Ijumaa, 15 Desemba 2017

Ole Nasha aitaka Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kuandaa Wataalamu katika fani za ufundishaji na ujifunzaji

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha ameiagiza Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kurejea jukumu lake la msingi la kuwaandaa wataalamu katika fani za Elimu ya Watu Wazima na Maendeleo ya Jamii.
Naibu Waziri ametoa agizo hilo katika mahafali ya 53 ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima yaliyofanyika katika viwanja vya Taasisi hiyo jijini Dar es Salaam, ambapo amesema kwa kufanya hivyo kutasaidia kutatua  changamoto za ufundishaji na ujifunzaji wa stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesaba  (KKK) kwa vijana na watu wazima.

Naibu Waziri Ole Nasha amesema Wizara tayari ilishatoa Mwongozo wa shule za Msingi na Sekondari  kutumika kama vituo vya kutolea Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo rasmi, wakati utaratibu wa kuvitumia Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi FDC ukiwa unaendelea.

Mheshimiwa Ole Nasha amesema serikali kwa kushirikiana na wadau imeendelea kutekeleza Mipango mbalimbali ambayo inawawezesha vijana na watu wazima waliokosa fursa katika Mfumo Rasmi wa Elimu kujiendeleza kielimu na kumudu changamoto za maisha.

Naibu Waziri Ole Nasha amewataka wahitimu kwenda kufanya kazi kwa weledi katika vituo watakavyopangiwa ili kusaidia juhudi za Serikali za kupambana na adui ujinga.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Dkt. Fidelice Mafumiko amesema Taasisi i naendelea kuongeza fursa zaidi katika utoaji Elimu kwa kupitia programu za mafunzo kwa kutumia njia ya ujifunzaji huria na masafa kwa ngazi ya Stashahada.


Dtk. Mafumiko amasema hadi sasa Taasisi imeongeza vituo  vya mafunzo vya Elimu ya Watu Wazima  kutoka vituo 13 hadi kufikia 21 katika mikoa13.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.