Serikali
ya Tanzania na Benki ya Dunia wamesaini makubaliano ya mkopo wa Shilingi
bilioni 203 za Kitanzania (Dola za Marekani milioni 122) kwa ajili ya kusaidia, kukuza na kuendeleza Mpango wa
Matokeo Makubwa Sasa (BRN) katika sekta ya Elimu wenye lengo la kuimarisha na
kuboresha elimu ya msingi na sekondari.
Makubaliano
hayo yalitiwa saini na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Dkt. Servacius
Likwelile kwa niaba ya Serikali na Benki
ya Dunia iliwakilishwa na Mkurungezi Mkazi wa Benki hiyo nchini, Philippe
Dongie. Makubaliano hayo yamefanyika leo jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia
Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi Dkt.
Servacius Likwelile amesema fedha zilizopatikana zitasaidia Mpango wa
Matokeo Makubwa Sasa katika Elimu kuboresha ubora wa Elimu ya Msingi na
Sekondari.
Aidha,
Dkt. Likwelile alisema Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa katika Elimu umelenga
pamoja na masuala mengine Kuimarisha ufaulu na kuboresha uwazi shuleni kwa
kupitia upangaji wa shule kitaifa kwa kuzingatia matokeo ya mitihani kwa shule
za msingi na sekondari kwa kuzingatia ubora wa ufaulu na kutekeleza upimaji wa
ujuzi wa stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa darasa la pili katika
shule zilizochaguliwa.
Mpango
huo pia umelenga kutoa motisha kwa shule
zote za Msingi na Sekondari zilizoonyesha maendeleo katika ufaulu na zilizofanya vizuri ili kuboresha viwango vya ufaulu na kutoa motisha zisizo za
kifedha na kuondoa madai ya muda mrefu ya walimu wa shule za Msingi na Sekondari ili Kuondoa malalamiko
ya walimu hao.
Aidha,
Dkt. Likwelile alisema Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa umelenga kuzisaidia shule
na kuondoa ugawaji wa rasilimali usiozingatia usawa kwa kutengeneza na
kusambaza vifaa vya kujifunzia kwa vitendo kwa shule za Msingi na Sekondari,
kuandaa Mafunzo ya KKK kwa walimu wa shule za Msingi, utekelezaji wa programu ya kujenga uwezo wa walimu na
wanafunzi katika ufundishaji na
Ujifunzaji na kuboresha mfumo wa ufuatiliaji wa Ruzuku za Uendeshaji wa Shule.
Akizungumza
katika hafla hiyo, Mwakilishi wa Benki ya Dunia aliipongeza Tanzania kwa kupata
mkopo huo na kuitaka Serikali kutumia vizuri fedha ilizozipata kama ilivyokusudiwa ili kuboresha Elimu nchini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi,
Profesa Sifuni Mchome, ameishukuru Benki ya Dunia kwa fedha itakayotolewa
ambayo itasaidia katika kuhakikisha kuwa utekelezaji wa Mpango wa Matokeo
Makubwa Sasa (BRN) katika sekta ya Elimu unafanikiwa.
Aidha,
Naibu Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Dkt. Deo Mutasiwa
alisema Wizara yake imejiandaa kikamilifu kuhakikisha kuwa fedha zitakazopatikana
zinatumika kama zilivyokusudiwa na kuhakikisha zinawafikia walengwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.