Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dkt. Shukuru Kawambwa ameipongeza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini (VETA) kutokana na mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitatu kati ya mwaka 2011 na 2014. Mafanikio hayo ni pamoja na kuongezeka kwa wanafunzi waliojiunga na mafunzo ya ufundi stadi kutoka 102, 700 mwaka 2011 hadi 159, 345 mwaka 2014, kuongezeka kwa ushirikishwaji wanawake katika nafasi mbalimbali katika elimu ya ufundi stadi kutoka asilimia 35 mwaka 2011 hadi asilimia 42 mwaka 2014 na kuongezeka kwa udahili kwa walimu wa mafunzo ya ufundi stadi ngazi ya cheti kutoka 276 mwaka 2011 hadi 939 mwaka 2014 na ngazi ya stashahada kutoka walimu 34 mwaka 2011 hadi 89 mwaka 2014.
Waziri
Kawambwa alitoa pongezi hizo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa hafla fupi iliyofanyika
jijini Dar es Salaam ya kuwaaga Wajumbe wa Bodi ya Ufundi Stadi ya Taifa
iliyomaliza muda wake ambapo aliyataja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na kukamilika
na kuanza kutekelezwa kwa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (2012/13 -2016/17) wa
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi na kuimarika kwa mifumo mbalimbali
ya Uongozi na Usimamiaji wa Fedha.
Aidha,
Dkt. Kawambwa alisema VETA katika kipindi hicho imeweza kujenga vyuo vipya vya
Mikoa vya Manyara, Lindi, na Pwani. Pia,
kukamilisha ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi - Kipawa ICT na Chuo cha Ufundi
Stadi cha Wilaya cha Makete na Chuo cha
Hoteli na Utalii cha Arusha (VHTTI).
VETA
pia imekamilisha maandalizi ya msingi katika maeneo patakapojengwa vyuo vipya vya Mkoa vya Simiyu, Geita, Njombe
na Rukwa.
Mafanikio
mengine yaliyopatikana ni pamoja na kukamilika na kuanza kutekelezwa kwa sera
na miongozo mbalimbali ya kuwezesha kutolewa elimu na Mafunzo ya ya ufundi
stadi yaliyo bora, kuanzishwa kwa viwango 53 vya stadi za kazi na kuhuishwa kwa mitaala mbalimbali na kuanzishwa
kwa mahusiano na makubaliano mbalimbali kitaifa na kimataifa katika kuendeleza
na kuimarisha elimu na mafunzo ya ufundi stadi.
Pamoja na kutoa pongezi kwa Menejimenti ya
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa mafanikio yote
yaliyopatikana wakati ikiwa chini ya usimamizi wa Bodi iliyomaliza muda wake,
Waziri Kawambwa aliwaasa kuongeza bidii zaidi ili kupata mafanikio makubwa zaidi
ya yale waliyofikia.
“Naiasa
Menejimenti ya VETA kuipa ushirikiano
mkubwa Bodi mpya nitakayoiteua muda si mrefu ili kuelekeza nguvu zao kutatua
changamoto zilizopo,” alisema Dkt. Kawambwa.
“Aidha, bado ufumbuzi unatakiwa wa jinsi ya
kuwapata wakufunzi wenye umahiri wanaotakiwa kutoa mafunzo katika vyuo vyetu
kulingana na hali ya sasa ya mabadiliko ya mara kwa mara ya Sayansi na
teknolojia. Hali ya sasa ya kutegemea
walimu wenye "trade test" au ngazi ya aina moja kufundisha ngazi ile
ile inabidi iepukwe. Lazima mikakati maalumu iandaliwe ya kupata wakufunzi
walio mahiri kutoka vyanzo mbalimbali,” alisema Waziri Kawambwa.
Bodi
ya Ufundi Stadi ya Taifa iliyomaliza muda wake ilikuwa inaongozwa na Profesa
Idrisa Bilal Mshoro na iliingia madarakani tarehe 1 Agosti, 2011 ilipoanza kazi
rasmi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.