Jumatatu, 21 Julai 2014

Kuweni Wabunifu Zaidi - Prof. Mchome

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome amewataka Watumishi wa Wizara hiyo kuwa wabunifu zaidi na kuhakikisha kuwa wanachokibuni kiwe kinatekelezwa na kuchukua hatua kwa wasiotekeleza maelekezo ya kisera pamoja na kuwazawadia wanaotekeleza kwa ufanisi maelekezo yanayotolewa.

“Watumishi wa Wizara hii tunatakiwa tujiulize tunafanya ubunifu gani ili kuhakisha wahitimu katika ngazi mbalimbali wanapata maarifa yanayotakiwa na wanaoweza kusaidia nchi katika kuleta maendeleo katika nyanja mbalimbali,” alisema Profesa Mchome.

Profesa Mchome alikuwa akizungumza na Watumishi wa  Makao Makuu na Taasisi zilizoko chini ya Wizara hiyo katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (Julius Nyerere International Convention Centre), Ijumaa 18 Julai, 2014 ikiwa ni utaratibu aliojiwekea wa kukutana na watumishi hao na kujadiliana namna bora zaidi ya kuboresha utendaji kazi katika wizara.

Aidha, Profesa Mchome alizungumzia umuhimu wa kuboresha Muundo wa Wizara hiyo ili kuwezesha namna bora ya kutekeleza majukumu yake baada ya ugatuaji wa uendeshaji na usimamizi wa shule za Sekondari kwenda kwenye Halmashauri chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI na kwa kufuata Hati Idhini iliyounda Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliyotolewa na Mheshimiwa Rais, Desemba 2010.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.