Jumapili, 27 Mei 2018

ZAIDI YA BILIONI NNE KUTUMIKA KWENYE MIRADI YA UTAFITI.


·         WAZIRI NDALICHAKO ASISITIZA KUWA ZISITUMIKE VINGINEVYO

Serikali imetoa zaidi ya bilioni nne kwa ajili ya Taasisi na Watafiti walioshinda maandiko ya miradi 8 ya utafiti ambayo itaanza kufadhiliwa mwaka huu wa fedha.

Akizungumza jijini Dar es Salaam kabla ya kukabidhi hundi kwa Taasisi zilizoshinda fedha hizo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa. Joyce Ndalichako amesema miradi yote iliyopata fedha ni ile ambayo ina malengo madhubuti ya kuimarisha uchumi wa viwanda hadi ifikapo 2025.

Waziri Ndalichako amesema kufadhiliwa kwa miradi hiyo nane kutaleta mchango mkubwa wa uzalishaji wa dawa nchini na kupunguza uagizwaji wa dawa kutoka nje, uboreshaji wa maabara za uhandishi jeni, kuongeza ushindani wa bidhaa, kuongeza uzalishaji wa mazao, uzalishaji wa mimea, pamoja na kuchangia katika uanzishwaji wa viwanda.
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikabidhi hundi kwa Taasisi na Watafiti walioshinda maandiko ya Miradi ya utafiti unaosimamiwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH)

Waziri Ndalichako amezitaka taasisi zilizopata fedha hizo kuzitumia kwa uadilifu na kwa malengo yaliyokusudiwa na siyo vinginevyo.

Miradi hiyo nane ni pamoja na ule wa umaliziaji wa kiwanda cha uzalishaji wa dawa na maabara ya utafiti ya mabibo, uimarishaji wa miundombinu ya utafiti na ugunduzi wa dawa katika chuo kikuu cha tiba (MUHAS), Muhimbili, ununuzi wa vifaa na uboreshaji wa maabara ya uhandisi jeni ya Taasisi ya Mifugo TALIRI kwa ajili ya kuongeza kasi ya uzalishaji wa mifugo, Uboreshaji wa maabara ya Chanjo ya Taasisi ya Taifa Kibaha.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akipokelewa na baadhi ya watumishi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) mara baada ya kuwasili katika Taasisi hiyo jijini Dar Es Salaam. 

Miradi mingine ni Uboreshaji wa maabara ya udongo, ili kuimarisha Afya ya Udongo kwa ajili ya kilimo endelevu kwa lengo la kuimarisha uchumi wa viwanda, Uboreshaji wa maabara ya kisasa ya utafiti wa mbogamboga na matunda kaskazini mwa Tanzania (HORTI Tengeru), Ukarabati wa mtambo wa utafiti wa kutengeneza mvinyo  katika taasisi ya utafiti wa kilimo, Makutopora na uboreshaji wa usimamizi wa maabara za uchakataji wa mazao ya taasisi ya utafiti wa viwanda TIRDO. 
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH Dk. Amosi Nungu akizungumza na washiriki wa Mkutano wa utoaji wa hundi kwa washindi wa maandiko ya miradi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni