Jumanne, 17 Aprili 2018


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA


Anuani ya simu “ELIMU”
Simu: 026  296 35 33
Baruapepe:info@moe.go.tz
Tovuti: www.moe.go.tzChuo cha Masomo ya  Biashara na Sheria,
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Jengo Na. 10,
S. L. P. 10,
40479 DODOMA.           
Tarehe: 17 Aprili, 2018
TAARIFA KWA UMMA
KUHUSU UFANISI KATIKA USIMAMIZI WA UREJESHAJI WA MIKOPO NA UKUSANYAJI WA MADENI NA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU

A.    UTANGULIZI
Ndugu Waandishi wa Habari, napenda kutumia nafasi hii kuishukuru kwa dhati Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa kufanya ukaguzi huu ambao umeainisha mafanikio na changamoto mbalimbali zilizopo katika Usimamizi na urejeshwaji wa Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu. Pia namshukuru CAG kwa kuibua changamoto ya kuchelewa kwa mradi wa ujenzi katika Chuo cha Ualimu Ndala pamoja na ushauri wake na mapendekezo kwa ujumla aliyoyatoa yenye lengo la kuhakikisha ufanisi katika usimamizi na matumizi ya fedha za umma kwa Wizara na Taasisi zote zilizo chini ya Wizara yangu, unaimarika.


Kwa kuzingatia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha nidhamu inakuwepo katika matumizi ya umma na kuleta matokeo chanya kwa wananchi wake, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia itahakikisha kuwa mapendekezo yaliyotolewa na CAG yanafanyiwa kazi kikamilifu.
Baada ya maelezo hayo ya utangulizi, ningependa kuzungumzia hatua ambazo Wizara yangu imezichukua kutokana na taarifa ya CAG.

B.     HOJA NA MAPENDEKEZO YA CAG

1.      Kuhusu urejeshaji wa mikopo na ukusanyaji wa madeni
Ndugu Wanahabari, taarifa ya CAG imeonesha kuwa makusanyo ya mikopo iliyoiva ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ilikuwa kati ya asilimia 32 na 48 kwa kipindi cha mwaka 2012/2013 hadi 2016/2017.  Taarifa inaonesha pia kuwa kuanzia mwaka 2015/2016 hadi 2016/2017 makusanyo yaliongezeka kutoka shilingi bilioni 28 hadi bilioni 116 ikilinganishwa na kipindi cha kati ya mwaka wa fedha 2012/13 na 2014/15 ambapo makusanyo yalikuwa kati ya Shilingi bilioni 15 hadi shilingi bilioni 22. Ongezeko hili la mwaka mmoja ni zaidi ya asilimia 300. Pamoja na mafanikio hayo yanayotokana na jitihada kubwa inayofanywa na Menejimenti ya Bodi ya Mikopo, CAG ameonesha kuwa bado kiwango cha urejeshwaji hakiridhishi kutokana na kutokuwepo kwa mikakati thabiti ya ukusanyaji wa madeni ya Mikopo.

Wizara imepokea maoni ya CAG na ningependa kuwahakikishia kuwa Serikali inaendelea kuimarisha mikakati yake ya ukusanyaji madeni ya mikopo. Tumeendelea kuchukua hatua ambazo zimeleta tija katika ukusanyaji wa madeni, na tutaendelea kuchukua hatua zaidi kama alivyoshauri CAG.  Kwa mfano, katika mwaka wa fedha 2017/18 hadi kufikia mwezi Machi 2018, jumla ya Shilingi bilioni 132.30 zilikuwa zimekusanywa, hii ni sawa na asilimia 101% ya lengo la mwaka 2017/18, ambalo ni Shilingi bilioni 130. Makusanyo ya mwaka 2016/17 yalikuwa ni shilingi bilioni 116.

2.      Kuwabaini na Kuwadai Wanufaika wa Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
Taarifa ya CAG inaonesha kuwa shughuli za kuwabaini wanufaika wa mikopo hazikufanyika ipasavyo hasa kwa kipindi cha mwaka 2012/2013 na 2014/2015 ambapo kiwango cha kuwabaini wanufaika kilikuwa ni asilimia 28 tu. Udhaifu katika kuwabaini wanufaika ulitokana na mapungufu katika kupanga na kutoa taarifa za kaguzi za kuwabaini wanufaika wa kipindi cha miaka minne yaani kutoka mwaka 2012/2013 hadi 2015/2016.  Pia kulikuwa na udhaifu wa ufuatiliaji wa madeni hata kwa wanufaika ambao walikuwa tayari kurejesha walikuwa hawapatiwi ankara za malipo. Taarifa ya CAG inaonesha kuwa kiwango cha kuwabaini wanufaika kimeongezeka hadi kufikia asilimia 51 kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Pamoja na jitihada zinazoendelea kufanywa na Bodi ya mikopo katika kuwabaini na kuwadai wanufaika, Napenda kutumia fursa hii kuiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kuchukua hatua za haraka kuwabaini na kuhakikisha wanufaika wote ambao hawajaanza kurejesha mikopo yao wanaanza kurejesha mara moja. Vinginevyo hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao. Aidha, Mapendekezo yote ya CAG ya namna yakuimarisha zaidi njia za kuwabaini na kuwadai wanufaika yafanyiwe kazi mara moja.


3.      Uchukuaji wa hatua dhidi ya wadaiwa sugu wa madeni ya mikopo
Ndugu Wanahabari, taarifa ya CAG imeonesha kuwa kulikuwa na udhaifu katika kuwabaini wadaiwa sugu na kwamba kanzidata ya Bodi ya Mikopo ilikuwa inaonesha idadi ndogo sana ya wadaiwa sugu 18 ukilinganisha na hali halisi ya wadaiwa sugu 163,394.  Pia taarifa imeonesha kuwa ni wadaiwa sugu wawili tu ndiyo walikuwa wamefikishwa mahakamani.  Aidha, Bodi haikukusanya kikamilifu faini za waajiriwa 70 waliofikishwa mahakamani na hawakuwatumia ipasavyo wadhamini katika kukusanya madeni kwa wanufaika waliokiuka masharti ya urejeshaji wa mikopo.  CAG amependekeza hatua za kisheria zichukuliwe mara kwa mara kwa wanufaika wanaokiuka masharti ya urejeshaji mikopo.  Pia wadhamini na waajiri wachukuliwe hatua za kisheria wanaposhindwa kutekeleza wajibu wao katika ukusanyaji wa mikopo.

Serikali imepokea maoni ya CAG na inapenda kuuhakikishia umma kuwa hatua za kuimarisha kanzidata ya HESLB tayari zimeshaanza kuchukuliwa. Wadaiwa sugu wameendelea kubainishwa, kutangazwa hadharani na kutakiwa walipe mikopo yao.  Katika mwaka wa fedha 2017/18 jumla ya wadaiwa sugu 147,231 walibainishwa na kutakiwa kujitokeza kulipa mikopo yao, kati yao wanufaika wapatao 42,213 wamejitokeza na kuanza kulipa mikopo yao kwa utaratibu uliowekwa. Wanufaika ambao hawajajitokeza wanaendelea kuhamasishwa, kuelimishwa na kusakwa kupitia kaguzi-endelevu za waajiri na biashara (routine inspections) na kupitia vyanzo vinginevyo mahususi.

Nawasihi wanufaika wote kujitokeza kwa hiari ili kuepuka usumbufu utakaojitokeza kwa kuchukuliwa hatua za kisheria. Nawahimiza Wakurugenzi wa Bodi ya Mikopo kuongeza mikakati ya usimamizi ili kasi ya kuwasaka wadaiwa wote iongezeke. Msisite kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria kwani tayari mmeshafanya kazi kubwa ya kutoa elimu.

4.      Matumizi ya Teknolojia ya kisasa katika kuendesha shughuli za urejeshaji wa mikopo
Taarifa ya CAG imependekeza Bodi ya mikopo iimarishe matumizi ya teknolojia inayofaa kama vile malipo kwa njia ya simu ili kurahisisha mchakato wa urejeshaji wa mikopo na ulipaji wa madeni ya mikopo; na urahisi wa upatikanaji wa taarifa kama vile salio la mkopo na tozo nyingine kama vile faini. 

Serikali imepokea ushauri huo na tayari Bodi ya Mikopo imeingia mkataba na Kituo cha Kompyuta cha Chuo cha Dar es salaam (UCC-UDSM) ambacho kinaendelea na maboresho makubwa ya mifumo ya TEHAMA. Maboresho hayo yanalenga kuifanya mifumo ya utoaji na urejeshaji mikopo kuzungumza na mifumo ya nje kama vile mitandao ya simu ili kuboresha ufanisi hususan katika urejeshaji wa mikopo. Kazi hii itakamilika mwezi Desemba, 2018. Baada ya kukamilika kwa maboresho hayo, wateja wa HESLB wataweza kupata Ankara zao kupitia njia za mtandao. Pia wataweza kurejesha mikopo yao kwa kutumia njia fanisi zaidi za malipo zikiwemo za simu za mkononi (mobile platforms).

5.      Jukumu la Uangalizi katika utekelezaji wa Malengo ya urejeshaji wa mikopo na ukusanyaji wa mikopo
Taarifa ya CAG ilibaini ufuatiliaji hafifu katika kuhakikisha Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inafikia malengo yake ya ukusanyaji mikopo.  Bodi ya Wakurugenzi haikuweka kipaumbele cha kutosha katika mikakati ya urejeshwaji wa mikopo na ukusanyaji wa madeni ya mikopo.  Bodi ya Wakurugenzi haikuchukua hatua zozote kuhakikisha malengo ya ukusanyaji mikopo yanafikiwa.

Wizara inatambua udhaifu mkubwa uliokuwepo katika Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu. Tayari Wizara imechukua hatua za kuimarisha Menejimenti ya Bodi ya Mikopo na kuhakikisha kuwa watendaji walioshindwa kusimamia wajibu wao ipasavyo katika utoaji na urejeshaji wa mikopo wanachukuliwa hatua. Uimarishaji wa Menejimenti umeenda sambamba na uteuzi wa Bodi mpya ya Wakurugenzi iliyoteuliwa mwezi Agosti 2017 ambayo ina wataalamu wenye uzoefu na weledi wa kusimamia majukumu ya msingi ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu. Bodi ya Wakurugenzi imewekewa malengo mahsusi katika kusimamia utoaji, uchakataji na urejeshaji wa mikopo. Aidha, Wizara pia imeweka utaratibu wa kuingia mkataba wa utendaji kazi na Taasisi zote zilizo chini ya Wizara, ikiwemo Bodi ya Mikopo, kwa lengo la kuimarisha uwajibikaji.

6.      Kuchelewa kukamilika kwa Mradi wa Ujenzi wenye thamani ya Shilingi 4,634,441,632.00 katika Chuo cha Ualimu Ndala
Sambamba na ukaguzi wa ufanisi katika usimamizi na urejeshaji wa mikopo, Taarifa ya CAG ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali kwa mwaka unaoishia Juni, 2017 imebainisha kuchelewa kukamilika kwa Mradi wa Ujenzi katika Chuo cha Ualimu Ndala.  Mradi huu umegawanywa katika sehemu kuu mbili (ambazo ni Lot 1 na Lot 2). Ujenzi  wa Lot 1 ambayo ilihusisha ujenzi wa nyumba za walimu, mabweni ya wanafunzi, makataba, maabara na ukumbi wa mihadhara haikuweza kuanza mwaka 2016 kama ilivyotarajiwa kutokana na Mzabuni aliyepatikana kuwa na bei ya juu sana (shilingi 6,082,803,478.00) kulingana na bajeti ya mradi iliyotengwa. Kulingana na Sheria ya Manunuzi, Wizara ilitangaza upya zabuni hiyo ili gharama zake ziendane na fedha zilizotengwa kwa kazi hiyo. Mkandarasi amepatikana kwa bei ya shilingi 4,634,441,632.10. Kazi rasmi za ujenzi zimeanza tarehe 24/02/2018 na zinatarajiwa kukamilika kwa kipindi cha miezi 18 tangu kuanza kwa kazi.

Ili kuhakikisha manunuzi katika yanafanyika kwa kasi nzuri zaidi, Wizara imeiomba Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) ifanye tathmini ya ufanisi na utendaji kazi wa Kitengo cha Manunuzi ili kubaini changamoto zilizopo na kupendekeza namna ya kuongeza ufanisi wa Kitengo hicho. PPRA walianza rasmi kazi hiyo tarehe 26/03/201 na wanatarajia kuikamilisha ifikapo tarehe 28/04/2018.

HITIMISHO

Ndugu Wanahabari,
Napenda kuhitimisha kwa kumshukuru Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa kuanisha maeneo mbalimbali ambayo sisi kama Wizara tunahitajika kuyatathmini na kuyaboresha. Ripoti yake itatusaidia sana katika kuhakikisha kuwa tunafikia lengo letu la kutoa elimu bora kwa ufanisi zaidi. Niendelee kuwaasa watendaji wote ndani ya Wizara yangu kuhakikisha wanazingatia sheria, kanuni na taratibu katika kutekeleza majukumu yao.  Fedha zote za umma zinazoelekezwa kwenye Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia zinapaswa kutumika kwa ufanisi.  Watumishi wote wawe na uzalendo, waweke maslahi ya taifa mbele kuliko kutafuta mianya ya kufanya ubadhirifu wa fedha za umma. Serikali hii ya Awamu ya Tano haitasita kuchukua hatua kwa yoyote atakayekiuka taratibu za fedha na taratibu za utumishi wa umma.

Natoa wito kwa Viongozi wote wa Wizara na Taasisi zilizo chini ya Wizara yangu kupitia kwa makini taarifa za CAG na kufanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa ili kuongeza tija katika kuwatumikia watanzania.

Imetolewa na:
Prof. Joyce L. Ndalichako (Mb)
Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia
17 Aprili, 2018


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni