Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce
Ndalichako amezitaka Taasisi zinazotoa Elimu ya Juu hapa nchini kufuata
taratibu, Sheria na kanuni za nchi katika kuendesha Taasisi hizo.
Waziri Ndalichako ametoa kauli hiyo hii leo jijini Dar es
Salaam alipofanya ziara ya kushtukiza katika Chuo Kikuu cha Kampla kilichopo
Gongo la Mboto ambapo amebaini kuwepo
kwa idadi kubwa ya watumishi ambao hawana vibali vya Makazi na Ajira.
Waziri Ndalichako amesema Chuo hicho kumekuwa na
udanganyifu wa taarifa za kiutumishi ambapo watu walioajiriwa kama madereva na
wahudumu wamekuwa wakiingizwa katika orodha ya watumishi ambao ni Walimu huku wakijua watumishi hao
hawana sifa za kuwa Walimu.
Waziri Ndalichako amesema baadhi ya walimu katika chuo
hicho kutoka nje ya nchi wanakuja kama wanafunzi lakini wakifika Chuoni hapo
wanahalalishwa na kuwa walimu ambao wanafundisha wanachuo bila kuwa sifa
stahiki.
Profesa Ndalichako pia amekitaka chuo hicho kuhakikisha
kinafuatilia kwa karibu nidhamu ya wanafunzi wanaosoma Chuo hapo kwa
kuhakikisha wanazingatia na kufuata taratibu, kanuni na sheria za nchi.
“Nidhamu ni jambo la
msingi sana, sasa hakikisheni wanafunzi wanaomaliza katika chuo hiki wanakuwa
na nidhamu ikiwa ni pamoja na kuzingatia kanuni na taratibu za ndani na nje ya nchi na siyo vinginevyo, maana kuna
baadhi ya wanafunzi ambao nyaraka zinaonyesha wamemaliza kwenye Chuo hiki na
wako nje ya nchi lakini hawana maadili, liangalieni hili kwa umakini,”alisema
Profesa Ndalichako.
Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dk. Anna
Makakala amezitaka Taasisi zote za Elimu
nchini kuhakikisha zinatoa ushirikiano kwa ofisi hiyo ili kuepuka kukiuka
taratibu na miongozo iliyowekwa na nchi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.