Alhamisi, 4 Julai 2019

OLE NASHA ATAKA COSTECH KUSIMAMIA HAKI MILIKI ZA KAZI ZA WABUNIFU


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha ameitaka Tume ya Sayansi na Teknolojia nchini kusimamia wabunifu kupata haki ya umiliki wa bunifu zao.

Naibu Waziri Ole Nasha ametoa agizo hilo jijini Dar es Salaam, wakati alipotembelea mabanda ya Taasisi za Elimu zilizo chini ya Wizara zilizoshiriki maonesho ya 43 ya biashara ya kimataifa maarufu kwa jina la Sabasaba na kukutana na mmoja wa wabunifu aliyeomba serikali imtambue kwa kuwa amebuni nyenzo ya kufundishia mfumo wa sayari shuleni.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha akipata maelezo ya bunifu mbalimblai zilizopo katika banda la VETA wakati alipotembelea maonesho ya 43 ya biashara za kimataifa jijini Dar es Salaam.
Alisema ni vizuri wabunifu wanapoandaa kazi zao zikatambuliwa na kupatiwa haki miliki ya bunifu au ugunduzi walioufanya lakini pia kuendelea kuwafadhili ili waweze kukuza bunifu zao.

“Ninyi COSTECH hakikisheni bunifu mbalimbali nilizoziona hapa sabasaba katika mabanda yetu haziishii katika maonesho tu, bali zikuzwe na tumieni nafasi hii ya maonesho kuwakutanisha wabunifu na wafanya biashara kwa ajili ya uzalishaji,” alisema Naibu Waziri Ole Nasha.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akiangalia moja ya bidhaa zinazozalishwa na VETA wakati alipotembelea banda la Taasisi hiyo katika maonesha ya bishara za kimataifa Jijini Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine Waziri Ole Nasha ameipongeza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa kazi nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya ya kukuza ubunifu na ujuzi na kuwataka kuendelea kusimamia bunifu mbalimbali za wanafunzi ili ziingie katika soko na kutatua changamoto mbalimbali za kijamii.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akipata maelezo ya matumizi ya vitabu kutoka kwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania Dkt. Aneth Komba wakati alipotembelea banda la TET katika maonesho ya Sabasaba jijini Dar es Salaam.
Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia zilizoshiriki maonesho ya Sabasaba kwa mwaka 2019 ni pamoja na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE), Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu Mzumbe, Tume ya Nguvu za Atomiki nchini (TAEC), Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST).

NDALICHAKO AWASHUKIA VIKALI SKAUTI TANZANIA

Jumatano, 3 Julai 2019

WATAALAMU WA SAYANSI WATAKIWA KUSHAURI MATUMIZI YA SAYANSI NA TEKNOLOJIA KATIKA MAENDELEO


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amewataka wanasayansi wanachama wa Akademia ya Sayansi Tanzania (TAAS), kutumia ujuzi wao kutoa ushauri wa matumizi ya Sayansi na Teknolojia katika shughuli za maendeleo nchini.

Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa Baraza la tatu la Akademia hiyo ambapo amewataka kuhakikisha wanasimamia vyema ustawi wa Baraza hilo ili liweze kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha Sayansi, Teknolojia na Ubunifu vinatumika kama nyenzo ya kuleta maendeleo endelevu ya uchumi nchini.

“Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21 unalenga kujenga uchumi wa viwanda ili kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025; Mpango umeeleza bayana kuwa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ni nyezo muhimu katika azma hivyo serikali na wataalamu kama ninyi tuna wajibu wa kuhamasisha matumizi ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu katika jamii,” alisema Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Baraza la tatu la Akademia ya Sayansi Tanzania Jijini Dar es Salaam.
Alisema ni vizuri Baraza hilo likajikita katika kukuza na kuendeleza Ubunifu na Ugunduzi wa maarifa ya kisayansi katika nyanja za kijamii na kiuchumi kwa kutoa ushauri na maoni kuhusu Sera na mikakati ya kuendeleza Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ikiwa ni pamoja na kufanya tafiti za kisayansi zenye kutoa utatuzi wa changamoto katika jamii hasa kipindi hiki dunia inapoelekea katika mapinduzi ya nne ya viwanda.

Kiongozi huyo aliongeza kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imechukua hatua mbalimbali za kuhamasisha matumizi ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya kufundishia katika ngazi zote za elimu ikiwa ni pamoja na kuzindua Mwongozo wa kutambua na kuendeleza Ugunduzi, Ubunifu na Maarifa, kuanzisha vituo vya kulea ubunifu na ugunduzi na kwamba itaendelea kushirikiana na Baraza hilo ili kuhakikisha masuala ya sayansi, teknolojia na ubunifu yanafanikiwa.
Rais mteule wa Baraza Jipya la Akademia ya Sayansi Tanzania, Prof. Yunus Mgaya akizungumza wakati wa uzinduzi wa Baraza hilo uliofanyika Jijini Dar es Salaam.
“Utaona katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali imewawezesha wabunifu 30 kwa kutoa zaidi ya Shilingi bilioni 1, hii inatokana na ukweli kwamba inawatambua na ina lengo la kuendeleza kazi zao,” aliongeza Waziri Ndalichako.

Katika hatua nyingine Waziri Ndalichako amempongeza Rais Mteule wa Baraza jipya la Akademia ya Sayansi Tanzania Prof. Yunus mgaya pamoja na mabaraza yaliyotangulia kwa kuendeleza Akademia hiyo iliyoanza rasmi mwaka 2005, kwani wanachama wake wamekuwa wakifanya kazi mbalimbali za kujitolea na kwamba anatambua mchango wao katika kukuza na kuendeleza matumizi ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
Wajumbe wa Baraza la Akademia ya Sayansi Tanzania wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako wakati wa   uzinduzi wa baraza hilo uliofanyika Jijini Dar es Salaam.
Awali akizungumza katika hafla hiyo Rais huyo mteule wa TAAS Mgaya amesema Akademia hiyo imejipanga kuongeza wanachama na kufanya tafiti, kusaidia wanasayansi kuchapisha tafiti hizo katoka majarida yanayotambulika kimataifa, lakini kubwa zaidi ni kuhuisha matumizi ya Sayansi na teknolojia katika maendeleo ya uchumi.

Baraza la Akademia ya Sayansi Tanzania lina wanachama wanasayansi 131 kutoka nyanja mbalimbali za Sayansi nchini.
Mmoja wa wajumbe la Baraza jipya la Akademia ya Sayansi Tanzania, Prof. Julie Makani akipokea vitendea kazi kutoka kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako.

Rais wa Baraza la Akademia ya Sayansi Tanzania aliyemaliza muda wake, Prof. Esther Mwaikambo akiongea wakati wa hafla ya uzinduzi wa Baraza jipya uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Mtendaji Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt. Amos Nungu akiongea wakati wa hafla ya uzinduzi wa Baraza jipya uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza la tatu la Akademia ya Sayansi Tanzania mara baada ya uzinduzi wa Baraza hilo.