Jumapili, 10 Novemba 2019

WAZIRI NDALICHAKO ATEMBELEA SHULE YA WASICHANA MISUNGWI

WAZIRI NDALICHAKO AZINDUA OFISI ZA UTHIBITI UBORA WA SULE WA WILAYA ZA MISUNGWI NA SHINYANGA

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako leo Novemba 9, 2019 amefungua majengo ya ofisi mpya za Uthibiti Ubora wa Shule za Halmashauri ya  Wilaya ya Misungwi na Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.

Akizungumza baada ya ufunguzi wa ofisi hizo Waziri Ndalichako amewataka wathibiti Ubora wa Wilaya kufanya kazi kwa bidii na weledi na waone kuwa uwepo wa ofisi hizo uwe chachu ya kuendelea kutoa taarifa za ukaguzi wa shule zenye ubora na kwa wakati. Ndalichako amewataka kuhakikisha kuwa changamoto zinazoainishwa katika kaguzi zao zinafanyiwa kazi ili kuinua ubora wa elimu hususan katika taaluma  na sekta ya elimu  kwa ujumla katika wilaya hizo.

"Tumieni ofisi hizi kuwa chachu ya kuwawezesha kufanya kazi kwa ufanisi na kutoa taarifa za changamoto zinazozikabili shule pamoja na sekta nzima ya elimu ili ziweze kufanyiwa kazi kwa haraka," amesema Profesa Ndalichako.

Prof. Ndalichako amesema serikali itahakikisha changamoto zote zinazowakabili wathibiti ubora wa shule nchini zinafanyiwa kazi kwa dhati ili  kuzipunguza ama kuzimaliza kabisa  ikiwemo ukosefu wa ofisi na vitendea kazi.

Akizungumzia uboreshaji na ujenzi wa miundombinu ya sekta ya elimu  unaoendelea nchini,  Profesa Ndalichako amesema suala hilo ni endelevu na litakuwa likifanyiwa kazi muda wote ili kuwezesha utoaji wa elimu bora kwa watoto wa Kitanzania.

Aidha, Waziri Ndalichako amewataka wathibiti ubora wa shule kwa kushirikiana na Maafisa Elimu kufanya tathimini za kina kila mara ili kubaini sababu halisi za mdondoko wa wanafunzi wote wa kike na kiume.

"Tumeona hapa Misungwi takwimu zinaonyesha mdondoko mkubwa zaidi upo kwa upande wa watoto, hivyo fanyeni tathimini ili tujue sababu na kuacha kuegemea upande mmoja wa mtoti wa kike na kwamba sababu ni mimba" amesema Profesa Ndalichako

Mkuu wa wilaya ya Misungwi, Juma Sweda ameishukuru serikali kwa kuhakikisha wathibiti ubora wa shule wanapata ofisi za kisasa na vitendea kazi na kuhaidi  kuwa wilaya ya Misungwi itaendelea kusimamia ubora wa elimu na kuongeza ufaulu katika ngazi zote.

"Sisi tutaendelea kusimamia utoaji wa elimu bora kwa watoto wote wa hapa Misungwi pamoja na kupunguza  mdondoko wa wanafunzi kwa kuanzisha mpango wa kutoa chakula shuleni" amesitiza Mkuu wa Wilaya.

Naye Mthibiti Mkuu wa Wilaya hiyo, Faustine Sahala ameishukuru serikali kwa kuona changamoto zilizokuwa zikiwakabili za ukosefu ofisi ambapo walipatiwa zaidi ya shilingi milioni 152 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi hizo.
Sahala amesema ujenzi wa ofisi hiyo umekamilika kwa asilimia 100 pamoja na ununuzi wa vitendea kazi ikiwemo mashine  ya kurudufu (photocopy), ufungaji  mtandao wa internet, uwekaji samani,  camera za ulinzi (CCTV) na ujenzi wa vyoo vya nje.

Katika Mpango huu Serikali inajenga ofisi 100 za Wadhibiti Ubora wa shule katika Halmashauri 100  kwa shilingi bilioni 15.2






Jumatano, 6 Novemba 2019

WAZIRI NDALICHAKO AKUTANA NA MKUU MPYA WA ELIMU KUTOKA UNICEF



Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako leo Novemba 6, 2019 amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Elimu Tanzania kutoka Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) Tanzania, Dkt. Daniel Baheta.

Dkt. Baheta amefika katika ofisi za Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia zilizopo Jijini Dodoma kwa lengo la kujitambulisha  baada ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo ambapo amemweleza waziri kuwa UNICEF inatekeleza vipaumbele vitatu katika sekta ya elimu.

Mkuu huyo amevitaja vipambele vya Kimataifa vya UNICEF kuwa ni kuwa ni ubora katika utoaji elimu na ujifunzaji, elimu kwa  vijana, ajira  na kutatua changamoto ya mdondoko wa wanafunzi katika shule.

Waziri Nadlichako amesema angependa kuona UNICEF ikishirikiana zaidi na Serikali  katika kuimarisha mafunzo ya stadi za maisha ambazo zitawawezesha wanafunzi wa kike kukwepa vishawishi vinavyosababisha mdondoko shuleni na ukuzaji wa ushirikishwaji jamii katika kusimamia ubora wa elimu na wanafunzi.

Katika mazungumzo yao wamekubaliana kutekeleza programu   ambazo ni pamoja na kuanzisha mfumo wa kidigitali wa kusimamia mahudhurio ya wanafunzi na kuwezesha mawasiliano kati ya Taasisi za elimu  na wazazi.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako awakiangalia kishikwambi pamoja na wageni kutoka UNICEF

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akizungumza na Mkuu wa Elimu kutoka UNICEF Tanzania Dkt. Daniel Bahate (Mwenye suti ya bluu) aliyefika ofisi kwake leo jijini Dodoma kwa lengo la kujitambulisha. 
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akiwa katika picha ya pamoja na Dkt Daniel Bahate (kushoto) Mkuu wa Elimu kutoka UNICEF Tanzania.

MIAKA 4 YA SERIKALI YA AWAMU YA TANO. MWANAFUNZI AELEZA ALIVYOFAIDIKA NA...

Jumatatu, 4 Novemba 2019

WANAFUNZI MWAKA WA KWANZA WALIOPATA MIKOPO WAFIKIA 46,838

Jumapili, Novemba 3, 2019

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza orodha ya awamu ya tatu yenye jumla ya wanafunzi wa mwaka kwanza 4,785 waliopata mikopo yenye thamani ya TZS 14.3 bilioni na hivyo kufanya jumla ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliopata mikopo yenye thamani ya TZS 162.86 bilioni hadi sasa kufikia 46,838.

Orodha ya kwanza ilitolewa Oktoba 17 mwaka huu na ilikuwa na wanafunzi wa mwaka wa kwanza 30,675 waliopata mikopo yennye thamani ya TZS 113.5 bilioni. Orodha ya pili ilitolewa Oktoba 26 mwaka huu ikiwa na wanafunzi wa mwaka wa kwanza 11,378 waliopangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 35.06 bilioni.

Taarifa iliyotolewa leo (Jumapili, Novemba 3, 2019) na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru imeeleza kuwa wanafunzi waliopata mikopo katika awamu ya tatu wanaweza kupata taarifa zao kupitia akaunti walizotumia kuomba mkopo maarufu kama SIPA – Student’s Individual Permanent Account.

Pamoja na SIPA, Badru amesema majina yote ya waombaji waliofanikiwa kupangiwa mikopo katika awamu hii ya pili yanapatikana katika mtandao wa HESLB wa uombaji mkopo (https://olas.heslb.go.tz) na tovuti ya Bodi (www.heslb.go.tz).

“Awamu hii ya tatu inajumuisha wanafunzi wahitaji ambao wamekamilisha taratibu za udahili pamoja na kukamilisha marekebisho ya maombi yao yaliyokuwa na dosari … tutaendelea kufanyia kazi maombi yanayorekebishwa na wale wenye sifa watapangiwa,” amesema Badru. 

Kuhusu taratibu za malipo kwa wanafunzi, Badru amesema fedha za wanafunzi waliopata mikopo zimeshapelekwa vyuoni na vyuo vimeleekezwa kuhakikisha fedha zinawafikia wanafunzi walengwa mara wanapofika na kukamilisha taratibu za usajili.

“Serikali imeshatupatia TZS 125 bilioni ambazo tulikuwa tunazihitaji kwa ajili ya malipo ya robo ya kwanza ya Oktoba hadi Disemba mwaka huu na sisi tumeshatuma vyuoni na maafisa wetu wameanza kwenda vyuoni ili kukutana na wanafunzi na kutatua changamoto iwapo zitajitokeza,” amesema Badru.

Badru amesema katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imetenga TZS 450 bilioni kwa ajili ya jumla ya wanafunzi 128,285. Kati yao, wanafunzi 83,285 ni wenye mikopo wanaoendelea na masomo ya mwaka wa pili, tatu na kuendelea.

Bodi inapenda kuwasihi waombaji wa mikopo kuwa watulivu wakati mchakato wa upangaji wa mikopo kwa wanafunzi wenye sifa kwa awamu inayofuata ukiendelea.

Mwisho.