Jumanne, 5 Desemba 2017

Chuo cha Ufundi Arusha chatakiwa kukamilisha ukarabati ili kuwezesha vifaa vilivyonunuliwa kutumika.
Naibu waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha amekitaka chuo cha Ufundi cha Arusha kukamilisha ukarabati na upanuzi wa karakana  zake ili kuwezesha vifaa vya kisasa vilivyonunuliwa vianze kutumika.

Naibu waziri Ole Nasha ametoa agizo hilo alipofanya ziara katika Chuo hicho kilichopo mkoani Arusha ili kujionea utendaji kazi, ambapo amesisitiza kuwa serikali ya awamu ya tano imejielekeza katika kuboresha elimu ya ufundi ili kufikia malengo ya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.

Ole Nasha amesema kutokana na umuhimu huo serikali nimeamua kuwekeza katika uboreshaji wa vyuo vinavyotoa Elimu ya ufundi kwa kununua  vifaa vya kisasa na kukarabati miundombinu ya vyuo hivyo ili viweze kuzalisha raslimali watu watakaowezesha nchi kujenga uchumi wa viwanda.

 Naibu waziri amesema chuo hicho kimepata vifaa vya kufundishia na kujifunzia vya kisasa vilivyogharimu kiasi cha shilingi bilioni 14 kutoka nchini Australia ikiwa ni  sehemu ya jitihadi zinazofanywa na serikali ya kuboresha namna ya utoaji wa elimu ya Ufundi kwa lengo kusaidia kuzalisha vijana wengi wenye taaluma ya kisasa katika ufundi.

Ole Nasha amevitaka vyuo vyote vya ufundi kutambua kuwa vina jukumu kubwa la kuwatengeneza vijana watakaokuwa na weledi na umahiri katika kuchangamkia fursa za kazi zitakazokuwa zikipatikana katika miradi mikubwa ya maendeleo.


Kwa upande wake  Kaimu Mkuu wa Chuo Dkt. Erick Mgaya amesema vifaa vya kisasa vilivyonunuliwa vitawezesha kurahisisha zoezi zima la ujifundishaji na ujifunzaji kutokana na kuongezeka kwa udahili. 



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni