Alhamisi, 23 Agosti 2018


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA

    Anuani ya simu “ELIMU”
   Simu: 026  296 35 33
   Baruapepe:info@moe.go.tz
   Tovuti: www.moe.go.tz
  



  
     Chuo cha Masomo ya 
     Biashara na Sheria,
     Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Jengo Na. 10,
     S. L. P. 10,
     40479 DODOMA.           

   
TAARIFA KWA UMMA

KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA BODI YA KITAALAMU YA WALIMU TANZANIA

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Agosti 21, 2018 imewasilisha maelezo kuhusu Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalamu ya Walimu Tanzania katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Jijini Dodoma.
Muswada wa Sheria hii unalenga kuanzisha Bodi ya Kitaalam ya Walimu Tanzania itakayosimamia utaalamu wa ualimu nchini kwa walimu wote walio katika Utumishi wa Umma na Sekta Binafsi kuanzia walimu ngazi ya Astashahada, Stashahada na Shahada.

Pamoja na mambo mengine, Bodi itakayoundwa kwa Sheria hiyo: itasajili, itaweka viwango vya ubora wa ualimu, itasimamia maadili na miiko ya ualimu ya kitaalamu, itafanya tafiti kuhusu masuala ya utaalam wa ualimu na kusimamia maendeleo ya utaalamu wa ualimu kwa ujumla.

Uanzishwaji wa Bodi hiyo ni utekelzaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 inayohimiza Serikali kuhuisha Mfumo na Muundo wa Uongozi, Usimamizi na Uendeshaji wa Sekta ya Elimu ili uwe na tija na uwajibikaji, na kuhakikisha kuwa maadili na haiba ya walimu yamezingatiwa katika ngazi zote za elimu na mafunzo.

Inatarajiwa kwamba, baada ya Sheria inayopendekezwa kutungwa na kutekelezwa ipasavyo, matokeo yafuatayo kupatikana:

a) Walimu wote nchini kutambuliwa na kusajiliwa na chombo cha kitaalamu, hivyo kuwepo kwa mfumo madhubuti wa kushughulikia walimu watakao kwenda kinyume na maadili ya utaalamu wa ualimu.
b) Kuwa na mfumo mzuri wa usimamizi, uthibiti na uendelezaji wa utaalamu wa ualimu.
c)  Kulindwa kwa hadhi ya taaluma na utaalamu wa ualimu kwa kuzuia watu wasiokidhi vigezo na viwango stahiki kufanya kazi ya ualimu.
d)Walimu waliopo katika utumishi wa ualimu kuwa na sifa kulingana na matakwa ya Sheria inayopendekezwa, na hivyo jamii kupata elimu yenye viwango stahiki.

Muswada tajwa unatarajiwa kusomwa kwa mara ya pili na ya tatu katika Mkutano wa Kumi na Mbili (12) wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaotarajiwa kuanza Septemba 4, 2018.  
Wizara inawakaribisha wananchi kushiriki kikamilifu katika hatua zote za utungwaji wa Sheria hii ili kuweza kupata Sheria bora kwa maslahi mapana ya walimu na nchi kwa ujumla.

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
21/8/2018





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni