Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imewasilisha
mapendekezo ya Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalamu ya Walimu Tanzania kwenye
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.
Akiwasilisha mapendekezo hayo
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa William Ole Nasha
amesema Bodi hiyo itasimamia usajili, weledi na maadili ya kitaalamu ya walimu
katika sekta ya umma na binafsi.
Naibu Waziri amesema kupitia bodi
hiyo Pia itainua hadhi ya taaluma ya ualimu kwa kusajili walimu wote
kulingana na viwango vya ubora wa ualimu na kuwapa leseni ya kufundisha
katika ngazi stahiki.
Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William Ole Nasha akiwasilisha Mapendekezo ya Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalamu
ya Walimu kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii
Jijini Dodoma
Pia kupitia bodi hiyo ya
kitaalamu itakuwa na jukumu la kuimarisha utaalamu wa walimu kwa kuchochea ari
ya kujiendeleza kitaalamu miongoni mwa walimu na kuongeza fursa za ajira
katika soko la ndani na nje ya nchi.
Naibu Waziri Ole Nasha amesema
utaalamu wa ualimu hapa nchini umekuwa ukisimamiwa na vyombo mbalimbali ambavyo
vililenga kwenye ajira, maslahi ya walimu na maadili ya walimu kiutumishi huku
masuala ya usimamizi na maendeleo ya utaalamu wa ualimu kutokuwa na sheria na
chombo mahususi cha kuyasimamia.
Amesema kuundwa kwa Bodi
mahsusi ya kusimamia Utaalamu wa Walimu ni suala la msingi katika kuinua ubora
wa Elimu nchini na suala hili limezingatiwa kwenye Sera ya Elimu na Mafunzo ya
mwaka 2014 iliyotamka bayana kuwa Serikali itahuisha Mfumo na Muundo wa
Uongozi, Usimamizi na Uendeshaji katika Sekta ya Elimu ili uwe na tija na
uwajibikaji.
Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William Ole Nasha akiwasilisha Mapendekezo ya Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalamu
ya Walimu kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii
Jijini Dodoma
Pia Sera hiyo imetamka kuwa
Serikali itahakikisha kuwa maadili na haiba ya ualimu na watumishi wengine
yanazingatiwa katika ngazi zote za Elimu na mafunzo hivyo kuanzishwa kwake kuna
tija katika usimamizi wa Utaalamu wa Ualimu.
Walengwa wa Bodi ya Kitaalam ya
Walimu Tanzania inayopendekezwa itamhusu mtu yeyote aliyefuzu mafunzo ya
ualimu katika Chuo cha Ualimu au Chuo Kikuu kinachotambuliwa na mamlaka husika
katika ngazi ya Astashahada, Stashahada, Shahada, Shahada ya Uzamili na Uzamivu.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William Ole
Nasha akiwa na Viongozi Wakuu wa Wizara, Wakurugenzi na watumishi wengine wa
Wizara wakiwasili katika viwanja vya Bunge kwa ajili ya kuwasilisha Mapendekezo
ya Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalamu ya Walimu kwenye Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.