Alhamisi, 12 Desemba 2019

OLE NASHA: WAKUU WA SHULE HIMIZENI WANAFUNZI WASHIRIKI MASHINDANO YA UANDISHI WA INSHA

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha amewataka Wakuu wa Shule zote za sekondari nchini kuwahimiza wanafunzi wao kushiriki katika mashindano ya uandishi wa insha za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Ole Nasha amesema mashindano hayo ni sehemu ya mkakati wa kujenga uelewa kwa wanafunzi juu ya kazi na mipango ya maendeleo ya Jumuiya hizo.

Ole Nasha ameyasema hayo leo jijini Dodoma katika hafla ya utoaji zawadi kwa washindi wa shindano la uandishi wa insha za SADC na EAC kwa mwaka 2019 na kuongeza kuwa mashindano haya yana faida kubwa zaidi ya kupata zawadi kwani washindi wanaweza kuyatumia kujiongezea wasifu wao siku za mbeleni na hivyo kuwaongezea sifa za kupata ajira.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha akiongea na washiriki (hawapo pichani) waliohudhuria hafla ya utoaji zawadi kwa washindi wa shindano la uandishi wa insha za SADC na EAC, 2019 iliyofanyika jijini Dodoma.
"Niwaambie wanafunzi, kushinda sio suala la kupata zawadi tu bali kunakujengea wasifu ambao huko mbeleni utakusaidia unapoomba ajira unakuwa na wasifu wa ziada utakaokufanya upate ajira kirahisi," alisisitiza Ole Nasha.

Katika hatua nyingine Waziri Ole Nasha ameonesha  kushangazwa na wanaobeza kiwango cha elimu itolewayo nchini ambapo amesema ushindi unaopatikana kutoka kwa wanafunzi wa kitanzania unaonesha dhahiri kuwa elimu ya Tanzania ni bora.
Baadhi ya wanafunzi, walimu na wazazi walioshiriki katika hafla ya utoaji zawadi kwa washindi wa shindano la uandishi wa insha za SADC na EAC mwaka 2019 wakisikiliza hotuba ya mgeni rasmi ambaye ni Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha (hayupo pichani).
Mwanafunzi Ruvina D. Warimba kutoka shule ya sekondari Morogoro, ambaye pia ndio mshindi wa tatu wa shindano la uandishi wa insha za SADC Kanda akitunukiwa cheti na Mwakilishi toka SADC, Agnes Kayola. Katikati ni Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha na kulia ni Kaimu Kamishna wa Elimu, Augusta Lupokela.
Mratibu wa mashindano ya Uandishi wa Insha, Sylvia Chinguwile akiongea katika hafla ya utoaji zawadi kwa washindi wa shindano la uandishi wa insha za SADC na EAC mwaka 2019.
"Kuna maneno huko nje kuwa elimu yetu haina kiwango, kama ni kweli inawezekanaje mwanafunzi wetu anaibuka mshindi wa tatu katika mashindano yanayoshirikisha nchi zaidi ya 15," amehoji Ole Nasha.

Awali, akisoma risala katika hafla hiyo, Mratibu wa mashindano hayo, Sylvia Chinguwile amesema mashindano hayo yamekuwa chachu kwa vijana kufanya utafiti, kujifunza na kufahamu vizuri mchakato wa uimarishaji mahusiano kwa nchi wanachama wa SADC na EAC .

Akielezea zaidi kuhusu mashindano hayo, Chinguwile amesema mchakato wake huanza baada ya kikao cha wakuu wa nchi wanachama ambao hukubaliana mada zitakazoshindaniwa. Baada ya hapo kila nchi hutakiwa kutangaza na kubainisha vigezo vya ushiriki na kwamba insha za wanafunzi huwasilishwa wizarani baada ya kuteuliwa insha bora katika ngazi ya shule na kusahihishwa na jopo la wataalamu.

Chinguwile amewataja washindi wa mashindano hayo na shule wanazotoka kuwa ni Vanessa Lema (Longido), Thomas Kalisti (Kibasila), Monica Nyamhanga (Heritage), Dennis Mmuni (St. Maximillian), Hance Mwang'onda (Mbagala), Julieth Mpuya (Kilangalanga), Grant Mkonyi (Tanga Tech), Mandela Abel (Kibaha), Rebecca Thadayo (Loyola), Sharifa Hamadi (Benbella), Cynthia Masuka (Longido) na Ruvina Warimba (Morogoro) ambaye alishika nafasi ya tatu katika shindano la kanda la SADC.
Hafla hiyo pia imehudhuriwa na mwakilishi kutoka EAC, Dkt. James Jowi, mwakilishi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Eliab Chodota na Mwakilishi kutoka SADC, Agnes Kayola ambao wamewapongeza wanafunzi hao kwa ushindi na kuwataka wanafunzi wengine nchini kushiriki mashindano hayo.

Washindi hao kutoka shule mbalimbali za serikali na binafsi wamezawadiwa fedha taslimu za kitanzania na dola za kimarekani pamoja na kutunukiwa vyeti. Fedha hizo zimetolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambapo wametoa kiasi cha Sh. 300,000 kwa washindi wote huku SADC na EAC wakitoa kati ya dola 500 hadi 50 kulingana na kiwango cha ushindi.
Kaimu Kamishna wa Elimu, Augusta Lupokela akiongea katika hafla ya utoaji zawadi kwa washindi wa shindano la uandishi wa Insha za SADC na EAC 2019 iliyofanyika jijini Dodoma.
Mwakilishi kutoka EAC, Dkt. James Otieno Jowi akiongea na washiriki katika hafla ya utoaji zawadi kwa washindi wa uandishi wa insha za SADC na EAC, 2019 iliyofanyika jijini Dodoma.

Mwanafunzi Dennis Mmuni akikabidhiwa cheti na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha katika  hafla ya utoaji zawadi kwa washindi wa shindano la uandishi wa insha za SADC na EAC, 2019 iliyofanyika jijini Dodoma.

Ijumaa, 29 Novemba 2019

NDALICHAKO AZINDUA CHUO CHA VETA NDOLAGE WILAYANI MULEBA - 380 KUDAHILIWA JANUARI 2020

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amezindua chuo kipya cha VETA Ndolage kilichopo Kamachumu Wilaya ya Muleba mkoani Kagera kilichojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 281.

Ujenzi wa Chuo hicho ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya kushirikiana na jamii kufikisha Elimu ya Ufundi karibu na Wananchi pamoja na kujenga Vyuo vya VETA katika kila Wilaya nchini ifikapo mwaka 2020, ambapo Wizara imetenga zaidi ya Sh. bilioni 40 katika mwaka huu wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Vyuo vya VETA katika Wilaya 25 nchini.

Ujenzi wa Chuo cha Ndolage ulianzishwa na Wananchi kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Muleba  Kaskazini, Charles Mwijage ambapo wananchi walitoa kiwanja na kuanza ujenzi wa madarasa kwa kutumia michango yao.

Akizungumza katika hafla hiyo Profesa Ndalichako amewataka VETA  kuhakikisha wanajenga majengo yote yanayohitajika  katika Chuo hicho kwa kutumia mapato ya ndani ya VETA.

"Nimezindua Chuo hiki lakini sijaridhishwa na majengo, ni machache na hayana hadhi kwani Wizara imetoa hela kulingana na mahitaji  yenu, inakuwaje bado kuna changamoto za majengo? Natoa miezi sita mkamilishe kwa fedha zenu," alisisitiza Ndalichako.

Wakati huo huo Ndalichako amewashukuru Wananchi wa Ndolage na Mbunge wa Jimbo hilo  kwa  hatua ya kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha watoto na Vijana katika eneo hilo wanapata Elimu kwa kujitolea ardhi bure kwa ajili ya ujenzi huo na kuchangia fedha za vifaa.

Aidha, Mkuu wa Mkoa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti, ameishukuru Wizara ya Elimu kwa ujenzi wa Chuo hicho na ameahidi kuhamasisha Wananchi kuandikisha Vijana wao kujiunga na Chuo hicho.

Akitoa salamu za VETA, Mwenyekiti wa Bodi ya VETA, Peter Maduki amesema Chuo hicho kitadahili wanafunzi 80 wa kozi za muda mrefu na wanafunzi 300 wa kozi fupifupi ambao wanatarajiwa kuanza mafunzo Januari mwaka 2020.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mbunge wa Jimbo hilo la Muleba kaskazini, Charles Mwijage ameishukuru Serikali kwa kujenga Chuo  hicho huku akiushauri uongozi wa VETA kuongeza mafunzo ya fani ya usindikaji mazao  kwani wananchi wa eneo hilo wamejikita katika kilimo.

Mafunzo mengine yatakayotolewa katika Chuo hicho ni ya fani za  Uashi, Ushonaji, Uhazili, Urembo na Uungaji wa Vyuma.

TANZANIA CHINA KUJENGA CHUO KIKUBWA CHA VETA MKOANI KAGERA

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amezindua ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Kagera na kusema kuwa ujenzi wa chuo hicho ni muendelezo wa jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano kuhakikisha kunakuwa na Vyuo vya ufundi stadi vya Mikoa na Wilaya.

Akizindua ujenzi wa chuo hicho mkoani Kagera Waziri Ndalichako amesema  chuo hicho  kinajengwa  na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kutokana na uhusiano mzuri wa muda mrefu tulio nao  na kwamba pindi ujenzi  utakapokamilika vijana wengi wa kitanzania watapata fursa ya kusoma katika chuo hicho na kupata ujuzi katika fani mbalimbali zitakazo fundishwa.

"Kama nilivyosema Tanzania na China ni marafiki na rafiki yako anaangalia mahitaji yako, waswahili husema akufaaye kwa dhiki ndio rafiki wa kweli. China imeona Tanzania inajenga uchumi wa Viwanda ikiwa ni azma ya serikali ya awamu ya Tano  nao wakaamua watuunge mkono katika ujenzi wa Chuo cha Ufundi stadi ili kuandaa vijana wenye ujuzi watakaofanya kazi katika viwanda.

"Nikuombe Balozi  tufikishie shukrani zetu za dhati kwa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya watu wa China kwa msaada huu mkubwa na wa kihistoria ,"aliongeza Waziri Ndalichako

Waziri Ndalichako amesema ujio wa mradi huo utaongeza ajira kwa vijana wa kitanzania kwa kuwa wazawa 400 wataajiriwa katika mradi huo ikiwa ni pamoja na kupata  ujuzi  kulingana na kazi watakazokuwa wakizitekeleza.

"Vijana watakaofanya kazi eneo la mradi pamoja na kufanya kazi  watapata na mafunzo, kwa hiyo ujuzi wao wa kiufundi utaimarishwa kupitia kazi ambazo watakuwa wakifanya katika mradi,"alisema waziri Ndalichako.

Katika hatua nyingine Waziri Ndalichako ameitaka Mamlaka ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA kupitia upya fani zilizopangwa kutolewa katika chuo hicho ili ziendane na Mazingira halisi ya kiuchumi kwa wakazi wa eneo hilo.

"Nimepitia fani ambazo zimeanishwa kutolewa katika chuo hiki pindi kitakapokamilika, nikiangalia eneo ambalo chuo kinajengwa ni eneo la ziwa na watu wa Kagera au wazazi wa hapa ni wavuvi lakini sijaona kozi ya uvuvi sasa tunawaletea mambo ya uchomeleaji, ufundi bomba, useremala, upakaji rangi kwenye bahari, nilitegemea kuwe na fani ya uvuvi pia
 tuweke fani zinazoendana na mazingira," alisema Waziri Ndalichako

Kwa upande wake Balozi wa China nchini Tanzania Balozi WANG Ke amesema Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania amezingatia maboresho ya sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kuwaongoza watanzania kuelekea dira ya  maendeleo 2025 hivyo China iko tayari kuchangia maendeleo katika sekta ya elimu ili kufikia malengo ya elimu ambayo serikali ya tanzania imejiwekea.

Nae Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Generali Marco Gaguti  amewataka wanakagera hasa vijana kushiriki vizuri katika kazi za ujenzi zitakazofanyika katika mradi huo  ili kupata ujuzi wa ufundi ambao utawasaidia kushirikia katika kazi za ujenzi zitakazojitokeza katika Mkoa wa Kagera mara baada ya mradi kukamilika.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi   VETA Dkt. Pancras Bujulu amesema Chuo hicho kinajengwa katika eneo lililotolewa na wananchi wa kijiji cha Burugo wilayani Bukoba na lina ukubwa wa hekta 40. 5 sawa na hekari 100.

Dkt. Bujulu amesema Chuo hicho pindi kitakapokamilika kitatoa fani za useremala, uchomeleaji, upakaji rangi, ufundi bomba na kitachukua wanafunzi 800 wa kozi ndefu na 2000 wa kozi fupi

Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi cha Mkoa wa Kagera kinajengwa kwa msaada wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China  kwa gharama za fedha za kitanzania sh bilioni 19.4  ambapo ujenzi wake utachukua miezi 18

Gharama hizo zinajumuisha usanifu, upembuzi yakinifu na ujenzi mpaka ukamilike.

Jumapili, 24 Novemba 2019

VYUO BINAFSI VINA MCHANGO MKUBWA KWENYE UTOAJI WA ELIMU YA JUU: PROF. NDALICHAKO

Serikali imesema inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na vyuo binafsi katika kuleta maendeleo ya elimu ya juu kikiwemo Chuo Kikuu cha St. John’s cha hapa nchini.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa Jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako wakati wa mahafali ya kumi ya Chuo Kikuu cha St. John’s ambapo amesema kuwepo kwa vyuo binafsi hapa nchini kunasaidia na kuwezesha nchi yetu kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaopata mafunzo ya elimu ya juu.

Waziri Ndalichako amesema Chuo hicho kimekuwa kikitoa mchango mkubwa katika utayarishaji wa wataalamu katika fani mbalimbali ikiwemo fani ya ufamasia, uuguzi, ualimu wa Sayansi na Sanaa, kilimo, usimamizi wa fedha, uendeshaji katika utawala, masoko, uhasibu na wataalamu wa maabara.

“Nimeelezwa kuwa tangu chuo hichi kuanza mwaka 2007 hadi hivi sasa kimeweza kutoa wahitimu wasiopuungua elfu kumi na mbili, huu ni mchango mkubwa kwa Taifa letu, hongereni sana,” alisema Prof Ndalichako.


Amewapongeza wahadhiri wa Chuo hicho kwa kazi nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya ya kuwafundisha vijana ambapo amewataka kuendelea kuwaandaa vema wahitimu ili wakawe chachu na mfano wa kuigwa katika jamii wanazokwenda kuishi baada ya kuhitimu masomo yao.

“Nimefurahi kusikia kuwa Chuo hiki pamoja na masuala ya kitaaluma kinatilia mkazo suala la maadili, kinasisitiza umuhimu wa wanachuo kumuheshimu Mungu, kuwa waadilifu, kufanya kazi kwa bidii na kuwa tayari kuhudumia wengine,” aliongeza Prof. Ndalichako.


Katika hatua nyingine Waziri Ndalichako amesema suala la utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya juu ni kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Tano ili kuhakikisha wanafunzi wote wanaostahili kupata mikopo wanapata na kuwawezesha kusoma bila changamoto yoyote.

“Nimefarijika kusikia kwamba idadi ya wanafunzi wanaopata mikopo katika chuo cha St. John’s imeongezeka na kwamba mikopo hiyo inatoka kwa wakati, na hii niwaambie ukweli ni mpango wa Mhe. Rais. Mtakumbuka wakati akifanya kampeni aliahidi na kueleza namna alivyokuwa akisononeka kuona watoto wa kitanzania, wanafunzi wa elimu ya Juu walivyokuwa wakihangaika kupata fedha za mikopo, hivyo jambo la kwanza aliliolifanya alipoingia madarakani ni kuongeza kiasi cha fedha kinachotolewa kwa ajili ya mikopo kutoka bilioni 341 mwaka 2014/15 na sasa fedha zilizotengwa  kwa mwaka 2019/20 ni sh bilioni 450,” alisema Waziri Ndalichako.




Waziri Ndalichako aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inatoa fedha za mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa wakati akitolea mfano wanafunzi  ambao wameanza masomo mwanzoni mwa mwezi Novemba 2019 Serikali imetoa fedha zao tangu mwezi Septemba.

“Hadi kufikia Oktoba 15, 2019 Serikali ilikuwa imekwishatoa jumla ya sh bilioni 185 sawa na asilimia 41 ya fedha ambazo zimepangwa kwa ajili ya wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa mwaka 2019/20,” alisema Waziri Ndalichako.

Waziri Ndalichako ametumia fursa hiyo kuviagiza vyuo vyote nchini ambavyo kwa namna moja au nyingine bado havijatoa fedha kwa wanafunzi kutoa fedha hizo kwani Serikali inatoa fedha kwa ajili ya wanafunzi na sio kwa ajili ya vyuo.

Aidha Waziri Ndalichako amewataka wanafunzi wanaohitimu masomo ya elimu ya juu kuwa mabalozi wazuri wa vyuo walivyosoma na Taifa kwa ujumla huku akiwataka kuwa wazalendo na watu ambao wanaweka maslahi ya taifa mbele na kupinga vitendo vya aina yoyote vyenye lengo la kuvuruga amani na mshikamano wa Taifa letu.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha St.John’s, Prof. Yohana Msanjila amesema wanafunzi wanaohitimu katika Chuo hicho kwa mwaka 2019 wako 1,730 huku akiipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuongeza idadi ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu wanaopata mikopo ikiwa ni pamoja na kuwa na usimamizi mzuri wa utoaji mikopo ya elimu ya juu.

“Fedha za wanafunzi na ada zao zinatolewa mapema tofauti na miaka ya nyuma. Nakuomba mgeni rasmi Mhe. Prof. Joyce Ndalichako utufikishie pongezi zetu kwa Mhe. Rais kwamba siku hizi fedha za mikopo na ada za wanafunzi zinafika kwa wakati na hii imesaidia kudumisha utulivu chuoni. Hongera kwa Serikali yetu, hongera Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya juu,” alisema Prof Msanjila.

Mahafali ya kumi ya Chuo Kikuu cha St. John’s kwa mwaka 2019 yalikuwa na Kauli mbiu isemayo “Udijitalishaji wa Elimu ya Juu kwa Vyuo binafsi: Kiungo Bora kwa Uchumi wa Viwanda.”