Jumatano, 15 Agosti 2018

SERIKALI KUJENGA MAJENGO MAPYA CHUO CHA UALIMU SUMBAWANGA

Serikali imesema itajenga majengo mapya ya Chuo cha Ualimu Sumbawanga ili kukihamisha kutoka  kwenye majengo ya Kanisa Katoliki ambayo yamekuwa yakitumika kwa muda.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akiwa mkoani  Rukwa kwenye ziara  ya kukagua miradi ya Elimu inayotekelezwa katika mikoa ya Rukwa na Katavi ambapo amesema kwa sasa ni vigumu kufanyia ukarabati majengo yanayotumika kwa sababu si maliya serikali.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na Wanachuo, Wakufunzi na Wafanyakazi wa Chuo cha Ualimu Sumbawanga (Hawapo pichani) ambapo serikali imeahidi kujenga majengo mapya kwa ajili ya Chuo cha Ualimu Sumbawanga

Waziri Ndalichako amesema suala la uboreshaji wa miundombinu ya chuo hicho lipo ingawa changamoto iliyopo ya eneo pamoja na majengo kuwa si mali ya chuo hicho na kwamba kanisa Katoliki wanalihitaji eneo hilo kwa matumizi mengine.

“Chuo Cha Ualimu Sumbawanga hakijasahaulika katika kufanyiwa ukarabati, changamoto iliyopo ni kuwa eneo hili mlikaribishwa lakini mkang’ang’ania sasa wenyewe wanataka eneo lao ” alisisitiza Waziri Ndalichako.

Aidha Waziri amesema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/19 kiasi cha shilingi bilioni 36 kimetengwa kwa  ajili ya kuvifanyia ukarabati vyuo saba vya Ualimu, huku Chuo Cha   Ualimu Murutunguru na Kabanga vikitarajia kujengwa upya.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akipokea taarifa ya Mkoa wa Rukwa kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Khalifan Haule mara baada ya kufanya ziara ya Kikazi katika mkoa huo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo amesema anawashukuru Kanisa Katoliki jimbo la Sumbawanga kwa kuruhusu Chuo hicho kufanya shughuli zake katika eneo lake kwa muda mrefu, kwani mwanzoni kanisa hilo lilijenga majengo hayo ili kwa lengo la kuanzisha chuo cha kilimo.

Mkuu huyo wa mkoa amesema tayari  mkoa wake umeshatafuta eneo lingine ambalo Chuo hicho kitahamishiwa, na kuwa hivi sasa tayari Mkoa  umesharatibu taratibu  za kuanza kulipa fidia kwa wakazi ambao eneo Lao litachukuliwa kwa ajili ya matumizi ya Chuo hicho.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo akimuonyesha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako baadhi ya majengo ya Chuo cha Ualimu Sumbawanga









Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.