Jumanne, 28 Agosti 2018

WAZIRI NDALICHAKO AWATAKA WALIMU WA DARASA LA KWANZA NA LA PILI KUONESHA UMAHIRI KATIKA KUFUNDISHA STADI ZA KKK


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amewataka walimu walioshiriki mafunzo ya kujengewa uwezo wa kumudu Stadi za Kusoma Kuandika na Kuhesabu (KKK) kuonesha umahiri unaotakiwa katika kufundisha Stadi hizo ili kuleta mabadiliko chanya miongoni mwa wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili pindi watakaporejea katika vituo vyao vya kazi.

Waziri Ndalichako ameyasema hayo mkoani Morogoro wakati akifunga mafunzo hayo ambapo amesema pamoja na mambo mengine ana imani kuwa kupitia mafunzo hayo walimu wa darasa la kwanza na la pili wameongeza mbinu ambazo watazitumia kuwafundishia wanafunzi waweze kumudu stadi hizo kwani ndio msingi bora wa kumudu masomo yanayofundishwa kwenye darasa la tatu hadi darasa la saba.

“Nyumba imara hujengwa na msingi imara hivyo mafunzo haya ni muhimu sana kwenu walimu mnaofundisha Darasa la kwanza na la pili ili muweze kuwaandaa wanafunzi kumudu vyema masomo katika ngazi za Elimu zinazofuata” Alisisitiza Ndalichako

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiongea na walimu (hawapo pichani) wakati wa kufunga mafunzo ya uimarishaji wa Stadi za KKK. Amewataka walimu hao kutumia mbinu walizopata, upendo na hamasa kuwafundisha watoto ili wapate ujuzi na maarifa yatakayoleta tija katika Taifa

Waziri Ndalichako alisema lengo la Serikali ni kuendelea kuwapatia walimu wengi mafunzo ya ufundishaji wa Stadi za KKK pamoja na mbinu zingine za ufundishaji.

“Mtakumbuka Agosti 18, 2018 nilizindua matumizi ya Vikaragosi katika kufundisha Stadi za Kusoma Kuandika na Kuhesabu kwa Wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili jijini Dar es Salaam, hizi zote ni juhudi za Serikali kuhakiksha ufundishaji unaimarika na wanafunzi wanaelewa” Aliongeza Waziri Ndalichako
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akipokea Kitabu cha Picha kama zawadi kutoka kwa walimu walioshiriki mafunzo ya kuimarisha Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) katika Chuo cha Ualimu Morogoro, Mjini Morogoro.

Katika hatua nyingine Waziri Ndalichako amewataka Walimu wote nchini kuunga mkono juhudi za serikali za kuunda bodi ya utaalamu wa walimu kwa kuwa ina lengo la kuutambua ualimu kama taaluma na utaalamu ikiwa ni pamoja na kulinda hadhi ya mwalimu.

Mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kumudu Stadi za KKK yanatolewa kwa walimu 1600 wa mikoa ya Dar es Salaam, Geita, Kagera, Mwanza na Tanga ambayo shule zake zina mkondo zaidi ya mmoja. 
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akigawa cheti kwa mmoja wa walimu walioshiriki mafunzo ya uimarishaji wa Stadi za KKK wakati wa kufunga mafunzo hayo yaliyofanyika katika Chuo cha Ualimu Morogoro, Mkoani Morogoro.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni