Jumatatu, 21 Mei 2018

EP4R IMEIFANYA SHULE YA SEKONDARI WASICHANA SONGEA KUWA MPYA


Mkuu wa shule ya Sekondari wasichana Songea Tupoke Ndwala amesema shule yake ilipokea zaidi ya milioni Mia mbili kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknlojia kwa ajili ya ukarabati wa mabweni na tayari wamekwisha karabati bweni moja ambalo Lina uwezo wa kuchukua wanafunzi wa kike 115.

Akizungumza na waandishi wa habari Ndwala amesema kabla ya kupokea Fedha hizo kwa ajili ya ukarabati hali ilikuwa mbaya, ikizingatiwa kuwa shule hiyo ni miongoni mwa shule kongwe hapa nchini na hivyo ilikuwa haijafanyiwa ukarabati.

“Kwa kweli naipongeza sana Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa ukarabati huu ambao kwa kweli sasa hivi muonekano wa shule na mabweni umeifanya shule iwe mpya, mandhari ya shule ni nzuri, walimu na wanafunzi ambao ndiyo watumiaji wakubwa wa miundombinu hii kwa kweli wanafurahia pia wanajifunza na kufundisha kwa Amani”, anasema Ndwala ambaye ni Mkuu wa shule hiyo ya Sekondari wasichana Songea.
BWENI la MPUTA ni moja ya BWENI lililokarabatiwa katika shule ya sekondari wasichana Songea, (Songea Girls Secondary School) iliyopo manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma.

Kwa upande wao baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wameelezea kufurahishwa na ukarabati huo na kusema kuwa hivi sasa mabweni yanapendeza hata ukitaka kupiga kumbukumbu ya picha kuonyesha kuwa nilisoma hapa inavutia tofauti na ilivyokuwa awali mabweni yalikuwa  hayavutii. 

Mary Komba anasema awali mabweni kwa maana ya Dari, Sakafu, Vitanda, makabati  na hata rangi iliyokuwa imepigwa ukutani ilikuwa mbaya lakini sasa hivi tumerejea kwenye hali ya nzuri na tunafurahia mno.

“Kwa kweli tunaipongeza sana Serikali ya awamu ya Tano kwa kutuboreshea miundombinu hii ya shule, sasa hivi mabweni yetu ni mazuri na yanapendeza sana hivyo tunaahidi na sisi tutasoma kwa bidii na kufaulu kwa kuwa miundombinu ni mizuri ya kujifunzia”, anasema Mary Komba mmoja wa wanafunzi wa kidato Cha Tano katika shule hiyo.
Muonekano wa sasa wa BWENI la MPUTA baada ya Kufanyiwa ukarabati na fedha zilizotolewa na Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia kupitia programu yake ya lipa kulingana na Matokeo, EP4R.

Katika hatua nyingine timu  ya Maafisa kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na na wanahabari walifika katika shule ya Msingi Tembo Mashujaa na kufurahishwa na namna mwalimu wa darasa la pili alivyokuwa akitumia mbinu za kufundishia za kuimbaa , kucheza na wanafunzi wake kwa lengo la kuwafundisha wanafunzi hao.

Mwalimu Assumpta Banda ambaye anafundisha wanafunzi wa darasa la pili  anasema ualimu ni Wito, nidhamu, uadilifu na upendo kwa wale unaowafundisha na kuwa hayo ndiyo yamekuwa maisha yake na anaipenda sana kazi yake.

“ Mwezi ujao ninastaafu, kazi ya Ualimu ni wito. Madarasa haya ya chini ndiyo Msingi wa Elimu hivyo naishukuru sana Serikali kwa kutupatia mafunzo ya KKK ambapo hivi sasa tunatumia zana na mbinu za kufundishia hali ambayo inarahisisha mwanafunzi kuelewa kwa wepesi na pia watoto wanaoenda shule”, anasema Ndwala.
Ukarabati ukiwa unaendelea katika mabweni mengine katika shule ya sekondari wasichana Songea. Shule hiyo ipo kwenye manispaa ya Songea mkoani Ruvuma

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni