Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia
Prof. Joyce Ndalichako amewataka wanasayansi wanachama wa Akademia ya Sayansi
Tanzania (TAAS), kutumia ujuzi wao kutoa ushauri wa matumizi ya Sayansi na
Teknolojia katika shughuli za maendeleo nchini.
Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo jijini
Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa Baraza la tatu la Akademia hiyo
ambapo amewataka kuhakikisha wanasimamia vyema ustawi wa Baraza hilo ili liweze
kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha Sayansi, Teknolojia na Ubunifu
vinatumika kama nyenzo ya kuleta maendeleo endelevu ya uchumi nchini.
“Mpango wa Pili wa Maendeleo
wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21 unalenga kujenga uchumi wa viwanda ili
kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025; Mpango umeeleza bayana kuwa Sayansi,
Teknolojia na Ubunifu ni nyezo muhimu katika azma hivyo serikali na wataalamu kama ninyi tuna wajibu wa
kuhamasisha matumizi ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu katika jamii,” alisema
Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Baraza la tatu la Akademia ya Sayansi Tanzania Jijini Dar es Salaam. |
Alisema ni vizuri Baraza hilo likajikita katika kukuza na
kuendeleza Ubunifu na Ugunduzi wa maarifa ya kisayansi katika nyanja za kijamii
na kiuchumi kwa kutoa ushauri na maoni kuhusu Sera na mikakati ya kuendeleza Sayansi,
Teknolojia na Ubunifu ikiwa ni pamoja na kufanya tafiti za kisayansi zenye
kutoa utatuzi wa changamoto katika jamii hasa kipindi hiki dunia inapoelekea
katika mapinduzi ya nne ya viwanda.
Kiongozi huyo
aliongeza kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imechukua hatua mbalimbali za
kuhamasisha matumizi ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya kufundishia katika ngazi zote za elimu ikiwa
ni pamoja na kuzindua Mwongozo
wa kutambua na kuendeleza Ugunduzi, Ubunifu na Maarifa, kuanzisha vituo vya
kulea ubunifu na ugunduzi na kwamba itaendelea kushirikiana na Baraza hilo ili
kuhakikisha masuala ya sayansi, teknolojia na ubunifu yanafanikiwa.
Rais mteule wa Baraza Jipya la Akademia ya Sayansi Tanzania, Prof. Yunus Mgaya akizungumza wakati wa uzinduzi wa Baraza hilo uliofanyika Jijini Dar es Salaam. |
“Utaona katika mwaka wa fedha 2018/2019
Serikali imewawezesha wabunifu 30 kwa kutoa zaidi ya Shilingi bilioni 1, hii
inatokana na ukweli kwamba inawatambua na ina lengo la kuendeleza kazi zao,”
aliongeza Waziri Ndalichako.
Katika hatua
nyingine Waziri Ndalichako amempongeza Rais Mteule wa Baraza jipya la Akademia
ya Sayansi Tanzania Prof. Yunus mgaya pamoja na mabaraza yaliyotangulia kwa
kuendeleza Akademia hiyo iliyoanza rasmi mwaka 2005, kwani wanachama wake
wamekuwa wakifanya kazi mbalimbali za kujitolea na kwamba anatambua mchango wao
katika kukuza na kuendeleza matumizi ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kwa
ajili ya maendeleo ya taifa.
Awali akizungumza katika hafla hiyo Rais huyo
mteule wa TAAS Mgaya amesema Akademia hiyo imejipanga kuongeza wanachama na
kufanya tafiti, kusaidia wanasayansi kuchapisha tafiti hizo katoka majarida
yanayotambulika kimataifa, lakini kubwa zaidi ni kuhuisha matumizi ya Sayansi
na teknolojia katika maendeleo ya uchumi.
Mmoja wa wajumbe la Baraza jipya la Akademia ya Sayansi Tanzania, Prof. Julie Makani akipokea vitendea kazi kutoka kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako. |
Rais wa Baraza la Akademia ya Sayansi Tanzania aliyemaliza muda wake, Prof. Esther Mwaikambo akiongea wakati wa hafla ya uzinduzi wa Baraza jipya uliofanyika jijini Dar es Salaam. |
Mtendaji Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt. Amos Nungu akiongea wakati wa hafla ya uzinduzi wa Baraza jipya uliofanyika jijini Dar es Salaam. |
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza la tatu la Akademia ya Sayansi Tanzania mara baada ya uzinduzi wa Baraza hilo. |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.