Serikali, sasa Vyuo binafsi ni vyema vikaliangalia hili,” alisema Mzee Mkapa.


Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin William Mkapa akiwa ameongozana na viongozi mbalimbali wakati wa maadhimisho ya Jubilee ya miaka 25 ya Chuo Kikuu Cha Jordan kilichopo Mkoani Morogoro.

Awali akizungumza katika Jubilee hiyo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya utoaji elimu ya juu ili kuongeza ubora na kuwa haitavifumbia macho vyuo ambavyo havitatii na kuzingatia vigezo, sheria, taratibu na kanuni za uendeshaji wa vyuo hapa nchini.

“Nitoe wito kwa vyuo vyote nchini kuhakikisha vinakidhi vigezo vya uendeshaji wa vyuo, tofauti na hapo serikali haitasita kuchukua hatua stahiki kwa vyuo vitakavyokwenda kinyume. Lengo la serikali ni kuhakikisha Elimu bora inatolewa nchini ili kuzalisha wataalamu wenye uwezo na maarifa kwa ukuaji wa uchumi,”alisema Waziri Ndalichako.


Waziri Ndalichako amesema hadi sasa Tanzania kuna vyuo vikuu na vyuo vikuu vishiriki 49 ambapo kati ya hivyo  34 ni vyuo binafsi ambayo ni sawa na asilimia 69.4, hivyo Serikali inatambua mchango mkubwa wa Vyuo binafsi na amekipongeza Chuo Cha Jordan kwa kutimiza miaka 25. 


Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa akizindua Kitabu Maalumu wakati wa maadhimisho ya kutimiza miaka 25 kwa Chuo Kikuu Cha Jordan, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia pia alishiriki maadhimisho hayo.

Aidha Waziri Ndalichako alisisitiza pia kuwa serikali inaendelea kuimarisha Bodi ya Mikopo ili kutoa mikopo zaidi kwa wanafunzi ambapo alisema kumekuwa na ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaopata mikopo  hiyo ambapo kutoka mwaka 2004/05 hadi  mwaka 2018/19 wanufaika wa mikopo kwa ujumla ni 480,405.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Steven Kebwe  amesema Chuo Cha Jordan kutimiza miaka 25 ni hatua kubwa na kuwa Chuo hicho ni miongoni mwa vyuo vya mfano katika mkoa huo kwa sababu mkoa haujawahi kupokea taarifa za wanafunzi wa Chuo hicho kujihusisha na makundi wala vitendo viovu. Aidha ameahidi kushirikiana na chuo hicho kwa kutumia watalaamu wanaoandaliwa hapo kwa ajili ya maendeleo ya Mkoa.
Baadhi ya Wanafunzi na wageni mbalimbali wakifuatilia hotuba mbalimbali za Viongozi wakati wa Maadhimisho ya Miaka 25 ya Chuo Kikuu cha Jordan kilichopo Mkoani Morogoro.