Ijumaa, 24 Novemba 2017

Dkt. Akwilapo awataka wahitimu wa ADEM kusimamia kanuni na taratibu katika utendaji kazi.

 Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leornard Akwilapo amewataka wahitimu wa kozi za Uongozi na Usimamizi wa Elimu zinazotolewa na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) kuhakikisha wanasimamia utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka(2014), Sheria, Kanuni na Taratibu za Elimu ili kupunguza migogoro shuleni

Katibu Mkuu ameyasema hayo katika mahafali ya Ishirini na tano (25) yaliyofanyika katika Chuo hicho kilichopo Bagamoyo Mkoani Pwani ambapo amewataka ADEM  kuendelea kusimamia utekelezaji wa Mtaala kwa ufanisi, kutoa takwimu sahihi za shule, kupanga mipango ya maendeleo ya shule inayotekelezeka, kusimamia fedha za elimu bila malipo kwa ufanisi.

Eneo lingine ambalo Katibu Mkuu ametaka litiliwe mkazo ni    pamoja na kudhibiti nidhamu za wanafunzi mara warudipo katika vituo vyao vya kazi.

Dkt. Akwilapo amesema mafunzo ya uongozi na usimamizi wa Elimu pamoja na Ukaguzi wa Shule ni muhimu katika kuwapa uwezo walimu na viongozi wa elimu kufanya kazi zao kwa weledi, ufanisi na kwa kujiamini zaidi hususani katika kipindi hiki cha maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia.

Amewataka wahitimu kuwa chachu ya mabadiliko katika Uongozi na Utawala Bora pamoja na  Uthibiti Ubora wa Shule nchini kwa kutumia ujuzi, maarifa, stadi na mbinu mpya walizozipata katika mafunzo ikiwa ni pamoja na   maarifa waliyoyapata kuyaeneza kwa walimu ambao hawajapata fursa ya kupata mafunzo hayo.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni