Jumatano, 2 Oktoba 2019

WAZIRI NDALICHAKO AZINDUA KIWANDA CHA KUTENGENEZA SAMANI –VETA DODOMA


       •   Ataka VETA kutumia mafundi wao kujenga Vyuo vya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi 
           vya Wilaya

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako ameitaka Mamlaka ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kuhakikisha wanatumia mafundi wao kujenga Vyuo 25 vya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi vya Wilaya nchi nzima.

Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo Jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa kiwanda cha kutengeneza samani cha Ufundi Stadi na Huduma Dodoma ambapo amesema haiwezekani VETA wakawa wanafundisha kujenga lakini wao wakiwa na kazi za ujenzi wanatafuta mafundi kutoka nje.

“Kama VETA mnafundisha kujenga lazima tuone mnafanya kazi kwa vitendo sio mnataka kupaka rangi mnatafuta mafundi wa mtaani nimesema marufuku nataka kuona hizi VETA 25 zinajengwa na ninyi kwa kutumia mafundi wenu vinginevyo nifute mafunzo ya ufundi, “alisema Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akifungua jiwe la msingi la Kiwanda cha VETA Dodoma. Pembeni ni Mbunge wa Dodoma Mjini na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira,  Vijana na Walemavu Mhe. Anthony Mavunde.
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt John pombe Magufuli imeendelea kuviimarisha vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi ili kuhakikisha  vinatoa mafunzo bora na mafunzo ya kisasa ambayo yanaendana na teknolojia ya kisasa na ndio maana inatumia fedha nyingi tena za walipa kodi kuhakikisha inajenga kiwanda cha samani na kutoa wito kwa vijana kujiunga na mafunzo ya useremala katika chuo hicho.

“Nimeambiwa hapa na Mwenyekiti wa Bodi kwamba takwimu za wanafunzi wanaosoma mafunzo ya ufundi seremala bado ziko chini lakini nipende kuwaambia ufundi seremala ni mzuri, kila mtu anahitaji vifaa vya ndani hivyo ni kozi ambayo inalipa natoa wito kwenu vijana kujiunga  na mafunzo haya na niwakaribishe  katika Chuo chetu cha VETA Dodoma ambacho kitakuwa na mafunzo ya kisasa kabisa,”aliongeza Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Kiwanda cha Samani VETA Dodoma.
Waziri Ndalichako ameupongeza uongozi wa VETA kwa kuweza kubuni na kutekeleza mradi wa kiwanda cha kisasa na kuwataka pamoja na kutoa mafunzo kuhakikisha wanakuwa na mpango mzuri wa uzalishaji mali utakaotumia mashine za kisasa zilizofungwa katika kiwanda hicho.

“Baada ya kuzindua kiwanda hiki nimekitembelea na kujionea namna kinavyoweza kufanya kazi kwa ufanisi, kutengeneza bidhaa kwa muda mfupi ni ukweli usiopingika kwamba  kimejengwa vizuri, naamini kitazalisha samani za hali ya juu na kwa bei nafuu na kuondoa dhana kuwa samani nzuri mpaka zitoke nje ya nchi,’aliongeza Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalicho akijaribu moja ya mashine katika kiwanda kipya cha samani cha VETA Dodoma.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Juma Nkamia amesema katika nchi nyingi duniani vyuo vingi vinavyozalisha nguvu kazi ni vyuo vya VETA na kuwataka vijana wanaosoma katika chuo hicho na wale walio nje ya chuo hicho kutoa hamasa kwa watanzania kusoma kwenye vyuo vya VETA ili kupata ujuzi utakaowawezesha kujiajiri.

Nae Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA Peter Maduki amesema kiwanda hicho kitaendelea kuzalisha samani kwa ubora na kulingana na soko na kwamba uwepo wa Kiwanda hicho utasaidia kuongeza mapato yatakayotokana na uzalishaji wa samani zenye ubora na gharama nafuu.

Maduki alimweleza Waziri kuwa katika kufanikisha hilo watahakikisha wanaweka Menejimenti itakayoweza kuendesha kiwanda hicho na kuona malengo yaliyowekwa yanafikiwa huku akimweleza Waziri kuwa changamoto kubwa wanayoipata katika vyuo vya Veta ni kushindwa kupata na wanafunzi wa kutosha wa fani ya useremala.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalicho akitoa maelekezo wakati alipotembelea kiwanda cha samani cha VETA mara baada ya kukizindua rasmi.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA)..Pancras Bujulu alimweleza Waziri Ndalichako kuwa ujenzi wa kiwanda cha utengenezaji samani Dodoma umetekelezwa kwa awamu mbili moja ikiwa ya ujenzi wa jengo na miundombinu yake na awamu ya pili ikiwa ununuzi na ufungaji wa mashine na mitambo kazi zote zikigharimu  zaidi ya shilingi bilioni 3 ambazo ni fedha za ndani.

Hafla ya ufunguzi wa Kiwanda cha kutengeneza samani VETA Dodoma imekwenda sambamba na mahafali ya 36 ya Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma Dodoma.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalicho akielekea kwenye tukio la uzinduzi wa kiwanda cha Samani VETA Dodoma.

Ijumaa, 27 Septemba 2019

OLE NASHA: MSIWAGEUZE WATOTO WA KIKE MITAJI

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha amewataka wazazi kuacha kuwageuza mitaji watoto wao wa kike kwa kuwaozesha mapema na badala yake wawasaidie katika kupata elimu ili baadaye wawe msaada  kwao na taifa kwa ujumla.

Ole Nasha ameyasema hayo leo alipofanya  ziara ya kikazi wilayani Itilima mkoani Simiyu ambapo amekagua  ujenzi wa mabweni mawili ya wasichana katika shule ya sekondari Nkoma yenye uwezo wa kuchukua watoto 160 kwa wakati moja.

"Niwaambie kitu wazazi, kama unataka kumfanya mwanao wa kike mtaji basi mtaji mkubwa ni kumpa elimu na sio kumuozesha," alisema Ole Nasha.
 
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha akiongea na wazazi, walezi na wanafunzi wa shule ya sekondari Nkoma iliyopo wilaya ya Itilima mkoani Simiyu.
Baadhi ya wazazi na walezi wa wanafunzi wa shule ya Nkoma wakimsikiliza Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha (hayupo pichani) alipokuwa akiongea nao shuleni hapo.
Aidha Naibu Waziri Ole Nasha amewataka wazazi kuwekeza kwenye elimu ya watoto wao huku akisisitiza kuwa mtoto wa kike ana haki ya kupata elimu sawa na mtoto wa kiume, ambapo amesema katika jamii nyingi bado hawajawapa kipaumbele cha kupata elimu watoto wa kike.

"Kuna baadhi ya wazazi bado wanashawishi watoto wao kufanya vibaya katika mitihani yao ya mwisho ili wasiendelee na masomo. Nawaomba wazazi msishawishi watoto wa kike na kuwatilia vikwazo vya kukatisha masomo ili muwaozeshe. Mtoto wa kike ana nafasi ya kupata elimu sawa na mtoto wa kiume," alisema Naibu Waziri Ole Nasha.
Mwalimu Mkuu wa shule ya sekondari Nkoma, Sarah Matonya akisoma taarifa ya ujenzi wa mabweni mawili mapya mbele ya Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha (hayupo pichani).
Ole Nasha aliongeza kuwa serikali na wadau wa elimu wanatakiwa waendelee kutoa hamasa ya elimu kwa jamii, wanafunzi na wazazi ili miundombinu ya elimu inayojengwa iweze kutumika kwa faida ya wananchi wote katika kuboresha na kukuza elimu.

Naibu Waziri Ole Nasha amepongeza  usimamizi wa fedha za miradi ya elimu katika wilaya hiyo kutokana na kutokuwepo kwa malalamiko yoyote ya matumizi mabaya ya fedha hizo.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha akizindua mabweni katika shule ya sekondari Nkoma ya wilayani Itilima mkoani Simiyu.
Awali, akisoma taarifa ya ujenzi wa mabweni hayo, Mwalimu Mkuu wa shule ya sekondari Nkoma, Sara Matonya alisema mabweni hayo yamegharimu zaidi ya shilingi milioni 300 na kwamba kukamilika kwa mradi huo wa ujenzi wa mabweni kumechochea hamasa ya wanafunzi wa kike kusoma kwa bidii kutokana na kuboreshwa kwa mazingira ya kujifunzia.


"Mabweni haya mawili yana uwezo wa kubeba wanafunzi 80 kila moja na yamesaidia wanafunzi kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu wa zaidi ya kilometa 10 kufika shuleni. Wanafunzi wa kike pia wameepukana na vishawishi na mimba zilizokuwa zikiwasababishia kukatisha masomo," alisema Mwalimu Matonya.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha (katikati) akikagua moja ya mabweni mapya katika shule ya sekondari Nkoma iliyopo wilayani Itilima mkoani Simiyu.  Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Benson Kilangi na kulia ni Mbunge wa Itilima, Njalu Silanga.
Kwa upande wao wazazi na wanafunzi wameipongeza serikali kwa kutoa elimu bila malipo pamoja na kuwajengea mabweni, hali iliyopelekea kuongezeka kwa mahudhurio ya wanafunzi darasani, ufaulu na mwitikio wa elimu katika jamii.

"Tunaipongeza serikali kwa ujenzi wa mabweni haya ambayo yametupunguzia changamoto ya kutembea umbali mrefu na pia tumekuwa na muda mwingi wa kujifunza na kujisomea, na hivyo kutuwezesha kufanya vizuri katika masomo yetu," alisema Myano Ngusa, mwanafunzi wa shule ya sekondari Nkoma.
Mojawapo ya chumba katika bweni jipya la shule ya sekondari Nkoma ya wilayani Itilima mkoani Simiyu.
Katika ziara hiyo Ole Nasha pia alikagua ofisi ya Uthibiti Ubora wilaya ya Itilima ambazo ujenzi wake umekamilika pamoja na majengo ya VETA yanayoendelea kujengwa katika kijiji cha Kanadi wilayani humo.
Muonekano wa nje wa moja kati ya mabweni yaliyojengwa katika shule ya sekondari Nkoma ya Itilima mkoani Simiyu lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 kwa wakati mmoja.
Muonekano wa nje wa jengo la ofisi za Uthibiti Ubora wilaya ya Itilima mkoani Simiyu.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha akikagua ofisi ya Uthibiti Ubora wilaya ya Itilima mkoani Simiyu.
Muonekano wa ndani wa chumba kimojawapo katika majengo ya VETA, Itilima mkoani Simiyu.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha (mwenye skafu) akisikiliza maelezo kuhusu VETA kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Benson Kilangi.
Muonekano wa nje wa jengo la VETA la wilayani Itilima mkoani Simiyu.

Ijumaa, 20 Septemba 2019

WIZARA YA ELIMU KUWAKUTANISHA WADAU WA ELIMU ILI KUJADILI MASUALA YA ELIMU NCHINI


Waziri wa Eimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amefungua na kushiriki Mdahalo juu sekta ya Elimu uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Mjadala huo ulioandaliwa na Mwanachi Communications Ltd., (MCL) kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ulihusisha majadiliano juu ya uwezeshaji vijana katika kukuza maarifa na ujuzi mahususi.

Akifungua mdahalo huo Waziri Ndalichako amesema Serikali ya awamu ya Tano imewekeza kiasi kikubwa cha rasilimali ili kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji katika ngazi zote za elimu ili vijana wanaosoma wapate mafunzo katika mazingira yatakayowawezesha kuwa mahiri katika fani wanazosomea.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa ufunguzi wa mjadala juu ya uwezeshaji vijana katika kukuza maarifa ulioandaliwa na Mwananchi Communications Ltd., kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia jijini Dar es Salaam.
Prof. Ndalichako ameongeza kuwa katika ngazi ya elimu ya ufundi na elimu ya juu serikali inaboresha maabara na karakana na kuweka vifaa vya kisasa ili mafunzo kwa vitendo yafanyike kwa tija na kulingana na mazingira ya sasa. Aidha ametolea mfano wa maktaba ya kisasa inayojengwa katika Chuo Kikuu cha Teknolojia Mbeya (MUST) itakayokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 2,500 kwa mara moja ambayo inagharimu fedha za ndani zaidi ya shilingi bilioni 11.

Ndalichako amewashukuru MCL kwa kufungua njia ya kuwa na mijadala ya wazi juu ya maendeleo ya elimu na kuahidi kuandaa mjadala mwingine wa Elimu utakaohusisha wadau.  Pia amepongeza washiriki kwa kutoa maoni ambayo yana tija katika kuboresha elimu, huku akisisitiza kuwa elimu yetu inaandaa vijana mahiri ambao wanashiriki kujenga taifa.

"Humu ndani tumesikia fikra mahiri zinazotokana na vijana ambao wanasoma hapa hapa nchini na mitaala ni hii hii, hivyo tujiamini kuwa elimu yetu ni bora na inawezesha vijana kuwa mahiri katika fani mbalimbali," alisema Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako akiwa na baadhi ya wadau wa Elimu wakifuatilia mjadala juu ya uwezeshaji vijana katika kukuza maarifa uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Ndalichako amesisitiza juu ya uboreshaji elimu ya ufundi ambapo amesema katika mwaka huu wa fedha vyuo vipya vya VETA 25 vinajengwa kwa shilingi bilioni 40.

Ndalichako pia amesema Serikali kupitia VETA inaendelea na programu ya kutambua na kurasimisha ujuzi kwa vijana ambapo amesema mwaka huu zaidi ya vijana 10,000 watapatiwa mafunzo kutokana na ujuzi walio nao na kupatiwa vyeti vya kurasimisha ujuzi huo. Amesema lengo la kurasimisha ni kuwatambua, kuwapa stadi na kuwaongezea ujuzi vijana walioko katika maeneo mbalimbali ambao wamekuwa wakifanya kazi za ujuzi bila vyeti.

Awali, akizungumza katika mjadala huo Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Francis Nanai amemshukuru Waziri Ndalichako na Viongozi wa wizara kwa kukubali kushiriki mjadala na kupokea maoni.  Amesema wao kama sekta binafsi wanalo jukumu la kushirikiana na serikali katika kusukuma mbele maendeleo kulingana na eneo lao la biashara.

Akiongea katika Mjadala huo, Prof. Lughano Kusiluka ambaye ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe amesema Vyuo Vikuu vinaandaa mitaala kulingana na uhitaji wa soko na mahitaji ya wakati.  Amewaasa vijana pia kuona umuhimu wa kutumia elimu wanayopata na vipaji walivyo navyo kubuni biashara na kujiajiri badala ya kusubiri ajira.

Kusiluka amesema Vyuo vikuu vina programu za kukuza bunifu za wanafunzi na kuziendeleza kuwa biashara kupitia Vituo Atamizi na kambi za ujasiriamali.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akibadilishana mawazo na Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Ltd., Francis Nanai wakati wa  mjadala juu ya uwezeshaji vijana katika kukuza maarifa uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Naye mmoja wa washiriki, Abel Nyengo ameiomba Serikali kuhakikisha kila kijana aliyeko katika chuo anapata nafasi ya mafunzo kwa vitendo.

"Nishauri serikali kuwa mafunzo kwa vitendo iwe ni lazima na ipewe umuhimu mkubwa katika kutahini wanafunzi badala ya kutegemea mitihani,” alisema Nyengo.

Wananchi na wadau mbalimbali wametoa maoni mengi juu ya mada hiyo wakihusisha mitaala, utoaji elimu na ujuzi.