Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa James Mdoe amewataka wanafunzi ambao
wanakipaji cha ubunifu kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi ili waweze kuonyesha
vipaji vyao, kwa kuwa bunifu zao zinatakiwa zitatue changamoto mbalimbali hapa nchini.
Profesa Mdoe ameyasema hayo
leo mkoani Dodoma wakati akifunga jukwaa la Maonesho ya ubunifu kwa vijana
wenye umri kuanzia miaka 13 hadi 21 yanayosimamiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi
na Teknolojia chini ya Mradi wa kukuza Ujuzi, na stadi za kazi, ESPJ.
Kaimu Katibu Mkuu huyo
amesema vijana wabunifu wakiendelezwa vyema watapata fursa ya kuchangia uchumi
wa Taifa kupitia bunifu zao mbalimbali.
Kaimu
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe akizungumza
na wadau mbalimbali wa masuala ya ubunifu wakati akifunga maonesho ya ubunifu
yaliyohusisha wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari kutoka Tanzania bara na
Visiwani, yaliyofanyika mkoani Dodoma.
Kwa upande wake Naibu Katibu
Mkuu Dk. Ave Maria Semakafu akizungumza katika maonesho hayo ametambua mchango
wa kijana Keton Mbwiro ambaye amehitimu Elimu yake ya Msingi na ameweza kubuni kijiko
maalumu cha gari ambacho hutumika kuchimba na kuchota mchanga. Pia amebuni gari
la kubeba vifaa vya ujenzi hivyo ameahidi kuwa kijana huyo atapelekwa shule ya
ufundi ili aweze kujiendeleza.
“Keton Mbwiro ni kijana
mdogo lakini ameweza kubuni kitu ambacho miaka ya nyuma tulizoea kuona vitu vya
namna hii vinafanywa na wanafunzi wa vyuo vikuu, hivyo uwezo wake lazima
tuuendeleze kwa kuhakikisha anakwenda shule ya Ufundi, pia ni vyema watanzania
tukaachana na dhana ya kuwa vyuo vya ufundi ni vya useremala pekee bali ni
zaidi ya hapo.” anasema Dk. Semakafu.
Kaimu
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe akiwa na
baadhi ya watendaji wa Wizara hiyo wakiangalia moja ya ubunifu uliohusisha
mashine ya kusafishia/kuondoa uchafu kwenye mazulia. Maonesho hayo yamefanyika katika
Chuo Kikuu cha Dodoma, Mjini Dodoma.
Mradi wa kukuza Ujuzi na
Stadi za kazi, ESPJ ni mradi wa miaka miatano ambao unatekelezwa kwa
ushirikiano wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Benki ya Dunia,
lengo likiwa ni kuhakikisha mkakati wa Serikali wa Tanzania kuwa
nchi ya Uchumi wa viwanda
mpaka 2025 inatimia.
Prof.
James Mdoe ambae ni Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia akiwa
ameshika chupa yenye dizeli iliyotokana na kuyeyushwa kwa chupa za plastiki
ambazo zimekwisha matumizi yake.