Jumamosi, 2 Desemba 2017

Dkt. Semakafu: Simamieni Mfumo wa menejimenti ya viashiria hatarishi.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Avemaria Semakafu amewataka wakurugenzi wa Idara,  wakuu wa Vitengo na Taasisi zilizo  chini ya Wizara kuhakikisha wanasimamia  mfumo wa menejimenti ya viashiria hatarishi ili kudhibiti vishiria hatarishi vinavyoweza kukwamisha malengo ya Wizara kufikiwa.

Dkt Semakafu amesema hayo mjini Morogoro wakati wa kufunga mafunzo ya menejimenti ya viashiria hatarishi yaliyoendehswa na Wizara hiyo kwa lengo la kuwajengea uwezo  watumishi wa wizara hiyo wa ili kuwa na  uelewa wa namna ya kutambua vikwazo vinavyoweza kukwamisha utekelezaji wa majukumu yao.

Naibu Katibu Mkuu Semakafu amesema mafunzo hayo  yataiwezesha Wizara  kuwa na mfumo thabiti wa kushughulikia viashiria hatarishi na hatimae kuwa na daftari linaloainisha viashiria hatarishi pamoja na mikakati ya udhibiti.

Aidha Dkt. Semakafu amewataka Washiriki wote kuhakikisha wanafanyia kazi kikamilifu maudhui yaliyopatikana katika mafunzo hayo ikiwa ni pamoja na kuzingatia miongozo ya Serikali katika kutekeleza shughuli mbalimbali za Wizara.

Pia amemtaka mkaguzi mkuu wa ndani Anna Mhere kuhakikisha anaweka vigezo vya uchaguzi wa waratibu wa viashiria hatarishi katika idara na vitengo ili kupata waratibu ambao kweli watakwenda kutekelezamajukumu yao.

Mafunzo ya menejementi ya Viashiria hatarishi yalianza Novemba 27 na kukamilika Desemba 2, 2017  ambayo yalihusisha Wakurugezi wa Idara, Wakuu wa  Vitengo ndani ya Wizara pamoja na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara, na Wakurugenzi wasaidizi wa Wizara.

Wengine walionufaika na mafunzo hayo ni Wakuu wa Vyuo vya Elimu ya Ualimu, Wathibiti Ubora wa shule  Kanda, Wakaguzi wakuu wa ndani wa Wizara na Taasisi, Wakuu wa Miradi na wajumbe wanne kutoka kila idara na  Vitengo vya Wizara.






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni