Naibu Waziri wa
Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha ameitaka Tume ya Sayansi na
Teknolojia nchini kusimamia wabunifu kupata haki ya umiliki wa bunifu zao.
Naibu Waziri Ole Nasha
ametoa agizo hilo jijini Dar es Salaam, wakati alipotembelea mabanda ya Taasisi
za Elimu zilizo chini ya Wizara zilizoshiriki maonesho ya 43 ya biashara ya
kimataifa maarufu kwa jina la Sabasaba na kukutana na mmoja wa wabunifu
aliyeomba serikali imtambue kwa kuwa amebuni nyenzo ya kufundishia mfumo wa
sayari shuleni.
Alisema ni vizuri
wabunifu wanapoandaa kazi zao zikatambuliwa na kupatiwa haki miliki ya bunifu
au ugunduzi walioufanya lakini pia kuendelea kuwafadhili ili waweze kukuza
bunifu zao.
“Ninyi COSTECH
hakikisheni bunifu mbalimbali nilizoziona hapa sabasaba katika mabanda yetu
haziishii katika maonesho tu, bali zikuzwe na tumieni nafasi hii ya maonesho
kuwakutanisha wabunifu na wafanya biashara kwa ajili ya uzalishaji,” alisema
Naibu Waziri Ole Nasha.
Katika hatua
nyingine Waziri Ole Nasha ameipongeza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
Stadi (VETA) kwa kazi nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya ya kukuza ubunifu na
ujuzi na kuwataka kuendelea kusimamia bunifu mbalimbali za wanafunzi ili ziingie
katika soko na kutatua changamoto mbalimbali za kijamii.
Taasisi zilizo
chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia zilizoshiriki maonesho ya Sabasaba
kwa mwaka 2019 ni pamoja na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE), Chuo
Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
Chuo Kikuu Mzumbe, Tume ya Nguvu za Atomiki nchini (TAEC), Tume ya Sayansi na
Teknolojia (COSTECH), Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) na Chuo Kikuu cha Sayansi
na Teknolojia Mbeya (MUST).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.