Jumatatu, 6 Agosti 2018

AWAMU YA PILI MAFUNZO UTHIBITI UBORA YAANZA KATIKA KANDA TANO


Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeanza awamu ya pili ya kutoa mafunzo kwa Wathibiti Ubora  wa shule kwa Kanda za Dar es Salaam, Arusha, Moshi, Morogoro  na Mtwara juu ya  kutekeleza mfumo mpya wa Uthibiti ubora wa shule.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo ya wathibiti ubora mkoani Arusha Naibu Waziri William Ole Nasha amewataka watumishi hao kusimamia mfumo na mxhakato wa utoaji wa Elimu kwa kuhakikisha Sera, kanuni , sheria na mongozo inazingatiwa na wadau wote katika sekta ya Elimu.

Naibu waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William ole Nasha akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua mafunzo ya wathibiti ubora awamu ya pili yanayoendelea nchini.

 Naibu waziri ole Nasha amewataka wathibiti ubora kuhakikisha dhamira ya serikali inatimizwa kwa wathibiti ubora wa shule kuhama kutoka katika dhana ya ukaguzi kama wajuaji zaidi, au polisi kwa kukagua zaidi na badala yake wawe wathibiti ubora wa shule  kwa kuhakikisha kuwa wanawasaidia walimu, kwa lengo la kuhakikisha serikali inafikia malengo ya kuwa na uchumi wa viwanda.


Kwa upande wake  Mkurugenzi wa Uthibiti Ubora wa wizara hiyo, Euphrasia Buchuma amefungua mafunzo hayo jijini Dar es Salaam ambapo amewataka Wathibiti Ubora kuzingati mafunzo yanayotolewa ili kuwawezesha kufanyia kazi  yale yote yanayoelekezwa.
Baadhi ya washiriki wa Mafunzo Elekezi ya Mfumo Mpya wa Uthibiti Ubora wa Shule wakimsikiliza Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Euphrasia Buchumu (Hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yanayofanyika katika ukumbi wa shule ya sekobdari Zanaki Jijini Dar es Salaam

Buchuma amesema mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha wathibiti ubora wa shule kuweza kufanya  ukaguzi wa shule kwa kutumia mfumo mpya ambao ni shirikishi unaoangalia zaidi tendo la kujifunza, kufundisha na kufanya upimaji katika ngazi ya darasa.

Akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo  mthibiti ubora wa shule  kutoka Manispaa ya Ilala Diana Justine amesema mafunzo hayo yatawawezesha kutatua changamoto wanazokuta nazo  shuleni kwa kushirikiana na walimu, wanafunzi na jamii tofauti na awali walipokuwa wanakwenda kuangalia matatizo bila kutoa suluhisho la matatizo hayo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.